Fahamu faida za ulaji wa brokoli
- Ni pamoja na kuzuia ugonjwa wa moyo na kuimarisha afya ya mifupa kulingana na uwepo wa nyuzi nyuzi na vitamini.
- Kusaidia mmeng’enyo wa chakula na matatizo ya kiungulia.
Dar es Salaam. Kuna aina za nyingi za mbogamboga na kila moja ina faida zake katika mwili wa binadamu ikiwemo kuimarisha kinga mwilini.
Pamoja na wingi wa mboga hizo, kila moja ina faida zake mahususi ambazo unaweza usizipate katika aina nyingine za mboga au ukazipata kwa uchache.
Katikati ya aina hizo za mboga ipo brokoli, mboga maarufu inayosifika kwa faida nyingi za kiafya ikiwemo wingi wa kirutubisho adimu cha vitamini K ambacho hakipatikani kwenye mboga nyingi.
“Ni miongoni mwa mmea wenye vitamini C nyingi, vitamini K ambayo ni ‘very rare’ (adimu sana) kuipata. Vitamini K inapatikana kwenye vyakula vichache, ina madini ya chuma, vitamini D, A.
…Lakini pia ina madini mengi ina kalsium, magnesium, potassium,” amesema Irine Kweka, Afisa Lishe kutoka Hospitali ya Kondoa jijini Dodoma.
Hata hivyo, Kweka ameongeza kuwa sifa kubwa ya brokoili uwepo wa antioxidanti nzuri kulingana na uwepo wa vitamini.
Kwanini ule brokoli?

Ikiwa bado unajiuliza sababu za kuongeza brokoli katika mlo wako wa kila siku Kweka aliyekuwa akizungumza na Nukta Habari amebainisha kuwa moja aya faida ya kutumia mboga hiyo katika mlo ni kusaidia mmeng’enyo wa chakula kulingana na wingi wa nyuzinyuzi.
Nyuzi nyuzi hizo pia husaidia tatizo la choo kigumu, kudhibiti kiwango cha asidi kwenye tumbo, kukabiliana na kiungulia au vidonda vya tumbo,pamoja na kuongeza idadi ya bakteria wazuri tumboni, ambao ni muhimu kwa usagaji bora wa chakula.
Bakteria hawa husaidia kuvunjavunja chakula kwa ufanisi na pia huchangia katika afya bora ya kinga ya mwili.
Kuzuia magonjwa ya moyo
Ulaji wa Brokoli husaidia kupunguza viwango vya lehemu (cholesterol) mbaya (LDL) na kuongeza lehemu nzuri (HDL), hali inayosaidia kupunguza hatari ya kupata magonjwa ya moyo.
Kwa mujibu wa tovuti ya masuala ya afya, Medical News Today brokoli ina nyuzi nyuzi, antioksidanti, na kemikali za kibaolojia zinazopunguza kiwango cha ehemu na kudumisha utendaji mzuri wa moyo.

Uwepo wa nyuzi nyuzi hizo kwa wingi, husaidia kuzuia kuziba kwa mishipa ya damu kwa kupunguza kiasi cha mafuta mabaya mwilini hali inayoweza kupunguza uwezekano wa kupata shinikizo la damu, kiharusi, na mshtuko wa moyo.
Kuimarisha afya ya mifupa
Tovuti ya Naturmed Scientific inaeleza kuwa mifupa yenye nguvu inahitaji virutubisho muhimu kama vile kalsiamu, fosforasi, na vitamini K, vyote ambavyo hupatikana kwa wingi katika brokoli.
Vitamini K inasaidia katika mgandisho wa damu na pia huchangia uimarishaji wa madini kwenye mifupa, jambo ambalo linapunguza uwezekano wa mifupa kuwa dhaifu au kuvunjika kwa urahisi.

Mifupa yenye nguvu inahitaji virutubisho muhimu kama vile kalsiamu, fosforasi, na vitamini K ambavyo pia hupatikana kwenye brokoli. Picha/ La Muscle.
Pia, brokoli ina kiasi kikubwa cha madini ya magnesiamu na zinki, hali inayowafanya walaji wa brokoli kupunguza msongamano wa mifupa (osteoporosis), unaochangia mifupa kuwa dhaifu na rahisi kuvunjika.
Kinga dhidi ya saratani
Taasisi ya kansa ya nchini Marekani (National Cancer Institute) inabainisha kuwa brokoli ina kemikali zinazozuia ukuaji wa seli zenye uwezo wa kusababisha saratani.
Tafiti mbalimbali zimeonesha kuwa ulaji wa mara kwa mara wa mboga za jamii ya ‘cruciferous’, ikiwemo brokoli, unaweza kupunguza hatari ya saratani ya matiti, saratani ya tezi dume, na saratani ya utumbo mpana.

