Ugonjwa wa kipindupindu, kuharisha ulivyowatesa Watanzania mwaka 2025

  • Ugonjwa wa kuharisha ulikuwa ni ugonjwa ama hali iliyoripotiwa zaidi mwaka 2025 katika mikoa yote ya Tanzania

Dar es Salaam. Huenda Watanzania wakatakiwa kuchukua tahadhari za kiafya zaidi ili kujikinga na magonjwa ya kipindupindu na kuharisha ambayo takwimu za hivi karibuni za Wizara ya Afya zinayataja kuwasumbua zaidi wananchi mwaka 2025.

Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) kuharisha ni hali ya kiafya inayohusisha kujisaidia choo chepesi zaidi kuliko kiwango cha kawaida kwa zaidi ya mara tatu kwa siku, hali ambayo huchangiwa zaidi na maambukizi ya bakteria na virusi vinavyoathiri mfumo wa mmeng’enyo wa chakula.

Wakati mwingine kuharisha, hutajwa kuwa miongoni mwa dalili za ugonjwa wa kipindupindu unaosababishwa na bakteria aitwaye Vibrio cholerae, ambao kwa miaka ya nyuma ulitajwa kuchangia idadi kubwa ya vifo.

Takwimu za Mfumo Jumuishi wa Ufuatiliaji na Udhibiti wa Magonjwa (IDSR), zilizotolewa Februari 2, 2026 na Wizara ya Afya zinabainisha kuwa karibu nusu ya visa vyote 369,864 vya magonjwa yanayoripotiwa nchini vinatokana na ugonjwa wa kuharisha.

Visa 176,797 vilihusishwa na magonjwa ya kuharisha, sawa na asilimia 47.8 ya visa vyote vilivyoripotiwa katika robo ya kwanza na ya pili ya mwaka 2025.

Kila mtu hupata kuhara mara kwa mara, lakini inapodumu zaidi ya wiki nne, huchukuliwa kuwa kuhara sugu. Picha/ Gastro florida.

Takwimu hizo zinaonesha kuwa karibu mgonjwa mmoja kati ya wawili waliokwenda katika vituo vya afya alikuwa anakabiliwa na tatizo la kuharisha kutoka mikoa yote 26 ya Tanzania Bara.

Miongoni mwa mikoa iliyoongoza kwa visa vingi vya kuharisha ni Dodoma yenye visa 13,770 (asilimia 7.8), ikifuatiwa na Mara visa 13,622 (asilimia 7.7), Morogoro visa 11,879 (asilimia 6.7) na Rukwa visa 11,494 (asilimia 6.5). 

Mwezi wa Mei uliongoza kwa idadi kubwa ya visa, ambapo viliripotiwa visa 78,496 sawa na asilimia 21.2  ya visa vyote ikichangia vifo 33.

Mbali na Kuharisha kipindupindu pia kiliwatesa Watanzania mwaka 2025, visa 3,433  na vifo 26, sawa na asilimia 78.8 ya vifo vyote vikiripotiwa.

Nimonia, ‘typhoid’ pasua kichwa

Ripoti ya Wizara ya Afya inayataja magonjwa mengine yaliwasumbua Watanza ndani ya mwaka 2025 kuwa ni ugonjwa wa nimonia ambapo visa 133,310 vilirekodiwa ikifuatiwa na homa ya matumbo (typhoid) uliokuwa na visa 31,760.

Pneumonia ni maambukizi ya papo hapo ya njia ya hewa yanayohusisha alveoli na njia za hewa za mbali. Picha/ Dr J Suri.

Pia, kulikuwa na visa 12,062 vya kung’atwa na wanyama na visa 6,183 vya kung’atwa na nyoka, maambukizi makali ya njia ya hewa (SARI) yalishika nafasi ya sita kwa visa 4,213 pamoja na vifo saba vilivyoripotiwa.

Homa ya dengue pia yenye visa 84 na kichaa cha mbwa (rabies) kilichokuwa na visa 25 kiliingia katika orodha hiyo ya magonjwa 10 yaliyowatesa Watanzania suala linaloacha mzigo mkubwa wa udhaifu wa mwili kwa wananchi.

Ufaulu kidato cha nne unavyopanda na kushuka Tanzania

  • Takwimu zinaonesha ufaulu unashuka na kuongezeka  mwaka hadi mwaka katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba, 2025, ambapo ufaulu umeongezeka kidogo kulinganisha na miaka iliyopita.

Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo Januari 31, 2026 amesema kuwa ufaulu wa wanafunzi kwa kidato cha nne kwa mwaka 2025 ni asilimia 92.37. 

Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari unaonyesha kuwa ufaulu wa kidato cha nne umekuwa ukipanda na kushuka kwa miaka tofauti katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021.

Takwimu zinaonyesha kiwango cha ufaulu kiliongezeka kwa asilimia 0.67 na kufikia asilimia 87.79 mwaka 2022 kutoka asilimia 87.30 iliyorekodiwa mwaka 2021. Hata hivyo, ufaulu huo ulishuka kwa asilimia 0.32 na kufikia asilimia 87.65 mwaka 2023.

Ongezeko thabiti la matokeo ya kidato cha nne limeonekana kuanzia mwaka 2024 ambapo ufaulu uliongezeka kwa takriban asilimia 4.72 na kufikia asilimia 92.37.

Aidha, katika kipindi cha miaka mitano wavulana ndio wanaongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu zaidi ya wasichana wakiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 92.75 wakiwaacha mbali wasichana wenye wastani wa asilimia 90.71.

WHO yatoa mwongozo mpya wa lishe mashuleni kudhibiti unene uliopitiliza

  • Takribani watoto na vijana milioni 188 wa umri wa kwenda shule waliishi na unene uliopitiliza 2025.
  • Ni nchi 48 pekee kati ya 408 zilizo na sera zinazozuia matangazo ya vyakula visivyofaa kwa watoto.

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetoa mwongozo mpya wa kimataifa wa lishe mashuleni, unaoziitaka nchi wanachama kuimarisha mazingira ya lishe shuleni ili kudhibiti ongezeko la unene uliopitiliza na kukabiliana na changamoto ya utapiamlo kwa watoto.

Uzito au unene uliopitiliza hufafanuliwa kama mkusanyiko usio wa kawaida au wa kupita kiasi wa mafuta mwilini ambao unaweza kuweka afya hatarini ikichangiwa zaidi na mtindo mbovu wa maisha, ulaji usiozingatia kanuni za afya na tabia bwete.

Takwimu za WHO zinakadiria kuwa mwaka 2024 takribani watoto milioni 35 walio chini ya umri wa miaka mitano duniani kote walikuwa na uzito uliopitiliza suala linaloweka afya zao rehani.

Hali ni mbaya zaidi kwa watoto na vijana milioni 188 wenye umri wa kwenda shule ambao waliripotiwa na WHO kuwa na unene uliopitiliza, sawa na mtoto mmoja kati ya 10, idadi iliyozidi kwa mara ya kwanza watoto wenye uzito pungufu.

WHO inapendekeza shule ziweke kanuni za lazima zitakazohamasisha upatikanaji wa vyakula vyenye afya. Picha/Canva.

Kutokana na uwepo wa changamoto hiyo, January 27, 2026, WHO ilitoa mwongozo wa lishe mashuleni utakaohakikisha vyakula na vinywaji vinavyotolewa shuleni, pamoja na vinavyopatikana katika mazingira yanayozunguka shule, ni vyenye afya na lishe bora.

“Uzito kupita kiasi na unene uliokithiri kwa watoto vinaendelea kuongezeka duniani, huku utapiamlo bado ukiwa changamoto ya kudumu. Shule ziko mstari wa mbele katika kukabiliana na mzigo huu maradufu wa utapiamlo,” inaeleza sehemu ya taarifa ya WHO.

Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dk Tedros Adhanom Ghebreyesus aliyekuwa akizunngumza alisema kuwa lishe shuleni ina athari ya moja kwa moja katika afya na maendeleo ya watoto.

“Chakula ambacho watoto hula shuleni kinaweza kuathiri uwezo wao wa kujifunza na kuwa na madhara ya muda mrefu kwa afya na ustawi wao. Lishe sahihi shuleni ni msingi wa kuzuia magonjwa baadaye maishani,” alisema.

Takribani mtoto mmoja kati ya 10 duniani ana unene uliopitiliza. Shule zinaweza kuwa sehemu ya kutatua tatizo hili. Picha/ Canva.

Katika muktadha wa kitaifa, baadhi ya nchi ikiwemo Tanzania, tayari zina miongozo ya chakula cha shule inayolenga kuboresha lishe kwa wanafunzi kupitia Mpango wa Taifa wa Chakula Shuleni (NSFG).

Mpango huo unazingatia Sera ya Afya ya mwaka 2007, Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 na Mpango wa Taifa wa Sekta Jumuishi wa Miaka Mitano wa Utekelezaji wa Lishe 2016/17 hadi 2020/2.

Kwa mujibu wa Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia, utoaji wa huduma za chakula shuleni huchangia kuboresha afya ya wanafunzi, kupunguza utoro, kuongeza usikivu darasani na kuinua kiwango cha ufaulu.

