Matukio ya ulaghai mtandaoni yashuka kwa asilimia 25
- Mtwara yavunja rekodi ya kuwa na matukio machache zaidi ikiwa na matukio 25.
Dar es Salaam. Huenda watumiaji wa mitandao wakaondokana na changamoto ya ulaghai mtandaoni baada ya pungua kwa matukio hayo kwa asilimia 25 ndani ya kipindi cha miezi mitatu.
Kwa mujibu wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), ulaghai mtandaoni ni kitendo cha kutumia intaneti, simu, au mitandao ya kijamii kuiba pesa, taarifa za siri, ama kudanganya watu.
Ulaghai huu unaweza kufanyika kwa njia ya ujumbe wa uongo (kutumiwa SMS za kuomba fedha au kudanganya umeshinda zawadi), wizi wa nenosiri (kuombwa kutoa namba ya siri au namba ya uthibitisho – OTP) pamoja na kutumia viungo feki.
Takwimu za mawasiliano za robo ya mwaka inayoishia Juni 2026 zinazotewa na TCRA, zinaonesha ulaghai umepungua kutoka matukio 9,816 yaliyoripotiwa robo mwaka inayoishia Machi 2026 hadi kufikia matukio 7,334 katika robo ya mwaka inayoishia Juni 2026.
Kwa takwimu hizi ni sawa na kusema matukio 2,482 hayajaripotiwa ndani ya miezi mitatu iliyopita suala linalotoa ahueni kwa wananchi.
Rukwa kinara

Ripoti ya TCRA inabainisha kuwa mkoa ya Rukwa unaongoza kwa majaribio ya ulaghai ikiwa na matukio 2,495, zaidi ya robo tatu ya majaribio yote ya ulaghai nchini.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa mkoa huo umekuwa kinara kwa ulaghai kwa zaidi ya miaka mitano, ukipanda au kushuka kila baada ya miezi mitatu.
Licha ya kuwa kinara, takwimu za TCRA zinabainisha kuwa ulaghai mtandaoni katika mkoa wa Rukwa unapungua karibu kila mwezi suala linalotoa ahueni kwa wakazi wa eneo hilo.
Mathalan, katika ripoti ya robo ya kwanza 2025 matukio 7,385 yalirekodiwa mkoani Rukwa, yaliyopungua na kufikia matukio 3,444 katika robo ya pili, 2025.
Mbali na Rukwa, mkoa wa Morogoro umeshika nafasi ya pili kwa kurekodi matukio 2,129 huku wilaya ya Kilombero ikiripoti matukio 1,781 ambayo ni zaidi ya nusu ya matukio yaliyorekodiwa na mkoa mzima.
Mikoa mingine iliyoongoza kwa kuripoti matukio ya ulaghai kwa njia ya mtandao ni Dar es Salaam ikishika nafasi ya tatu ikiwa na matukio 615, ikifuatiwa na Mbeya yenye matukio 370.
Kwa upande wa mikoa iliyorekodi matukio machache zaidi ya ulaghai wa mtandaoni ni Shinganya ikiwa na matukio 33, ikifuatiwa na Lindi matukio 31 na Mtwara ikishika mkia kwa kuwa na matukio machache zaidi ikiwa na matukio 25.
Kwa upande wa Zanzibar mkoa wa Mjini Magharibi ndio umeongoza kwa majaribio ya utapeli kwa njia ya mtandao ukiwa na jumla ya matukio 35 huku Mkoa wa Kusini unguja ukifuata kwa kuwa na matukio 5.
Mtandao wa Yas waongoza

Ripoti ya TCRA inaonesha baadhi ya makampuni yanayo toa huduma za mawasiliano nchi yaliyorekodi kiwango kikubwa zaidi cha majaribio ya uhalifu.
Mtandao wa Yas ndiyo iliyorekodi idadi kubwa zaidi ya majaribio katika robo iliyoishia Juni, 2026 ikiwa na jumla ya matukio 2,306, sawa na asilimia 31.4 ya matukio yote.
Licha ya kuwa na idadi kubwa zaidi, Yas ilipunguza idadi ya matukio hayo kutoka 2,659 yaliyo rekodiwa miezi mitatu iliyopita hadi matukio 2,306, TTCL inafuata ikiwa na matukio 2,039, sawa na asilimia 27.8, huku Vodacom ikiwa na matukio 1,364, Airtel 1,053 na Halotel 572.