Mbali na kinga dhidi ya saratani, brokoli pia inasaidia wagonjw wa saratani kupunguza madhara yanayotokana na matibabu kama mionzi na dawa za kemikali.
Kuimarisha afya ya ngozi
Ngozi yenye afya inahitaji lishe bora, na brokoli ni moja ya vyakula vinavyotoa virutubisho muhimu kwa ngozi.
Vitamini C inayopatikana kwa wingi kwenye brokoli inasaidia mwili kutengeneza collagen, ambayo ni protini muhimu kwa uimara na mng’ao wa ngozi.

Brokoli pia ina vioksidishaji vinavyosaidia kupunguza athari za miale ya jua ambayo inaweza kusababisha uharibifu wa ngozi huku vitamini A na E, vilivyopo katika mboga hiyo ambavyo vikiifanya ngozi kuwa naunyevu wa kutosha.
Kudhibiti sukari ya damu
Kwa watu wenye ugonjwa wa kisukari, brokoli ni moja ya vyakula vinavyopaswa kujumuishwa katika lishe. Ina misombo inayosaidia kudhibiti viwango vya sukari kwenye damu kwa kupunguza upinzani wa insulini.
Uwepo wa sulforaphane inayopatikana kwenye brokoli inaweza kusaidia kupunguza viwango vya sukari kwa wagonjwa wa kisukari aina ya pili.

Sulforaphane husaidia kongosho kutoa insulini kwa ufanisi zaidi na hivyo kudhibiti sukari mwilini.
Mbali na hayo, nyuzinyuzi zilizopo kwenye brokoli husaidia kupunguza kasi ya mmeng’enyo wa wanga, na hivyo kuzuia kuongezeka kwa ghafla kwa kiwango cha sukari baada ya kula.
Hii ni muhimu kwa watu wanaotaka kudhibiti uzito na kuepuka hatari ya kupata kisukari.
Kusaidia kuzuia mchakato wa kuzeeka
Mchakato wa kuzeeka kwa kiasi kikubwa unahusishwa na mkazo wa oksidativi na kupungua kwa kazi ya kimetaboliki wakati wa maisha ya binadamu.
Ingawa kuzeeka ni mchakato wa asili usioepukika, ubora wa lishe unadhaniwa kuwa na mchango mkubwa katika kuamua jinsi jeni zinavyotumika na maendeleo ya magonjwa yanayohusiana na umri

Ili kuhifadhi virutubisho vyake, ni vyema kupika brokoli kwa muda mfupi kwa kutumia njia kama kuipika kwa mvuke au kuitumia katika saladi. Kwa kuongeza brokoli katika lishe yako ya kila siku, unaweza kufurahia afya bora na kuzuia magonjwa mbalimbali.
Nchi 10 Afrika zilizopokea msaada mkubwa sekta ya afya kutoka USAID 2023
Kwa miaka mingi, Shirika la Maendeleo la Kimataifa la Marekani (USAID) limekuwa msaada wa huduma za afya barani Afrika, likifadhili mapambano dhidi ya VVU/UKIMWI, kifua kikuu, magonjwa ya mlipuko, na kuboresha mifumo ya afya.
Kwa mujibu wa Shirika la Misaada la Serikali la Marekani (Foreign Assistant Government) nchi 10 zilizonufaika zaidi kwa mwaka 2023 ni Kenya, Nigeria, Tanzania, Uganda, Ethiopia, Msumbiji, Zambia, Afrika Kusini, Malawi, na DRC, ambapo misaada hii imewezesha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba, lishe bora, na huduma za afya ya uzazi.
Tanzania ni nchi iliyoongoza kwa kupokea msaada mkubwa katika sekta ya afya kutoka USAID ikipokea takriban Dola milioni 512.8 za Marekani, sawa na Sh1.32 trilioni.
Hata hivyo, kusitishwa kwa misaada hii kunaweza kuwa na athari kubwa katika nchi hizi kwa kukabiliwa na uhaba wa dawa za Virusi vya Ukimwi (VVU) na Upungufu wa Kinga Mwilini (UKIMWI), lishe, kifua kikuu, magonjwa ya mlipuko na vitisho vipya vya kiafya, vifaa vya afya, uzazi wa mpango na afya ya uzazi, usafi wa maji, pamoja na miradi mingine ya afya.
Bila ufadhili wa USAID, nchi hizi zinapaswa kutafuta vyanzo mbadala vya rasilimali ili kuzuia madhara kwa mamilioni ya watu wanaotegemea huduma hizi. Lakini je, mataifa haya yana uwezo wa kuziba pengo hili haraka? Ikiwa suluhisho halitapatikana, mustakabali wa afya barani Afrika unaweza kuwa hatarini.