WHO inakadiria kuwa zaidi ya watoto milioni 466 duniani hupata chakula kupitia programu za chakula shuleni jambo linaloimarisha afya ya akili na kuimarisha uwezo wao wa kimasomo.

Kuongeza vyakula vyenye afya na kupunguza vyenye sukari na mafuta yasiyo na afya ni hatua muhimu ya kuwalinda watoto. Picha/ Canva.

Hata hivyo, shirika hilo linaonya kuwa bado kuna upungufu wa taarifa kuhusu ubora wa lishe ya chakula hicho, hali inayoweza kusababisha changamoto za kiafya.

Katika mwongozo wake mpya, WHO inapendekeza shule ziweke kanuni za lazima zitakazohamasisha upatikanaji wa vyakula vyenye afya na kupunguza matumizi ya vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi na mafuta yasiyo na afya, pamoja na kudhibiti mbinu za kibiashara zinazowalenga watoto.

Kwa sasa, nchi 104 zina sera za chakula chenye afya mashuleni huku karibu robo tatu zikiwa na vigezo vya lazima vya kuongoza muundo wa chakula cha shule huku nchi 48 pekee zikizuia matangazo ya vyakula vyenye sukari nyingi, chumvi au mafuta yasiyo na afya.

Sekta ya fedha inavyoimarika Tanzania

  • Ukuaji huo umejidhihirisha kupitia ongezeko la idadi ya benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, mawakala wa benki pamoja na rasilimali za kibenki.

Dar es Salaam. Katika siku za hivi karibuni, sekta ya fedha nchini Tanzania imeendelea kuonesha mwelekeo chanya wa ukuaji, ikichochewa na kuongezeka kwa shughuli za kiuchumi, upanuzi wa taasisi za kifedha na kuimarika kwa imani ya wananchi katika mifumo rasmi ya fedha. 

Ukuaji huo umejidhihirisha kupitia ongezeko la idadi ya benki, taasisi za huduma ndogo za fedha, mawakala wa benki pamoja na rasilimali za kibenki, hali inayoashiria kuimarika kwa mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa taifa.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri wa Fedha, Laurent Luswetula aliyekuwa akizungumza Januari 21, 2025 katika uzinduzi maadhimisho ya kitaifa ya wiki ya huduma ya fedha, amesema hadi kufikia Septemba 2025, Tanzania ilikuwa na jumla ya benki za kibiashara 35, benki za kijamii mbili, benki za maendeleo mbili pamoja na benki tatu za huduma ndogo za fedha. 

Aidha, taasisi 2,811 za huduma ndogo za fedha pamoja na vikundi vya kijamii vya huduma ndogo za fedha 70,913 zilisajiliwa, huku taasisi mbili za ubadilishanaji wa fedha zikiongeza idadi ya watoa huduma rasmi nchini.

Aidha, Luswetula ameeleza kuwa upanuzi huo umeenda sambamba na ongezeko kubwa la mawakala wa benki nchini. Ambapo Idadi ya mawakala wa benki imeongezeka kutoka 106,176 hadi kufikia 145,430, jambo linalorahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha hadi ngazi ya jamii.

Mbali na ongezeko la taasisi, rasilimali za kibenki nazo zimeendelea kuimarika na kufikia Sh71.8 trilioni Septemba 2025, ikilinganishwa na Sh62.2 trilioni zilizorekodiwa Septemba 2024.

Aidha, katika kipindi kama hicho, amana za benki zimeongezeka hadi Sh50.2 trilioni kutoka Sh42.7 trilioni mwaka uliotangulia, hatua inayotafsiriwa kama ishara ya kuongezeka kwa imani ya wananchi katika sekta ya fedha.

Katika maelezo yake, Luswetula pia amebainisha kuwa mikopo kwa sekta binafsi imekua kwa kasi kubwa. Ikiongezeka na kufikia Sh42 trilioni mwaka 2025 kutoka Sh35 trilioni mwaka 2024, sawa na ukuaji wa asilimia 24.

Hata hivyo, pamoja na ongezeko la mikopo, amebainisha kiwango cha mikopo chechefu bado kiko katika hali inayodhibitiwa. 

“Mikopo chechefu imeongezeka kwa asilimia 2.78, kiwango ambacho bado kipo ndani ya ukomo wa kisheria wa asilimia tano,” ameeleza Luswetula.

Soko la hisa laongezeka 

Kwa upande wa sekta ndogo ya mitaji na dhamana, Luswetula amesema Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE) limeendelea kukua ambapo kuonesha ukuaji idadi ya kampuni zilizosajiliwa katika soko hilo imefikia 28 huku mifuko ya uwezeshaji ikifikia 21.

