Shilingi ya Tanzania yaanza kuimarika dhidi ya Dola ya Marekani 

February 24, 2026 4:35 pm · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Imeimarika kwa wastani wa Sh30 na Sh25 ndani ya wiki moja kupitia benki kubwa za biashara nchini za CRDB na NMB mtawalia.
  • Wachambuzi wa uchumi waeleza hali hiyo huleta kicheko na maumivu.

Arusha. Wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa kutoka nje ya Tanzania huenda wakaianza wiki mpya kwa matumaini kufuatia kuimarika kwa Shilingi ya Tanzania dhidi ya Dola ya Marekani.

Uchambuzi wa takwimu za viwango vya kubadilisha fedha za kigeni vilivyotolewa na benki kubwa za biashara nchini za CRDB na NMB unaonesha kuwa Shilingi ya Tanzania imeimarika kwa wastani wa Sh30 na Sh25 mtawalia dhidi ya Dola ya Marekani ndani ya wiki moja. 

Hali hiyo inaenda kutoa ahueni kidogo kwa baadhi ya wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje ya nchi kwa kutumia Dola ya Marekani. 

Kwa mujibu wa viwango hivyo vilivyotangaza na CRDB kwa ajili ya kutumika leo Februari 24, 2026 Dola ya Marekani inanunuliwa kwa Sh2,540 na kuuzwa kwa Sh2,620 kiwango kilichopungua kidogo kulinganishwa na kile kilichorekodiwa wiki iliyopita.

Februari 16 mwaka huu Dola ya Marekani ilinunuliwa kwa Sh2,570 na kuuzwa kwa Sh2,650 kupitia benki ya CRDB, kiwango ambacho kilikuwa kimeongezeka kutoka majuma yaliyopita. 

Mwenendo huo chanya umeakisiwa pia na viwango vilivyotolewa vya NMB vinavyoonesha kuwa Shilingi imerekodi ongezeko la thamani la wastani wa Sh25 ndani ya wiki moja. 

Dola ya Marekani leo inanunuliwa kwa Sh2,545 na kuuzwa kwa Sh2,625 katika benki ya NMB iklinganishwa na Sh2,570 iliyotumika na Sh2,650 vilivyotumika  Februari 16 mwaka huu.

Kuimarika kwa Shilingi hutoa ahueni kwa wafanyabiashara wanaoagiza bidhaa nje ya nchi kwa kutumia Dola ya Marekani.Picha/Thomas Blog.

Hata hivyo, viwango vya kubadili fedha za kigeni vinavyotumika na BoT kwa ajili ya kuuzia benki za biashara vimeendelea kuwa juu ya viwango vinavyotumika na taasisi hizo za kifedha. 

Viwango vya Benki Kuu ya Tanzania (BOT) leo Februari 24, 2026  vinaonesha kuwa Dola ya Marekani inanunuliwa kwa Sh2,555 na kuuzwa kwa Sh2,581 kutoka bei ya Sh2,547 iliyotumika kununua na Sh2,572 kuuza fedha hiyo Februari 16 mwaka huu.  

Hivi karibuni BoT iliwaeleza wanahabari kuwa Shilingi ya Tanzania inaendelea kuimarika ikirekodi ongezeko la asilimia 0.8 mwishoni wa robo ya nne ya 2025.

Ndani ya miezi miwili BoT imekuwa ikichukua hatua mbalimbali ili kuongeza Dola ya Marekani sokoni kutokana na shinikizo kubwa kwa Shilingi kuanzia mwanzoni mwa mwaka huu. 

Februari 18, 2026 BoT iliuza Dola za Marekani milioni 15 kupitia mnada maalum katika soko la fedha za kigeni, kwa wastani wa Sh2,587.85 kwa dola moja, ikilenga kuongeza upatikanaji wa fedha za kigeni na kuimarisha uthabiti wa shilingi.

Wataalamu wa uchumi wanaeleza kuwa kuimarika kwa Shilingi kutakuwa na ahueni na maumivu kwa Watanzania kutokana na mahitaji. 

Shilingi ikiimarika bidhaa za Tanzania huwa ghali zaidi kwa wanunuzi wanaolipa kwa fedha hiyo ya kigeni. 

Kicheko, maumivu

Profesa Alfred Kyondo, mchambuzi wa masuala ya uchumi na  Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam ameiambia Nukta Habari kuwa kwa waagizaji bidhaa kutoka nje ya nchi kuimarika kwa Shilingi kutawapa ahueni kwa kuwa watatumia Dola kidogo tofauti na awali. 

Pale shilingi inapopanda thamani dhidi ya Dola ya Marekani, amesema bidhaa za Tanzania huwa ghali zaidi kwa wanunuzi wanaolipa kwa fedha hiyo ya kigeni. 

Kwa mujibu wa Prof Kyondo, hali hiyo inaweza kuwafanya baadhi ya wanunuzi kuelekeza mahitaji yao katika nchi ambazo sarafu zake ni dhaifu zaidi, ambako wanaweza kupata bidhaa nyingi kwa gharama ndogo ya dola.

Ili kuona manufaa ya kuimarika kwa Shilingi hiyo nchini, amesema Serikali inatakiwa kudhibiti (stabilize) Shilingi ya Tanzania ili iendelee iwe na nguvu zaidi duniani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks