Hali ya kipato cha Mtanzania katika takwimu

Dar es Salaam. Ripoti ya Benki ya Dunia kuhusu Hali ya Uchumi wa Tanzania iliyotolewa Septemba 2026 inasema nguvu kazi iliyoajiriwa nchini Tanzania ina watu milioni 27.3 kati ya watu milioni 37 walio katika umri wa kufanya kazi.
Kati ya nguvu kazi hiyo waliojiajiri ni asilimia 75, asilimia 17 ni wafanyakazi wanaosaidia katika shughuli za familia huku wafanyakazi walioajiriwa katika ajira rasmi wakiwa ni asilimia 8 pekee ya nguvu kazi.Â
Hata hivyo, ripoti hiyo inasema kuwa Tanzania haikabiliwi na uhaba wa ajira, bali changamoto ya ubora wa ajira.
Ripoti inasema kuwa licha ya asilimia 68.7 ya watu walio katika umri wa kufanya kazi kuwa na ajira au shughuli za kiuchumi, sehemu kubwa ya nguvu kazi iko katika shughuli zenye kipato kidogo.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, wastani wa kipato cha Watanzania wengi wanaojishughulisha ni Sh1,005 tu saa, ikijumuisha faida na mapato yasiyo ya fedha.
Kwa kuzingatia wiki ya kazi ya kisheria ya Tanzania ya saa 45 kwa wiki, kipato hicho ni sawa na Sh45,225 kwa wiki na Sh195,975 tu kwa mwezi mzima.
Wakati huo huo, Benki ya Dunia imetumia Sh3,830 kwa saa kama kiwango cha malipo kinachoweza kutumika kutambua ajira yenye kipato cha heshima.
Hii ina maana kuwa kwa kuzingatia wiki ya kazi ya kisheria ya Tanzania ya saa 45 kwa wiki Mtanzania mwenye kazi yenye kipato bora anatakiwa kuwa anaingiza angalau Sh750,000 kwa mwezi.
Hii ni kwa kutumia vya kima cha chini cha mshahara vilivyokuwa vinatumika nchini Tanzania mwaka 2024.Â