Ifahamu mikoa 10 inayoongoza kwa uzazi wa mpango Tanzania
Dar es Salaam. Miongoni mwa masuala yanayogusa zaidi vijana wengi waliopo kwenye ndoa na wasio kwenye ndoa kwa sasa ni suala la kuwa na watoto.
Miongoni mwa maswali makubwa huwa ni lini wapate watoto, idadi ya watoto lakini ni njia gani sahihi itakayomfanya wanawake vijana wasipate ujauzito bila kutarajia. Wataalamu wanasisitiza kuwa ni vema wazazi vijana wakapanga mipango yao vema ya kijamii na kiuchumi kabla ya kupata watoto.
Hata hivyo, si watu wote wanapanga ipasavyo juu ya kupata watoto. Utafiti wa Afya ya Uzazi na Mtoto na Viashiria vya Malaria wa mwaka 2022 unabainisha kuwa nchini Tanzania takriban wanawake wanne kati ya 10 au asilimia 38 ya waliolewa wenye umri wa miaka 15 hadi 49 wanatumia njia ya aina yeyote ya uzazi wa mpango.
Ripoti ya utafiti huo uliofanywa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS) kwa ushirikiano na taasisi nyingine iwepo Wizara ya Afya inabainisha ipo baadhi ya mikoa yenye kiwango kikubwa cha wanawake wenye wanaotumia ipasavyo njia za uzazi wa mpango ikiongozwa na Njombe huku mingine ikitumia kwa kiwango kidogo sana kama Simiyu.
Je, waifahamu mikoa inayoongoza kwa matumizi ya njia za uzazi wa mpango Tanzania?
Ulaji milo mitatu ya chakula bado kitendawili Tanzania
- Idadi ya wanaokula milo mitatu yashuka kwa asilimia 8.2.
- Mtanzania mmoja kati ya 10, anakula mlo mmoja wa chakula.
- Uviko -19, uhaba wa chakula baadhi ya maeneo vyatajwa kama sababu.
Dar es Salaam. Wakati wataalamu wa afya wakihimiza kula milo mitatu ya chakula kwa siku au zaidi ili kuwa na afya bora, hali ni tofauti nchini Tanzania kwani idadi ya watu wanaokula milo mitatu kwa siku imeshuka kwa asilimia 8.2.
Kwa mujibu wa Ripoti ya Kufuatilia Hali ya Kaya Tanzania (NPS) ya mwaka 2020/21 iliyotolewa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), idadi ya Watanzania wanaokula milo mitatu imeshuka kutoka asilimia 71.2 mwaka 2014/15 mpaka asilimia 63 mwaka 2020/21.
Hii ni kumaanisha kuwa kati ya Watanzania kumi ni sita ndio wanaokula milo mitatu ya chakula au zaidi kwa siku.
Wakati idadi ya wanaokula milo mitatu au zaidi ikishuka, idadi ya wanaokula milo miwili hadi mmoja imeongezeka. Mathalani wanaokula mlo mmoja wameongezeka kutoka asilimia 0.6 mpaka 1.6 huku wanaokula milo miwili wakiongezeka kutoka 28.2 mpaka 35.4.
Uchambuzi wa takwimu uliofanywa na Nukta habari umebaini kuwa kwa mujjbu wa ripoti hiyo katika kila Watanzania kumi basi mmoja hula mlo mmoja tu wa chakula huku watatu kati ya 10 wakila milo miwili ya chakula.
Hata hivyo, hali ya ulaji wa chakula imeonekana mbaya zaidi katika maeneo ya vijijini kuliko mjini kwani, Watanzania waishio mjini wana wastani mzuri zaidi wa kula milo mitatu kwa asilimia 74.8 huku vijijini wakiwa na asilimia 57.3.
Vivyo hivyo, idadi ya wanaokula mlo mmoja vijijini ni kubwa zaidi ambao ni asilimia 1.8 wakati mjini ni 1.2 huku asilimia ya wanaokula milo miwili vijijini ikiwa ni mara mbili zaidi ya wale waishio mjini.
Huenda hali hiyo imechangiwa na kuwepo kwa upungufu wa chakula katika baadhi ya maeneo hapa nchini hali iliyosababishwa na mtawanyiko wa mvua pamoja na visumbufu.
