Jinsi ya kufungua programu zilizofichwa kwenye iPhone
- Zinaweza kufichwa, kufunguliwa na kurejeshwa kwa uthibitisho wa kibayometriki au nenosiri.
Dar es Salaam. Watumiaji wa simu za iPhone kutoka kampuni ya Apple yenye makao yake makuu California, Marekani, wameanza kufurahia uwezo wa kipengele kipya cha kuficha na kufunga programu kwenye simu zao kupitia toleo jipya la iOS 18 lililotolewa Septemba 2024.
Kipengele hicho husaidia kulinda programu na taarifa nyeti kutokuonekana na wengine wanapotumia simu kwa kuzificha programu kwenye folda maalumu ambalo uhitaji nenosiri au uthibitisho wa kibayometriki.
Ili kufunga au kuficha programu kwenye iPhone, bonyeza na ushikilie ikoni ya programu, kisha chagua ‘Require Face ID.’ Programu hiyo itatoweka kutoka kwenye skrini iliyozoeleka na haitapatikana hata kwenye matokeo ya utafutaji wa ‘Spotlight’.
Programu zilizofichwa huondolewa kwenye skrini kuu na kuhifadhiwa kwenye folda ya siri inayoitwa inayopatikana kwenye ‘App Library’. Picha |CNET
Lakini, wakati mwingine programu zinaweza kufichwa kwa makusudi au kwa bahati mbaya, na zikahitajika kutumiwa tena. Kujua hatua za kuziona kupitia mipangilio ni muhimu ili kusaidia kuzifungua bila kuhangaika.
Kuna njia mbili za kupata programu zilizofichwa kwenye iPhone, ya kwanza ni kufungua iPhone yako na kushuka hadi mwisho wa skrini ili kufikia ukurasa wa ‘App Library.’
Chini kabisa bonyeza ‘hidden folder’, kisha utaombwa kuthibitisha kwa kutumia ‘Face ID’ au ‘Touch ID’, ikiwa uthibitisho wa kibiometriki utashindikana, ingiza nenosiri.
Ukishafanya hivyo, utaweza kuona programu zote zilizofichwa. Ili kuzifungua, utahitaji kuthibitisha tena kwa njia hiyo hiyo yaani kwa kutumia Face ID, Touch ID, au nenosiri ili programu hizo zisifunguliwe na mtu mwingine yeyote bila kibali cha mwenye simu.
Njia ya pili ya kuna programu zilizofichwa ni kupitia mipangilio ‘settings’, hapa nenda kwenye ‘Settings’ kisha ‘Apps’ alafu uingie kwenye ‘Hidden Apps’, kuona programu zote zilizofichwa.
‘Screenshot’ ikionyesha unavyoweza kufunga programu za msingi kama ‘Notes’ kwa kuchagua ‘Require Face ID’ kwa usalama wa nyaraka zako. Picha |CNET
Wakati mwingine mtumiaji anaweza kuficha programu bila kukusudia na kuhitaji kuirejesha kwenye utaratibu wa upatikanaji wa kawaida kwenye ‘home screen’, ili kuirejesha fuata njia ifuatayo.
Fungua iPhone yako na nenda kwenye ‘App library’, kisha gusa ili kufungua folda ya programu zilizofichwa kwa kutumia Face ID au Touch ID.
Baada ya hapo, gusa na ushikilie programu mahususi unayotaka kuirejesha, alafu chagua ‘Don’t require Face ID,’ na uthibitishe kwa mara ya mwisho kwa kutumia uso, alama ya kidole au nenosiri.
Hatua hizo zitakapo fuatwa, programu lengwa itaondolewa kwenye folda la siri na kurudi tena kwenye skrini ya mwanzo, ambapo mtumiaji anaweza kufanya hivyo kwa kuitafuta kwenye ‘App library’ au kupitia ‘Spotlight’.
Unavyoweza kuandaa mirathi mtandaoni kupitia akaunti ya kidijitali
- Ni kwa kutumia nyenzo maalum ya usimamiaji wa mirathi ya kimtandao.
- Hupunguza upotevu wa taarifa mtandaoni baada ya mtumiaji kufariki.
Dar es Salaam. Matumizi ya teknolojia na mtandao yamezidi kushika kasi siku za hivi karibuni yakiwawezesha watu kuwasiliana huku wengine wakiitumia kuhifadhi mambo muhimu ikiwemo nyaraka za kibenki, hati za nyumba na kumbukumbu za maisha yao.
Lakini umewahi kufikiria nini kitatokea kwa taarifa ulizohifadhi mtandaoni baada ya kifo chako?