Aidha, ameainisha kuwa thamani ya uwekezaji katika masoko ya mitaji ilifikia Sh63.7 trilioni katika kipindi kilichoishia Desemba 2025.

“Jumla ya mauzo ya hisa na hati fungani katika soko la hisa la Dar es Salaam yamefikia Sh6.87 trilioni vilevile thamani ya mifuko ya uwekezaji wa pamoja ilifikia Sh4.35 trilioni katika kipindi hicho,” ameongeza Luswetula.

Fahamu mahitaji ya usingizi kwa watoto wachanga

  • Usingizi ni muhimu sana kwa ukuaji wa mwili na akili ya mtoto.

Dar es Salaam. Usingizi ni miongoni mwa mahitaji muhimu kwa binadamu, hususan watoto wachanga katika miaka miwili ya mwanzo ya maisha yao.

Tofauti na watu wazima, watoto huhitaji muda mwingi zaidi wa kulala ili kuwawezesha kukua vizuri na kuimarisha uwezo wa ubongo kufanya kazi kwa ufanisi.

Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya ya Stanford Medicine Children’s Health, watoto wachanga huhitaji hadi saa 17 za usingizi kwa siku, ambazo hugawanyika katika vipindi mbalimbali.

“Ratiba ya usingizi wa mtoto ni muhimu sana kwa ukuaji wake wa mwili, maendeleo ya akili (kumbukumbu, kujifunza na umakini), udhibiti wa hisia, pamoja na ujuzi wa mwendo wa mwili,” inaeleza tovuti hiyo.

Tovuti hiyo inabainisha kuwa watoto wenye umri wa kuanzia siku moja hadi miezi mitatu ya mwanzo wanahitaji kulala wastani wa saa 16 hadi 17 kwa siku, lakini mara nyingi hawalali zaidi ya saa 1 hadi 2 kwa wakati mmoja.

Aidha, watoto wenye umri wa miezi minne hadi 12 wanahitaji kulala wastani wa saa 12 hadi 16 kwa siku, huku wale wenye umri wa mwaka mmoja hadi miaka miwili wakihitaji kulala kati ya saa 11 hadi 14 kwa siku.

Tanzania kinara idadi ya Simba Afrika

Shirika la World Population Review limeitaja Tanzania kuwa na simba 14,500 idadi inayoifanya kuwa kinara wa idadi kubwa ya Simba barani Afrika.

Katika mbuga zake za kitaifa na mapori ya akiba nchini Tanzania, unaweza kuona simba jike wakiwinda alfajiri, madume wakinguruma na wengine wakiwinda au kupumzika katika vivuli vya miti.

Unaweza kujionea wanyama hao katika hifadhi mbalimbali ikiwemo Serengeti, Ngorongoro, Tarangire na Ruaha.

Hata hivyo, takwimu hizo zinatofautiana na zile zilizotolewa na IUCN pamoja na Taasisi ya Utafiti wa Wanyamapori Tanzania (TAWIRI) ambao waliripoti idadi ya simba hao kuwa 17,000.

Nchi nyingine yenye idadi kubwa ya simba ni Afrika Kusini (Simba 3,284), Botswana (Simba 3,063), Kenya (Simba 2,515) na Zambia (Simba 2,500)

Pamoja na hayo, Tawiri ilibainisha kuwa Tanzania imeongoza barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama wengine ikiwemo Nyati na Chui.


Fahamu faida za kutumia mifumo rasmi ya fedha

Dar es salaam: Matumizi ya mifumo rasmi ya fedha ni nguzo muhimu katika kuimarisha ustawi wa kifedha wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya uchumi ya Taifa kwa ujumla.

Kupitia mifumo hiyo, ikiwemo benki, taasisi za fedha zilizosajiliwa na huduma za bima wananchi hupata usalama wa fedha zao, uwazi wa miamala na ufuatiliaji sahihi wa mapato na matumizi. 

Kwa mujibu wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT) mifumo rasmi hupunguza hatari ya wizi, upotevu wa fedha na ulaghai, huku ikirahisisha malipo ya huduma mbalimbali kama ada, kodi na mishahara kwa njia salama na za haraka.

Aidha, akiba inayowekwa kwenye mifumo rasmi inalindwa kisheria, hupata riba, na hujenga historia ya kifedha (credit history) ambayo humwezesha mhusika kupata mikopo kwa ajili ya uwekezaji, biashara au mahitaji ya kijamii.

Kwa ujumla, kutumia mifumo rasmi ya fedha ni msingi muhimu wa ukuaji endelevu wa uchumi, unaochochea uwajibikaji, ufanisi na maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks