Mambo matatu ya kuzingatia unapotafuta kazi

  • Ni pamoja na kuandaa wasifu binafsi na barua ya maombi kwa ufanisi. 

Dar es Salaam. Ni ndoto ya kila mhitimu wa chuo kupata kazi ya kufanya anapomaliza masomo yake. Kazi inaweza kuwa ya kuajiriwa au kujiajiri katika shughuli mbalimbali za kibiashara.

Ndoto hizo hutimia kwa nyakati tofauti. Kwa wengine hupata kazi mapema na wengine husota mtaani wakitembeza bahasha na kutuma maombi kila nafasi zinapotangwa mtandaoni. 

Kama wewe ni mmoja wa watu hao, yapo mambo muhimu unayotakiwa kuzingatia wakati unasaka ajira ya ndoto yako ikiwemo kuandaa wasifu na barua ya maombi ya kazi inayojitosheleza. 

Mwanzilishi wa Jukwaa la Niajiri, Lilian Madeje anasema kuwa ni muhimu mtu anayetafuta kazi kuandika vizuri wasifu wake, ambao unaelezea taarifa zake kwa usahihi.

“Kwenye ‘CV’ (wasifu) kwa ujumla, lazima mtu ahakikishe amefanya uhuishaji (updating). Aweze kuainisha kwa uwazi elimu yake, namba za simu ziko sawa, na kuepuka makosa ya kisarufi ili anayepokea kwa upande wa pili asitumie muda mrefu kumuelewa muombaji anafanya nini,” anasema Madeje.

Wasifu binafsi ni muhimu uwe fupi, wenye mpangilio mzuri, na usio na makosa ya kisarufi. Picha/ Eastern Suburbs Mums.

Madeje anasema hakikisha barua ya kuomba kazi (Application/cover letter) au barua pepe iwe inajielezea vizuri, na ionyeshe ujuzi ulionao na jambo gani anaweza kufanya kwa nafasi husika.

“Kwenye ‘cover letter’ kuna wengine wanatuma bila ya ‘heading’ (kichwa), wengine unakuta hata ile ‘CV’ (wasifu) mtu hajaifanyia ‘labeling’ vizuri,” anasema Madeje. “Mtu inabidi awe na email (barua pepe) ya kujitambulisha vizuri, ni nani ambaye unamtafuta na kama hauna mtu angalau ujielezee kidogo, mimi ni fulani, nimeona tangazo kwenye gazeti au mtandaoni.”

Aidha, Madeje amebainisha kuwa ni vyema muombaji akajiwekea malengo ya kuomba kazi ili kujiongezea wigo wa kupata kazi. 

“Tunaelewa fika kwamba kazi hazitoshi kwa watu wanaotoka vyuoni, lakini pia mtu inabidi ufanye ‘research’ (utafiti) yako. Umetoka chuo, unaenda kufanya ‘application’ (maombi) wapi? Unajipa ‘target’ (malengo) zako, labda kwa kipindi kila wiki unataka kufanya ‘application’ kiasi X ili uweze kuongeza wigo wako,” anasema Madeje.

Niajiri ni jukwaa la kiteknolojia la maendeleo ya nguvukazi linaloimarisha ujuzi wa vipaji vya ngazi ya mwanzoni na kuwapa mwonekano kwa waajiri, huku pia likiwa na zana inayowawezesha waajiri kufikia vipaji bora sokoni.

Afisa Mwajiri kutoka Shirika la Islamic Help, Zubery Titee anasema kuwa CV na barua ya maombi ya kazi zinatakiwa kuonyesha ufanisi wa maombi na kuwa na muundo mzuri wa kitaalamu. 

Titee anasema wasifu huu unapaswa kujumuisha ujuzi, elimu, na uzoefu unaohusiana na nafasi ya kazi anayotafuta, na usitumie maneno mengi yasiyohitajika.

Kulingana na tovuti ya The Balance Careers , wasifu (CV) ni nyaraka ndefu inayojumuisha historia ya kitaalamu ya mtu, ikiwa ni pamoja na elimu, uzoefu wa kazi, utafiti, machapisho na mafanikio mengine. 

Wasifu pia hutumika kwa madhumuni ya kitaalamu, kama vile maombi ya kazi au nafasi za utafiti katika vyuo vikuu.

