Maeneo ya kujivinjari Dar, Pwani na Zanzibar mwisho wa mwaka

Dar es Salaam. Mwisho wa mwaka ni kipindi maalum ambacho wengi hutumia kujivinjari na kupumzika baada ya shughuli nyingi za mwaka mzima.

Kwa wakazi wa mikoa ya Dar es Salaam na Pwani na visiwa vya Zanzibar yapo baadhi ya maeneo ambayo unaweza kuyatumia kupumzika na kutuliza akili. Maeneo hayo yana vivutio vya kipekee ambavyo vimekuwa vikiwavutia watu ndani na nje ya nchi.

Nukta Habari  imekuandalia mapendekezo ya maeneo ya kujivinjari ambayo yanaweza kukufaa katika msimu huu wa sikukuu za mwisho wa mwaka. Twende pamoja! 

Kama wewe ni mkazi wa Dar es Salaam, maeneo haya yanaweza kuwa chaguo sahihi:

Fukwe za bure

Licha ya kuwa ni jiji kubwa na lenye shughuli nyingi za kibiashara, zipo fukwe mbalimbali unazoweza kutembelea bila kiingilio. 

Fukwe hizo ni Ununio beach inayopatikana mita chache kutoka kituo cha daladala  cha Ununio. Coco beach iliyo kilomita moja na nusu kutoka kituo cha mabasi cha Macho kilichopo Msasani. Ukiwa hapo utaweza kufaidi chakula maarufu cha mihogo  iliyochomwa au kukaangwa kwa ustadi ambayo mara nyingi huliwa kwa mishikaki au samaki.

Pia unaweza kwenda Rungwe beach inayopatikana Kunduchi, mita moja na nusu kutoka kituo cha mabasi cha Silver Sand. Bara beach inayosifika kwa mazingira mazuri ya kupiga picha iliyopo Kilomita moja kutoka kituo cha mabasi Kondo, Ununio nayo ni sehemu sahihi.

Mwonekano wa fukwe ya Rungwe iliyopo Kunduchi, mita moja na nusu kutoka kituo cha mabasi cha Silver Sand. Picha |Erick Nishael

Kwa wakazi wa Kigamboni, Pweza beach iliyopo iliyopo mita 10 kutoka barabara kuu inayoelekea Kibada nayo ni sehemu sahihi. Fukwe hizi zinafaa kwa mapumziko na shughuli nyingine za kijifurahisha ikiwemo kuogelea, kupunga upepo, mazoezi ya viungo, matembezi ya ufukweni na michezo ya watoto.

Mbali na fukwe za kula kipupwe bure, kuna vivutio vya asili, kihistoria, na kitamaduni kama visiwa vya Bongoyo, Mbudya na Pangavini maarufu kwa safari za boti, kupiga mbizi na kupumzika. 

Visiwa hivyo vina mandhari ya misitu ya asili na miamba ya matumbawe yenye rangi za kuvutia. 

Kama unataka kuongeza maarifa ukitalii Makumbusho ya Taifa yaliyopo Posta yamehifadhi mabaki ya kihistoria ya Tanzania. Pia Kijiji cha Makumbusho barabara ya Bagamoyo kinaonyesha maisha ya kitamaduni, michezo na sanaa za makabila zaidi ya 100 ya Tanzania.

Pia kuna vivutio vya kihistoria vinavyobeba urithi wa ukoloni, kama vile Msikiti wa Mtoro na Kanisa la St. Joseph, ambavyo vinaonyesha ushawishi wa Waarabu na Wazungu katika mkoa huu.

Machimbo ya filamu

Kama furaha haitimiliki bila kuangalia muvi basi jipange kutembelea miongoni mwa machimbo ya kijanja mjini yanayotumia teknolojia ya kisasa na kuonesha filamu mpya kila siku.