TTCL ilirekodi punguzo kubwa zaidi kwa asilimia, kutoka matukio 3,375 hadi 2,039, sawa na asilimia 39.59, kwa upande wa Vodacom matukio yalipungua kwa asilimia 27.56, huku Airtel matukio yakipungua kwa asilimia 24.73.
Wakati mitandao mingine ikirekodi kupungua kwa matukio, Halotel ndiyo iliyokwenda kinyume na mwenendo wa jumla, ikiripotiwa kuwa na matukio yaliyoongezeka kutoka 500 hadi 572 ikiwa ni sawa na ongezeko la matukio kwa na asilimia 14.4
Mapambano yanaendelea
Waziri wa Mawasiliano na Teknolojia ya Habari Angellah Kairuki aliyekuwa akizungumza katika uzinduzi wa ripoti hiyo amesema kupungua kwa matukio ya ulaghai wa mtandao nchini, kunatokana na jitihada za wazi za Serikali pamoja na wadau wa mawasiliano katika kukabiliana na tatizo hilo.
“Kupungua huku kwa matukio ya ulaghai kunatokana na upekuzi na ukaguzi mbalimbali zilizofanywa na TCRA kwa kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama kupitia Wizara ya Mambo ya Ndani, pamoja na wadau wa mawasiliano katika mikoa ya Dar es Salaam, Arusha, Mbeya na Mara zikiwalenga wahusika ambao wanafanya matukio ya ulaghai nchini…,” amesema Kairuki.
Kwa upande wa watumiaji wa mitandao ya simu amewahimiza kutoa taarifa za majaribio ya utapeli wanapokutana nayo kupitia namba 15040 ili zifuatiliwe na hatua za kisheria zipate kuchukuliwa ikiwemo kuzifungia namba hizo.
Aidha, Kairuki amesema Serikali inaendelea na kampeni mbalimbali zenye kuongeza uelewa na usalama kwa watumiaji wa huduma za kimawasiliano ikiwemo ‘futa au delete kabisa’ na ‘sambaza mchongo sio uongo’ inayosisitiza kutosambaza taarifa zisizo sahihi kwenye majukwaa ya kidigitali.
Fursa au changamoto, idadi ya vituo vya kubadili fedha za kigeni ikipaa Tanzania
- Imeongezeka zaidi ya mara 16 ndani ya kipindi cha miaka mitano.
Dar es Salaam. Kwa miji mikubwa ya utalii na biashara kama Arusha, Zanzibar na Dar es Salaam ni kawaida kukutana na mabango ya vituo vya kubadilisha fedha za kigeni vinavyowawezesha mamia ya wazawa na wageni kupata huduma hizo za kifedha.
Miaka michache tu iliyopita huduma hizo zilikuwa zikitolewa kupita matawi ya kibenki au vituo vichache vilivyokuwepo katika miji mikubwa pekee au katikati ya miji.
Kwa sasa hali hiyo imebadilika, baada ya kuongezeka kwa vituo hivyo zaidi ya mara 16 ndani ya kipindi cha miaka mitano.

Ripoti ya Usimamizi wa Sekta ya Fedha mwaka 2025 inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inabainisha kuwa vituo vya kubadilisha fedha za kigeni vimefikia 65 mwaka 2025 kutoka vituo vinne vilivyokuwepo mwaka 2021.
Hii ni sawa na kusema idadi ya vituo hivyo muhimu katika sekta ya uchumi imepaa kwa asilimia 1,525, jambo linaloashiria kupanuka kwa upatikanaji wa huduma rasmi za kubadilisha fedha za kigeni nchini.
NBS inafafanua kuwa vituo vinne vilivyokuwepo mwaka 2021, vilikuwa na matawi 40, pamoja na benki za biashara 34 vikiongezeka hadi vituo 65 vyenye matawi 182, benki 35 za kibiashara na hoteli 12 mwaka 2025.
Wakati vituo vya kubadilisha fedha za kigeni vikiongezeka BoT inabainisha kuwa mauzo ya fedha za kigeni yameongezeka kwa asilimia 19.3 ndani ya miaka mitano.
Mauzo hayo yalipaa kutoka Dola za Marekani 7.2 bilioni waka 2021 hadi Dola za Marekani bilioni 8.9 mwaka 2025,
BoT inabainisha kuwa ongezeko hilo imechangiwa na kuongezeka kwa shughuli za utalii nchi, biashara za kimataifa baina ya Tanzania na mataifa ya nje pamoja na sera nzuri za Serikali zinazovutia wawekezaji nchini.
Ni kicheko, maumivu
Mchambuzi wa masuala ya uchumi Paul Chengula, anasema kuongezeka kwa vituo hivyo ni fursa kwa wafanyabiashara na makampuni yanayojihusisisha na biashara hiyo.