Kwa upande mwingine, ‘resume’ ni taarifa fupi inayojumuisha taarifa muhimu kuhusu ujuzi, uzoefu wa kazi, na elimu. Lengo la ‘resume’ ni kutoa muhtasari wa haraka wa sifa za muombaji.

Ikiwa unabadilisha taaluma yako, unaanza katika nchi mpya, au umekuwa nje ya ajira kwa muda, wasifu wako unaweza kukusaidia kupata kazi yako ijayo kwa kuufanya kwa njia sahihi. Picha / Fiverr.

“Ni muhimu kuandaa ‘CV’ (wasifu) yenye kuvutia ambayo itaonyesha ‘profile’ yake, elimu, kozi mbalimbali, semina alizopata kushiriki pamoja na uzoefu katika kufanya kazi au kujitolea katika kazi,” anasema Titee.

Pia, uzoefu wa kazi unapaswa kuonyeshwa kwa uwazi kwenye wasifu ili kuwawezesha waajiri kufanya maamuzi sahihi.

“Waajiri wanapenda sana kuona uzoefu wa muombaji katika nafasi husika, na aghalabu hii ndio inatoa nafasi kubwa ya kuitwa kwenye usaili,” anaeleza Titee.

Uwezo wa kujieleza nao muhimu

Muombaji kazi awe na uwezo wa kujieleza vizuri kuhusu kile alichoandika kwenye wasifu wake binafsi. Maswali atakayoulizwa kwenye usaili yanaweza kutoka kwenye wasifu wake aliowasilisha. 

Titee anasema kuwa ni muhimu kwa muombaji kuwa na uelewa wa kina kuhusu jina na malengo ya taasisi anayotaka kujiunga nayo. Waajiri wanapenda kuona muombaji mwenye ufanisi na uelewa wa kweli kuhusu kampuni au shirika analotaka kujiunga nalo.

“Mfano, unaomba kazi katika Shirika la Islamic Help, lakini kwenye barua yako ya maombi unaandika ‘Islamic Help Foundation’. Hii inaweza kuwa dalili ya kutokuwa makini,” anasema Titee.

Ni vyema muombaji kuwa na uwezo wa kujieleza vizuri kuhusu kile alichoandika kwenye wasifu wake binafsi. Picha/ Fair screen.

Muombaji awe na uwezo wa kutetea kile kilichoandikwa kwenye wasifu wake, kwani maswali mengi yanaweza kutokea huko au uelewa wake wa jumla unaweza kusaidia na baadaye kuzingatiwa katika kupata ajira.

Kujiandaa vizuri ni hatua ya kwanza kuelekea kwenye mafanikio yako ya kazi. Usikose kufuatilia toleo la pili la chapisho hili litakalokufunza namna ya kuandaa wasifu.

 Lishe inavyoweza kukabiliana na matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa

  • Hii ni pamoja na ulaji wa matunda na mboga mboga.
  • Nchini Tanzania takribani watoto 7,500 huzaliwa na matatizo ya mgongo wazi pamoja na vichwa vikubwa.

Dar es Salaam. Lishe bora imetajwa kuwa miongoni mwa kinga za magonjwa ya mgongo wazi na vichwa vikubwa yanayowapata watoto wachanga wenye umri kati ya 0 hadi miezi miwili.

Magonjwa hayo ambayo kitaalamu huitwa ‘Spinal bifida and Hydrocephalus’ mara nyingi hugundulika pale tu mtoto anapozaliwa huku wengine wakichukua muda zaidi.

Kituo cha Kudhibiti na Kukinga Magonjwa nchini Marekani  (CDC) kimesema  watoto wengi wanaozaliwa na mgongo wazi mara nyingi hupata ulemavu wa kichwa kikubwa kunakosababishwa na ubongo kujaa maji.

Picha hii inaonesha mgongo wazi, ugonjwa ambao mtoto anazaliwa huku uti wa mgongo ukiwa wazi (kidonda/uvimbe mgongoni) kutokana na pingili za mgongo kutokuziba vizuri.picha/StoryMd

“Hii inatokea kutokana na kifaa cha ubongo kutokufanya kazi ipasavyo katika kuchuja na kutoa majimaji kupitia njia za asili ndani ya ubongo na uti wa mgongo. Matokeo yake ni kwamba kuna maji mengi yanakusanyika ndani na kuzunguka ubongo,” imesema CDC.

Majimaji hayo ya ziada yanaweza kusababisha sehemu za ubongo zinazojulikana kama ventrikali kuwa kubwa kupita kiasi, na hivyo kusababisha kichwa kuvimba. 

CDC imesema Miongoni mwa dalili za tatizo la kichwa kikubwa ni pamoja na kichwa cha mtoto kuwa kikubwa kuliko kawaida, macho kuelekea chini, utosi kuzidi kwa mtoto mchanga na mtoto kutapika sana na kuhisi kizunguzungu.

Kwa upande wa mgongo wazi kituo hicho kimezitaja dalili zake kuwa ni pamoja na mtoto kuwa na uvimbe ama kidondo katika uti wa mgongo, mtoto kuwa na baka, chale au nywele zisizo za kawaida katika eneo la uti wa mgongo.

Nchini Tanzania takribani watoto 7,500 huzaliwa na matatizo ya mgongo wazi pamoja na vichwa vikubwa huku watoto 1000 tu ndio wanaopatiwa matibabu kwa mwaka.

Takwimu hizo zimetolewa na Dk Hamisi Shabani kutoka katika Hospitali ya Taifa Muhimbili iliyopo jijini Dar es Salaam wakati akifanyiwa mahojiano kwenye kipindi cha televisheni kupitia Shirika la Utangazaji Tanzania (TBC) ambapo pia amewatoa hofu wazazi kwa kuwa tatizo hilo linatibika.

“Hili tatizo hasa la kichwa kikubwa linatibika na mtoto anarudi kuwa mtu mzima kabisa kama wanajamii wengine hili la mgongo wazi linategemea ule ulemavu umefikia kiwango gani lakini pia unatibika…

…Nisiwatishe Watanzania kwa sababu haya matibabu yanapatikana katika hospitali zetu,” ameeleza Dk Shabani ambaye pia ni daktari bingwa wa upasuaji wa magonjwa ya ubongo,uti wa mgongo pamoja na mgongo wazi.

Hata hivyo,daktari Hamisi amekiri kuwepo kwa kiwango kidogo cha elimu sahihi ya visababishi na tiba ya magonjwa hayo jambo linalopelekea kuwa na idadi kubwa ya watoto ambao hawajapatiwa matibabu.

Lishe bora suluhisho la kudumu

Wakati madaktari wakiendelea kuhamasisha tiba ya magonjwa hayo, wataalamu wa lishe wanasema lishe bora kwa mama mjamzito na wanawake wenye umri wa kuzaa ndiyo suluhisho la kudumu kwa matatizo ya mgongo wazi na vichwa vikubwa.

“Wanatakiwa waanze kutumia vile vidonge vya ‘Fefo’ mapema, vidonge hivi vina ‘combination’ (mchanganyiko) ya madini ya chuma na vitamini ya Foliki asidi ambayo inasaidia katika kupunguza matatizo ya watoto kuzaliwa na matatizo ya vichwa vikubwa na mgongo wazi, ”amesema Malimi Kitunda Mtaalamu wa lishe kutoka Taasisi ya Chakula na Lishe Tanzania (TFNC).

Mfano wa dawa ambazo wanawake wajawazito wanatakiwa kutumia kwa maelekezo ya wataalamu wa afya mara tu wanapokuwa wameanza kuhudhuria kliniki. Picha/Dk Mwanyika.

Malimi ameongeza kuwa pia ni vyema mtu kutumia vyakula ambayo vimeongezwa virutubishi vya madini ya foliki asidi kwa wingi kama vile mahindi na unga wa ngano ambao una ziada ya virutubisho.

“Kwa sasa hivi tunaongeza virutubishi vya foliki asidi kwenye mahindi na unga wa ngano kwa ajili ya kupambana na tatizo hilo la watoto kuzaliwa na tatizo la mgongo wazi pamoja na vichwa vikubwa,” amebainisha hilo Malimi.

Aidha, Malimi ameeleza kuwa kwa sasa virutubisho hivyo vinapatikana Tanzania na vimeanza kutumiwa na wazalishaji wakubwa wa unga wa mahindi na ngano.

Vyakula vyenye vitamini ya foliki asidi kwa wingi ni pamoja na  maharage, kabichi, mahindi, maini, mihogo, viazi, maziwa na mayai.

Hata hivyo, matunda kama papai,parachichi,ndizi,machungwa, tikiti maji, nanasi, kakara, tufaa, zabibu na matunda mengine pia yapaswa kuzingatiwa kabla na wakati wote wa ujauzito.

Tumbaku yazitikisa kahawa, korosho mauzo nje ya nchi Tanzania

  • Thamani ya mauzo nje ya nchi yaongezeka takriban mara mbili ndani ya mwaka mmoja.

Dar es Salaam. Tumbaku ni moja ya bidhaa tatu asilia zinazoongoza kwa kuuzwa kwa wingi nje ya Tanzania na zilizoingiza fedha nyingi za kigeni licha ya kupigwa vita na wadau wa afya kuwa inahatarisha maisha ya watumiaji. 

Kwa mujibu wa Ripoti ya Hali ya Uchumi Tanzania mwaka 2023 iliyotolewa na Wizara ya Fedha hivi karibuni, katika bidhaa za asilia zinazouzwa nje ya nchi tumbaku inachuana kwa mbali na kahawa na korosho. 

Korosho, kahawa, chai na mkonge ni miongoni mwa mazao makubwa ya asilia ambayo huchangia kwa kiwango kikubwa fedha za kigeni nchini ila ukuaji wa uzalishaji wa tumbaku umezidi kuyapiga kikumbo mazao hayo. 

“Mwaka 2023, thamani ya mauzo ya tumbaku nje ilikuwa Dola za Marekani milioni 340.4 (Sh828.2 bilioni) ikilinganishwa na Dola za Marekani milioni 178.5 (Sh411.5 bilioni) mwaka 2022, sawa na ongezeko la asilimia 90.7,” inasema ripoti hiyo iliyotolewa na Wizara ya Fedha.

Ripoti hiyo inaeleza kuwa mafanikio hayo yalitokana na kuongezeka kwa mauzo ya tumbaku kwa zaidi ya mara moja na nusu hadi kufikia tani 82,000 mwaka 2023 kutoka tani 49,300 mwaka 2022. 

Uuzaji wa zao hilo nje ya nchi ulienda sanjari na kiwango cha uzalishaji wa tumbaku ulioongezeka takriban mara mbili ndani ya mwaka mmoja kutoka tani 70,699 mwaka 2022 hadi tani 122,859 mwaka jana. 

Uzalishaji wa tumbaku umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka Tanzania jambo lililochochea ongezeko la kiwango cha zao hilo kuuzwa nje ya nchi. Picha: Akili Mnemba. Picha hii imetengenezwa na akili mnemba kwa ajili ya kuongeza muktadha kwenye makala hii tu na si kuonyesha uhalisia.

Bei yaibeba tumbaku

Wastani wa bei ya kuuza tumbaku uliongezeka kwa asilimia 14.5 katika soko la dunia na kufikia Dola za Marekani 4,150.8 (Sh11.1 milioni) kwa tani mwaka 2023 kutoka Dola za Marekani 3,624.1(Sh9.7 milioni) kwa tani mwaka 2022.

Ingawa kiasi cha wingi wa korosho kinachouzwa nje ya Tanzania ni zaidi ya mara mbili ya kiasi cha tumbaku na kahawa, thamani ya tumbaku kwenye soko la kimataifa inazidi kwa zaidi ya mara 1.5 ya thamani ya korosho na kahawa. 

Kwa hesabu hizo, tumbaku inakuwa bidhaa asilia yenye thamani kubwa zaidi inayouzwa nje ya nchi. Bidhaa nyingine zisizoasilia zinazochangia zaidi fedha za kigeni ni dhahabu, utalii na bidhaa za viwandani. 

Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na hamasa kubwa ya kuongeza ufanisi katika uzalishaji wa tumbaku kwa kutumia mbinu za kisasa za kilimo na kuimarisha uchakataji wake ili kupunguza athari kwa mazingira.

Mfano, kampuni Mkwawa Tobacco Processing Limited (MTPL), imeendelea kufanya uwekezaji mkubwa katika usindikaji tumbaku, ikiongeza ajira na kuinua uchumi wa wananchi na wafanyabiashara. 

Uwekezaji huo katika uzalishaji na usindikaji unaofanywa na wakulima na viwanda vya zao hilo, unafanya tumbaku kuwa ni miongoni mwa bidhaa asilia zinazochangia kiwango kikubwa kwenye pato la taifa.  