Unaweza kwenda Century Cinemax, ndani ya Mlimani City. Cinemax iliyopo Masaki ndani ya Aura Mall, kitu cha pekee kwenye hili chimbo ni kioo cha kuonesha filamu chenye ubora wa 4K huku mfumo wa sauti ikitumia teknolojia ya ‘Dolby Atmos’ kutoa sauti kutoka pande zote ndani ya ukumbi. 

Kama barabara ya Pugu ni rahisi kufikika kwako, Suncrest Cineplex ndani Quality Center Mall panaweza kukufaa kwa mazingira yake ya kisasa na tulivu. Filamu huoneshwa kwenye mwonekano wa hali ya juu (HD) na teknolojia bora ya sauti. 

Kama Mbezi Beach ni karibu unaweza kutembelea Silversands Cinema, ndani ya Silversands Hotel, kumbi iliyoboreshwa kuonesha filamu kwa teknolojia ya kisasa inayokidhi viwango vya kimataifa. Chimbo jingine ni Cineplex ndani ya Dar Free Market, Oyster Bay, ikitumia teknolojia ya 3D na mfumo wa kisasa wa sauti. 

Shughuli za manunuzi

Kwa kuzingatia msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka umewadia, Dar es Salaam inatoa fursa mbalimbali kwa wenyeji na wageni kujivinjari kupitia manunuzi ya bidhaa katika maduka makubwa. 

Mojawapo ni Mlimani City Mall, lililopo Ubungo, karibu na Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, ndani utapata maduka mbalimbali yanayouza bidhaa za kimataifa na za ndani. 

Baadhi ya maduka maarufu ukiwa Mlimani City ni pamoja na Game Store, Mr. Price, Miniso, Woolworths, Jet, LC Waikiki, Samsung Store yanayouza bidhaa za nyumbani, vifaa vya umeme, mavazi ya kisasa kwa watoto, vijana, na watu wazima na bidhaa za urembo.

Maduka makubwa ya nguo za mitindo na chapa maarufu dunuani yaliyopo Mlimani City. Picha |Mlimani City

Aura Mall, iliyopo Masaki, ni chaguo jingine kwa mpenzi wa mitindo na bidhaa za nyumbani. Duka hili linauza bidhaa za chapa maarufu za vifaa vya nyumbani, mapambo, mavazi na zawadi unazoweza kugawa kwenye msimu wa sikukuu. 

Kwa wanaopendelea bidhaa za utamaduni wa kipekee, Slipway Shopping Village, Oyster Bay, ni mahali sahihi. Maduka ya yanauza bidhaa kama vito vya mikono, kazi za sanaa za Kiafrika na mapambo ya ndani. 

Maduka mengine ni Shoppers Plaza yaliyo Masaki na Mikocheni. GSM Mall yaliyopo Mikocheni karibu na Ubalozi wa Marekani, barabara ya Pugu na Salamander Tower mtaa wa Mkwepu.

Klabu maarufu za starehe 

Jijini Dar es Salaam kuna klabu nyingi za starehe zinazovutia wakazi na wageni kula bata raha mstarehe. Mojawapo ni Elements iliyopo Oysterbay, mahali pazuri kwa wale wanaopenda muziki wa live, DJs maarufu na burudani za kiwango. 

Klabu nyingine ni Next Door Arena, George & Dragon, Rhapsody’s, Jade Night Club, The Slow Leopard zilizopo Masaki. Samaki Samaki Lounge na Level 8 Rooftop Lounge ndani ya Hyatt Regency, Posta na Escape One, Mikocheni.

Migahawa ya chakula na vinjwaji

Baadhi ya migahawa inayovutia watu wengi ni The Waterfront Sunset na Cape Town Fish Market, iliyopo Masaki, maarufu kwa vyakula vya baharini na kimataifa sambamba na mandhari inayovutia ya bahari. 

Kwa wapenda burudani na vyakula vya baharini, Samaki Samaki, Kariakoo na Masaki ni chaguo bora, na Breakpoint, Mwenge.