Watu wengi wamekua wakiacha mirathi ya mali zinazohamishika na wanazomiliki kwa wanafamilia wao ili wafaidike lakini husahau kuacha urithi wa taarifa muhimu walizohifadhi mtandaoni kwenye mikono salama.
Leo tunaangazia umuhimu wa kuandaa mipango ya kuhifadhi taarifa zako za mtandaoni kwa watu unaowaamini kabla ya kufariki.
Jinsi ya kuandaa mirathi ya akaunti yako
Intaneti imeongeza wigo wa ufikiaji na matumizi ya huduma mbalimbali kidijitali kama miamala ya kifedha, hifadhi ya nyaraka muhimu, hati, picha na video ambazo zinaweza kuwa na faida kwa watu wa karibu utakaowaacha, Google inaweza kuwaruhusu kupata baadhi ya vitu hivyo endapo utaamua mapema.
Kupitia huduma ya akaunti ya google isiyotumika, unaweza kuamua kitakachotendeka mara tu akaunti yako inapoacha kutumika kwa muda uliouweka, kuliko kuzuia kabisa ikae kwenye seva bila kufikika na watu muhimu wanaosalia.
Kwanza andaa orodha ya akaunti zote unazomiliki zikiwa na majina na nywila zake, kisha chagua watu au mtu unayemwamini atakayekuwa na jukumu la kuzisimamia kisha ufuate vigezo vya sera ya urithi ya mtoa huduma.
Kabla akaunti yako kufungwa kwa kutotumika ni muhimu kuweka mpangilio (setting) ili kupata taarifa kupitia barua pepe na ujumbe mfupi wa simu.
Warithi wa taarifa zako ulizohifadhi mtandaoni lazima wathibitishe kupitia ujumbe mfupi (SMS) kabla hawajapewa ruhusa ya ufikiaji wa taarifa hizo, pia unaweza kuwatumia jumbe binafsi za alama za kidijitali za vidole vyako ili kurahisisha zoezi hilo.
Baada ya kuthibitisha mrithi atapata sms itakayomjulisha kupewa taarifa hizo na kiungo maalum (link) itakayomuwezesha kupakua taarifa zote ulizohifadhi.
Usipoacha urithi wa kidijitali, watu wako wa karibu watahitaji kuwasiliana na Google juu ya akaunti yako ili kuwafahamisha kuwa umefariki, sambamba na kuwapa uthibitisho wa kifo ili waruhusiwe kupata vitu maalumu utakavyokua umeruhusu wao kuvifikia kwa sababu hawataweza kufungua vitu vyote vya kwenye akaunti yako.
Faida za kuacha mrithi wa taarifa za mtandaoni
Kupanga urithi wa akaunti za kidijitali husaidia ulinzi wa taarifa kwa kuhakikisha kuwa picha au video za familia, mawasiliano muhimu na nyaraka za kifedha zinabaki salama za kuweza kupatikana kwa warithi wako.
Pia husaidia kuwapunguzia watu wako wa karibu mzigo wa kutafuta na kupata taarifa zako baada ya kifo chako sambamba na kuhakikisha kuwa taarifa hizo zinatumika kulingana na matakwa yako.
Usikose sehemu ya pili ya makala hii ambapo tutaangazia jinsi unavyoweza kupata taarifa zilizohifadhiwa mtandaoni na ndugu, jamaa au rafiki aliyeaga dunia.
Idadi ya redio yazidi kupaa Tanzania
- Idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 17 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.
Dar es Salaam. Wakati dunia ikiadhimisha Siku ya Redio leo Februari 13, 2022, redio ni chombo muhimu ambacho Watanzania wana kitumia kupata habari zinazowawezesha kufanya maamuzi katika maisha yao ya kila siku.
Licha ya kuongezeka kwa changamoto za kifedha zinazoendelea kuvikabili vyombo mbalimbali vya habari duniani, idadi ya vituo vya redio Tanzania imezidi kuongezeka kwa kasi baada ya vituo 17 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.
Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) inaeleza katika ripoti mpya ya mawasilino ya robo ya mwisho ya mwaka 2021 kuwa hadi Desemba mwaka jana kulikuwa na vituo 210 vya redio nchini kutoka vituo 193 mwaka 2020.
Uchambuzi wa mwenendo wa takwimu za vituo vya redio uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) unaonyesha kuwa vituo vingi vya redio vilizaliwa mwaka 2016 baada ya vituo 42 kuanzishwa ndani ya mwaka mmoja.
Hata hivyo, mwaka 2018 ndiyo mwaka ambao vituo vichache zaidi vilianzishwa ndani ya mwaka mmoja kutokana na kuongezeka kwa vituo viwili tu vya redio kutoka 156 mwaka 2017 hadi 158 mwaka 2018.