“Wafanyabiashara wa kubadili fedha wananufaika zaidi kwa sababu inawapa fursa ya kuuza zaidi, lakini pia inawapa ajira vijana ambao wanafanya kazi katika maduka na makampuni hayo” amesema Chengula.
Chengula ameongezea kuwa, biashara ya fedha za kigeni imechochea kukua na kuongezeka kwa fursa mbalimbali za kiuchumi na kupungua ka njia za mkato zinazosababishia hasara Serikali.
“Uwepo wa hii biashara umeongeza wingi wa fedha za kigeni, jambo linalowezesha wafanyabiashara, watalii na wawekezaji kupata sarafu za kigeni kwa urahisi, lakini hata mtiririko wa fedha unakua ni wa uwazi hali inayochochea kuondoa, njia za mkato kama utakatishaji fedha” amesema Chengula.
Hata hivyo, Chengula amesema ongezeko la vituo hivyo linaweza kuwa changamoto kwa mabenki yaliyokuwa yakitawala biashara hiyo kwa sababu idadi ya wateja waliokuwa ikiwahudumia itapungua.
“Wanaoathirika zaidi ni mabenki, ambayo awali yalikua yameitawala biashara hii kwa kiasi kikubwa, sasa inawabidi wafanye njia nyingine kuhakikisha bado wanaendelea kuliteka soko” ameongeza Chengula.

Dar es Salaam kinara
Dar es Salaam imeendelea kuwa kitovu na mhimili mkubwa wa huduma za kubadilisha fedha za kigeni nchini Tanzania, ikiwa na nusu ya matawi yote ya kubadilishia fedha za kigeni nchini, ukiwa na takribani matawi 91 kati ya 182 yaliyopo nchini.
Hii ni sawa na kusema vituo vitano kati ya 10 vya kubadilishia fedha za kigeni vipo katika jiji la Dar es Salaam ambalo ni kitovu cha uchumi wa nchi na mataifa jirani.
Mbali na Dar es Salaam, Visiwa vya Zanzibar vimeshika nafasi ya pili ikiwa na matawi 33 ikifuatiwa na Arusha yenye matawi 31, Kilimanjaro matawi 10 na mikoa mingine iliyosalia ikiwa na jumla ya matawi 17.
Watalii waongezeka Tanzania, mapato yavunja rekodi mwaka 2025

- Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 6.7
Dar es Salaam.Tanzania imeendelea kuvutia wageni kutoka nchi mbalimbali duniani, huku sekta ya utalii ikirekodi mafanikio makubwa mwaka 2025.
Kwa mujibu wa ripoti ya Utafiti wa Watalii wa Kimataifa Wanaoondoka Nchini, iliyotolewa na Benki kuu ya Tanzania (BoT) na Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Idadi ya watalii wa kimataifa imeongezeka kwa asilimia 6.7.
Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka 2025 jumla ya watalii milioni 2.29 waliitembelea Tanzania kutoka milioni 2.14 iliyorekodiwa mwaka 2024.
Watalii hao waliingizia Tanzania Dola za Marekani bilioni 4.41 sawa na Sh11.6 trilioni ndani ya mwaka mmoja.
Ripoti ya NBS na BoT inabainisha kuwa wageni wengi wakitembelea nchini kwaajili ya mapumziko na likizo, wakivutiwa na uzuri wa tanzania na maeneo ya kujiachia yakiwa kama Serengeti, Ngorongoro, Tarangire, Mji mkongwe wa Zanzibari na fukwe za Bahari ya Hindi.
Fursa, watumiaji wa intaneti Tanzania wakifikia milioni 58.1
- Hadi kufikia robo ya mwaka inayoishia Desemba 2025, watumiaji wa intaneti walikuwa milion 58.1 kutoka milioni 56.3 iliyorekodiwa Septemba 2025.
- Intaneti hiyo hutumiwa zaidi na simu za janja.
- Hiyo inaongeza idadi ya Watanzania wanaonufaika na fursa za mtandaoni.
Dar es Salaam. Idadi ya Watanzania wanaotumia huduma za intaneti imeendelea kuongezeka kwa kasi na kufikia milioni 58.1 suala linalotajwa kuendelea kufungua fursa zaidi za kiuchumi.
Takwimu za mawasiliano za robo ya nne ya mwaka 2025 zilizotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) zinaonesha matumizi ya huduma z aintaneti yameongezeka kwa asilimia 3.2.