Soma zaidi
- Vyakula vinavyoimarisha kumbukumbu, uelewa wa kimasomo kwa watoto
- Mwaka 2022 umekuwa mgumu familia kuweka mlo mezani: UNCTAD
Kwa mujibu wa Taarifa ya Hali ya Chakula nchini ya mwaka 2020/21 imeeleeza kuwa pamoja na kuwa na ziada ya chakula halmashauri 17 kutoka mikoa nane nchini ilitarajiwa kukutana na uhaba wa chakula mwaka juzi.
“Upungufu huo umechangiwa na sababu mbalimbali ikiwemo mtawanyiko mbaya wa mvua, visumbufu vya mimea kama vile wanyamapori, ndege aina ya kwelea kwelea na viwavijeshi vamizi, ” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.
Aidha uwepo wa ugonjwa wa Uviko-19 uliathiri shughuli za kilimo kwani ulisababisha changamoto katika upatikanaji wa pembejeo muhimu za kilimo kama vile mbegu, mbolea, viuatilifu na zana za kilimo.
Janga hilo lilichangia watu kupoteza ajira na biashara, na hivyo kukosa kipato kwa ajili ya kukidhi ya mahitaji ya kila siku ya chakula.
Tangazo:
Kraken: Kirusi kipya cha Uviko-19 kinachowatesa wanasayansi
- Kinatajwa kuenea kwa kasi zaidi kuliko virusi vilivyopita.
- Uwezo wa kubadili jeni zake ni miongoni mwa sababu.
- Barakoa yatajwa kama njia bora zaidi ya kujikinga na kirusi hicho.
Dar es Salaam. Ingawa si jambo linalozungumzwa sana kwa sasa, lakini wasiwasi unaendelea kuongezeka kwa wanayansi ambao wanajaribu kutafuta ufumbuzi wa kukabiliana na makali ya kirusi kipya cha Uviko-19 ambacho kinaenea kwa kasi barani Ulaya.
Kirusi hicho kinachoitwa XBB.1.5 au Kraken ni matokeo ya mabadiliko ya kijeni ya kirusi aina ya Omicron XBB ambacho nacho kiliripotiwa kuwa na kasi kubwa katika kuenea kwake.
Kwa mujibu wa Shirika la Afya Duniani (WHO), kirusi hicho kiliripotiwa kwa mara ya kwanza Oktoba 2022, nchini Marekani na sasa tayari kimeenea katika nchi 38 barani Ulaya ikiwemo Sweden, Kanada, Australia na Ufaransa.
Disemba mwaka jana, China ilitangaza kuwa wastani wa watu 60,000 walipoteza maisha kutokana na virusi vya Omicron aina ya BA.5.2 na BF.7 vilivyozuka nchini humo.
Soma zaidi:
- Tanzania na Uviko-19: Maambukizi yaongezeka kwa asilimia 62
- Watanzania wahimizwa kujikinga dhidi ya magonjwa ya mfumo wa hewa
Mapema Januari mwaka huu Mkurugenzi wa masuala ya Teknolojia kutoka WHO, Maria Van Kerkhove alisema kirusi hicho ndiyo kinaambukiza kwa kasi zaidi kuliko aina nyingine za virusi.
“Sababu kubwa ni kutokana na kirusi hiki kuwa na uwezo wa kubadilisha jeni zake mara kwa mara hivyo si rahisi kukidhibiti,” anasema Kerkhove.
Pamoja na kwamba kirusi hichi kinaenea kwa kasi bado hakuna uhakika kwamba kinaweza kusababisha maafa makubwa kuliko ilivyokuwa awali.
Kutokana na uwezo wa kirusi hicho kujibadili mara kwa mara kulingana na mazingira wataalamu wa afya wameshauri pamoja na chanjo ya uviko-19 njia inayotajwa kuwa na uhakika zaidi ni kuvaa barakoa muda wote mtu anapokuwa kwenye mikusanyiko.
Kwa mujibu wa Kituo Cha Kudhibiti Magonjwa nchini Marekani (CDC) mpaka sasa asilimia 43 ya visa vya maambukizi ya Uviko-19 nchini humo yamesababishwa na kirusi hicho kipya.
Tangazo