Kama unafurahia upekee wa mandhari, The Slipway Waterfront na Akemi Revolving Restaurant ni sehemu zinazoweza kukidhi haja yako huku ukifurahia mwonekano wa jiji na bahari. Kwa ladha za Kiafrika, fika Addis in Dar, Masaki kwa vyakula tofauti ikiwemo vya Kihabeshi kama Injera.

Michezo ya watoto

Kama unatafuta maeneo ya kuwapeleka watoto kujivinjari, jiji hili lina sehemu mbalimbali zinazotoa burudani na michezo ya kuvutia kwa watoto wa rika tofauti kama Fun City Kigamboni, Kunduchi Wet ‘N’ Wild Water Park. Mlimani City Play Zone, Slipway Playground, Msasani Peninsula. Sea Cliff Village Play Area, Oysterbay na Diamond Jubilee Hall Playground, Upanga.

Mwonekano wa eneo la watoto kufurahia michezo ya maji lililopo Kunduchi Wet ‘N’ Wild Water Park, Dar es Salaam. Picha |Wetnwild

Maeneo hayo watoto wanaweza kufaidi michezo ya bembea, kuogelea, kuruka, kuendesha magari. 

Mkoa wa Pwani

Kwa wale wanaopenda safari za kitalii kama sehemu ya mapumziko ya mwisho wa mwaka, Mkoa wa Pwani kuna fursa adhimu za kufurahia uzuri wa asili na utamaduni.

Hifadhi ya Taifa ya Saadani ambayo ina upekee wa kupakana na bahari ya Hindi, ikiwa na ndege, wanyama wa baharini kama nyangumi, kasa wa kijani, na pomboo. Hifadhi hii utaipata Wilaya ya Bagamoyo.  

Pori la Akiba la Selous linalopatikana upande wa kusini mwa mkoa huo, likienea katika wilaya za Rufiji na Kisarawe, ni makazi ya simba, twiga, viboko, faru, pundamilia, na wanyama wengine wengi. Utaweza kufaidi vivutio maarufu hususan kambi za kitalii kama ‘Stiegler’s Gorge’ na ‘Mbuyu Camp’ pamoja na maeneo maalum ya kutazama wanyama.

Pia kuna hifadhi ya baharini ya Kisiwa cha Mafia chenye mchanga mweupe kwa asilimia 85, viumbe wa baharini kama matumbawe na samaki sambamba na uvuvi wa michezo. Mji wa Kale wa Bagamoyo, kitovu cha historia na utalii wa maeneo kama Kanisa la Kale, Soko la Watumwa, na Magofu ya Kaole huko nako ni sehemu sahihi unazoweza kufika. 

Mkoa wa Pwani una maeneo kadhaa yenye mazingira rafiki kwa watoto kufurahia michezo na kujifunza. Baadhi ni Eco Park Bagamoyo, Lazy Lagoon Island Lodge, Kibaha Family Park, Kaole Forest Reserve na hoteli nyingi za kitalii kama Bagamoyo Beach Resort, zinazotoa huduma maalum kwa watoto.

Maeneo haya watoto wanaweza kufurahia kwa michezo ya mpira wa miguu, mabwawa madogo ya kuogelea, kuunda majumba ya mchanga, kujifunza kuhusu wanyama wa asili na mazingira.

Coral beach club ndani ya Bagamoyo ni kiwanja cha maana kama unataka burudani za muziki wa moja kwa moja na vinywaji vya kiwango cha kimataifa.

Pia kuna Pwani Social Lounge, maarufu kwa burudani za usiku za muziki wa bendi za moja kwa moja, na Bagamoyo Art Club ukihitaji sehemu inayochanganya sana kwa matamasha ya muziki na onyesho la utamaduni wa Kiswahili.

Tembo wakitembea pembezoni mwa ufukwe wa bahari ya Hindi kwenye hifadhi ya Saadani. Picha | Tanzania Specialist.