Pamoja na uwekezaji huo kumekuwa na presha kubwa kutoka kwa wadau wa afya hasa wanaharakati wakiitaka Serikali kudhibiti vikali uzalishaji na utumiaji wa tumbaku unaochangia maradhi kwa binadamu ikiwemo matatizo ya mapafu.

Uteuzi Dk Ndugulile WHO kuipaisha Tanzania kimataifa

  • Ateuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya (WHO), Kanda ya Afrika na kuwa mtu wa kwanza kutoka Afrika Mashariki kushika wadhifa huo.
  • Mwanadiplomasia huyo huzungumza lugha zaidi ya moja.

Dar es Salaam. Tanzania imeendelea kung’aa katika anga za uongozi kimataifa mara baada ya Mbunge wa Jimbo la Kigamboni jijini Dar es Salaam Dk Faustine Ndugulile kuteuliwa kuwa Mkurugenzi wa Shirika la Afya Duniani (WHO) Kanda ya Afrika. 

Dk Ndungulile, ambaye ni daktari wa binadamu kitaaluma, sasa anaingia kwenye orodha ya wanadiplomasia mashuhuri Tanzania wanaoongoza taasisi za kimataifa katika ngazi ya dunia na kikanda. 

Kiongozi huyo anakuwa wa kwanza kutoka ukanda wa Afrika Mashariki kuchukua kijiti hicho kutoka kwa Dk Mtashidiso Moeti ambaye amehudumu katika nafasi hiyo kwa kipindi cha miaka 10 tangu mwaka 2014. 

Kwa mujibu wa WHO uteuzi Dk Ndugulile unatarajiwa kuridhiwa kwenye kikao cha 156 cha Bodi ya Utendaji wa WHO kitakachofanyika Februari, 2025 huko jijini Geneva, Uswizi ikiwa ndiyo mwanzo wa safari ya miaka mitano ya uongozi wa mtaalamu huyo wa afya. 

Dk Ndugulile (55) mwenye Shahada ya udaktari wa madawa pamoja na shahada ya uzamili kwenye mikrobiolojia na chanjo katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amewahi kushika nyazifa mbalimbali ndani ya Serikali ikiwemo ya unaibu waziri wa afya. 

Ushindi huo wa Dk Ndugulile aliyekuwa akichuana na wataalamu wengine kutoka Rwanda, Niger na Senegal ni moja ya hatua muhimu kwa Tanzania kuendelea kuimarisha taswira yake katika nyanja za kimataifa hususan katika taasisi kuu za kufanya maamuzi duniani. 

Nchi wanachama wa Afrika walimteua Dk Ndugulile jijini Brazzaville nchini Congo jambo ambalo amesema ni heshima kubwa kwake. 

“Nia yangu ni kufanya kazi pamoja nanyi na naimani kwamba kwa pamoja tutaweza kujenga Afrika yenye afya bora,” amesema Dk Ndugulile.

Dk Ndugulile, aliyewahi kuwa Waziri wa zamani wa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano alijunga na siasa tangu 2010 kupitia tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) huku akishikilia nyadhifa mbalimbali za uongozi kwenye sera za afya kutokana na uzoefu wake wa kazi.

Mtaalamu huyo wa afya ameongoza miradi mbalimbali katika huduma za afya nchini Tanzania na kuandika machapisho ya tafiti zinazohusu afya ya umma ambazo zimechangia katika maendeleo ya sera za afya inayolenga kuboresha afya ya wananchi.

“Dk Ndugulile amepata imani na uaminifu wa wanachama wa nchi wa kanda hii kwa kuchaguliwa kuwa Mkurugenzi wa WHO Kanda ya Afrika, hii ni heshima kubwa na jukumu kubwa sana…mimi na familia nzima ya WHO barani Afrika na duniani kote tutakusaidia katika kila hatua,” amebainisha Dk Ghebreyesus.

Hata hivyo, kuteuliwa kwake kama Mkurugenzi wa Shirika la Afya (WHO), Kanda ya Afrika ni hatua muhimu katika kufanikisha malengo ya afya kwa nchi za Afrika hii inathibitisha kutokana na  uzoefu na utaalamu wake kwenye uwanja wa afya.

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassan aliyekuwa akimpigia kampeni Dk Ndugulile alieleza kwenye mtandao wa X (zamani Twitter) kuwa kiongozi ameiheshimisha nchi na kwamba Afrika itanufaika na utaalamu wake. 