Migahawa Maarufu

The fish eagle restaurant (Bagamoyo) ukipenda vyakula vya baharini, vikiwa vimeandaliwa kwa ladha tofauti. Chaza Grill (Pwani Mkuza) maarufu kwa nyama choma, samaki wa kukaanga, na pilau, huku likiwa na mazingira ya familia kupoa. Sambamba na Bagamoyo beach view restaurant kwa vyakula vya asili vya Mtanzania na matunda ya msimu.

Utalii wa Ndani

Kama wewe ni mpenzi wa vivutio vya utalii basi Hifadhi ya Taifa ya Saadani yenye upekee wa eneo linalounganisha pori na pwani, hapo utaweza kuona wanyama kama nyani wakati umepumzika kando ya bahari. Sambamba na fukwe za mapumziko kama Nunge na Kaole Beach, Bagamoyo.

Maduka Makubwa

Miongoni mwa maeneo ya manunuzi ni Pwani plaza (Kibaha), na Kibaha Mall, maduka maarufu kwa ununuzi wa nguo, bidhaa za kielektroniki, na migahawa yenye vyakula vya haraka, pia Bagamoyo Craft Market zinapouzwa bidhaa za sanaa bunifu kama vinyago, mikoba, na vazi la batiki.

Kama Dar es Salaam na Pwani siyo chaguo lako basi Zanzibar inaweza kukufaa zaidi.

Miaka ya hivi karibuni sifa ya Zanzibar kama kituo cha utalii kwa wageni wa kimataifa zimeendelea kupaa, si bure ni kwa sababu ya mandhari yake ya kitalii na majengo yaliyobeba historia ya kuvutia.

Ina fukwe bora zaidi Afrika maarufu kwa mchanga wake laini na mweupe ikiwemo Kendwa, iliyochaguliwa kuwa fukwe bora Afrika na ya nne kwa ubora duniani kote.

Nyingine maarufu ni za Nungwi, Matemwe, Kiwengwa, Pongwe, Pingwe, Dongwe, Bwejuu, Paje, Jambiani, Kizimkazi, Michamvi-Kae, Makunduchi, Mtende na Nakupenda.

Mwonekano wa fukwe za Zanzibar, kutoka kushoto ni Kendwa ikifuata Mnemba na Nakupenda beach. picha |Tripadvisor

Zaidi ya fukwe 25, zinazopatikana upande wa kaskazini mwa kisiwa hicho zimechangamka zaidi kwa shuguli za utalii, wingi wa watu na malazi. Fukwe za mashariki ni tulivu na zinafaa kwa wapiga mbizi na michezo ya baharini, 

Msitu wa Jozani

Upo umbali wa kilometa 35 kutoka kusini mashariki mwa kisiwa cha Unguja katika ghuba ya Chwaka. Ndani yake utakutana na vitutio vya kipekee likiwemo daraja la mikoko iliyoshonana na kunawiri vizuri kwenye maji chumvi yaliyoko chini ya daraja hilo la mbao.

Pia kuna miti tofauti kama mitondoo, mivinje, mikaratusi, mikonge, mikangara shamba na misiliza  Msitu huu pia una wanyama ambao hupatikana ndani yake pekee kama Chura wa jozani, chui wa Zanzibar, jongoo wa jozani, paa nunga na kima punju.

Maandalizi na tahadhari

Hakikisha una bajeti ya kutosha ya kulipia bidhaa, chakula au burudani unayopanga kuipata . Zingatia kuwa kila eneo lina vitu vya bei tofauti kulingana na hadhi yake.

Mengi ya maeneo tuliyotaja hapo huu huwa na msongamano mkubwa wa watu mwishoni mwa mwaka. Panga mapema ratiba zako kutembelea eneo litakalokuvutia kuepuka msongamano.

Ni muhimu kuzingatia tahadhari zote za usalama unapokuwa katika fukwe hasa Dar es Salaam na Zanzibar ili umalize mwaka kwa furaha na amani.

Enable Notifications OK No thanks