“Nina imani kuwa ujuzi na uzoefu wako katika sekta ya afya utawezesha Afrika kuwa na sauti muhimu katika uwanja wa kimataifa katika kukabiliana na changamoto za kiafya kwa mamilioni ya watu katika bara letu,” amesema Rais Samia.

Unavyoweza kuandaa mirathi mtandaoni kupitia akaunti ya kidijitali

  • Ni kwa kutumia nyenzo maalum ya usimamiaji wa mirathi ya kimtandao.
  • Hupunguza upotevu wa taarifa mtandaoni baada ya mtumiaji kufariki.

Dar es Salaam. Matumizi ya teknolojia na mtandao yamezidi kushika kasi siku za hivi karibuni yakiwawezesha watu kuwasiliana huku wengine wakiitumia kuhifadhi mambo muhimu ikiwemo nyaraka za kibenki, hati za nyumba na kumbukumbu za maisha yao.

Lakini umewahi kufikiria nini kitatokea kwa taarifa ulizohifadhi mtandaoni baada ya kifo chako? 

Watu wengi wamekua wakiacha mirathi ya mali zinazohamishika na wanazomiliki kwa wanafamilia wao ili wafaidike lakini husahau kuacha urithi wa taarifa muhimu walizohifadhi mtandaoni kwenye mikono salama.

Leo tunaangazia umuhimu wa kuandaa mipango ya kuhifadhi taarifa zako za mtandaoni kwa watu unaowaamini kabla ya kufariki.

Jinsi ya kuandaa mirathi ya akaunti yako

Intaneti imeongeza wigo wa ufikiaji na matumizi ya huduma mbalimbali kidijitali kama miamala ya kifedha, hifadhi ya nyaraka muhimu, hati, picha na video ambazo zinaweza kuwa na faida kwa watu wa karibu utakaowaacha, Google inaweza kuwaruhusu kupata baadhi ya vitu hivyo endapo utaamua mapema.

Kupitia huduma ya akaunti ya google isiyotumika, unaweza  kuamua kitakachotendeka mara tu akaunti yako inapoacha kutumika kwa muda uliouweka, kuliko kuzuia kabisa ikae kwenye seva bila kufikika na watu muhimu wanaosalia.

Kwanza andaa orodha ya akaunti zote unazomiliki zikiwa na majina na nywila zake, kisha chagua watu au mtu unayemwamini atakayekuwa na jukumu la kuzisimamia kisha ufuate vigezo vya sera ya urithi ya mtoa huduma.

Kabla akaunti yako kufungwa kwa kutotumika ni muhimu kuweka mpangilio (setting) ili kupata taarifa kupitia barua pepe na ujumbe mfupi wa simu.

Warithi wa taarifa zako ulizohifadhi mtandaoni lazima wathibitishe kupitia ujumbe mfupi (SMS) kabla hawajapewa ruhusa ya ufikiaji wa taarifa hizo, pia unaweza kuwatumia jumbe binafsi za alama za kidijitali za vidole vyako ili kurahisisha zoezi hilo.

Baada ya kuthibitisha mrithi atapata sms itakayomjulisha kupewa taarifa hizo na kiungo maalum (link) itakayomuwezesha kupakua taarifa zote ulizohifadhi.

Usipoacha urithi wa kidijitali, watu wako wa karibu watahitaji kuwasiliana na Google juu ya akaunti yako ili kuwafahamisha kuwa umefariki, sambamba na kuwapa uthibitisho wa kifo ili waruhusiwe kupata vitu maalumu utakavyokua umeruhusu wao kuvifikia kwa sababu hawataweza kufungua vitu vyote vya kwenye akaunti yako.

Faida za kuacha mrithi wa taarifa za mtandaoni

Kupanga urithi wa akaunti za kidijitali husaidia ulinzi wa taarifa kwa kuhakikisha kuwa picha au video za familia, mawasiliano muhimu na nyaraka za kifedha zinabaki salama za kuweza kupatikana kwa warithi wako.

Pia husaidia kuwapunguzia watu wako wa karibu mzigo wa kutafuta na kupata taarifa zako baada ya kifo chako sambamba na kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinatumika kulingana na matakwa yako.

Usikose sehemu ya pili ya makala hii ambapo tutaangazia jinsi unavyoweza kupata taarifa zilizohifadhiwa mtandaoni na ndugu, jamaa au rafiki aliyeaga dunia.

Enable Notifications OK No thanks