Takwimu hizo zinaonyesha kuwa hadi kufikia Desemba 2025 watumiaji wa intaneti walifikia milioni 58.1 kutoka watumiaji 56.3 waliokuwepo Septemba 2025.
Idadi hiyo ni sawa na ongezeko la watumiaji milioni 1.8 ndani ya kipindi cha miezi mitatu kuanzia Septemba hadi Disemba mwaka jana.
Kwa mujibu wa TCRA, idadi hiyo inajumuisha laini zote zilizotumia huduma ya intaneti angalau mara moja katika kipindi cha miezi mitatu iliyopita, bila kujali teknolojia iliyotumika kupitia njia mbalimbali, zikiwemo laini za simu za mkononi, nyaya za faiba (fiber), pamoja na teknolojia za mawimbi (wireless).
Uchambuzi wa takwimu hizo uliofanywa na Nukta Habari kwa miaka 10 mfululizo umebaini ongezeko la watumiaji wa intaneti nchini Tanzania mwaka hadi mwaka.
Huenda ukuaji huo umechangiwa kwa kiasi kikubwa na kuendelea kuimarika kwa miundombinu ya mawasiliano nchini, ikiwemo ongezeko la minara ya simu iliyofikia 10,029 kufikia mwisho wa mwaka 2024.
Aidha, intaneti inayotumia mtandao wa simu za mkononi (mobile wireless internet) imeendelea kuwa njia kuu ya upatikanaji wa huduma hiyo, ikichangia asilimia 99 ya usajili wote wa intaneti nchini.
Mbali na ongezeko la matumizi ya intaneti, matumizi ya simu janja (smartphones) pia yameongezeka, ambapo kiwango cha upenyo wake kimefikia asilimia 41.82.
Hata hivyo, simu za kawaida (feature phones) bado zinaendelea kutumika kwa kiwango kikubwa zaidi zikiwa na asilimia 87.11 ya matumizi.
Ni fursa iliyojificha
Wachambuzi wa uchumi wanaeleza kuwa ongezeko hilo la matumizi ya intaneti linafungua fursa mpya katika biashara, elimu, huduma za kifedha na ajira za kidijitali, huku likichochea ukuaji wa uchumi wa kidijitali nchini.
Akizungumza kuhusu mwenendo huo, Profesa Abel Kinyondo wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) amesema kuwa ongezeko la usajili wa laini zinazotumia intaneti halimaanishi moja kwa moja kuwa idadi hiyo ni sawa na watumiaji halisi, kwa kuwa mtu mmoja anaweza kuwa na laini zaidi ya moja.
Amefafanua kuwa pamoja na changamoto zilizopo, intaneti imeleta mapinduzi makubwa katika shughuli za kiuchumi kwa kurahisisha biashara, masoko na huduma za kifedha.
“Leo mtu anaweza kufanya biashara akiwa sehemu yoyote nchini bila kulazimika kusafiri. Intaneti imeongeza urahisi wa kufanya miamala, kutangaza bidhaa na kupata taarifa mbalimbali kwa haraka,” amesema Profesa Kinyondo.
Hata hivyo, ameonya kuwa matumizi ya intaneti yanaambatana na changamoto mbalimbali zikiwemo uhalifu wa mtandaoni, udanganyifu katika biashara za mtandaoni na matumizi mabaya ya mitandao ya kijamii.
Pia amewataka vijana kutumia intaneti kwa manufaa, ikiwemo kujifunza ujuzi mpya, kufanya biashara na kutafuta maarifa, huku wakizingatia tahadhari dhidi ya matumizi yanayoweza kuhatarisha usalama wao binafsi na maadili ya jamii.
Bei ya maharage yaendelea kuwa kichomi Dar es Salaam

Dar es Salaam. Bei ya maharage imeendelea kuwa tulivu nchini kutokana na kutobadilika ndani ya wiki licha ya kuendelea kwa msimu wa mvua za masika katika maeneo mbalimbali nchini.
Kwa kawaida msimu wa mvua za masika na kipindi cha mfungo wa Ramadhan na Kwaresma kama hiki, bei za bidhaa za vyakula hupaa kutokana na kuongezeka kwa mahitaji na kupaa kwa gharama za uchukuzi kwa sababu ya athari ya mvua kwenye miundombinu.
Uchambuzi wa bei za jumla za mazao uliofanywa na Nukta Habari umebainisha kuwa kuwa bei hizo zimeendelea kuwa thabiti katika mikoa mbalimbali, huku tofauti kubwa ikionekana kati ya bei ya juu na ya chini.
Kwa mujibu wa takwimu za mazao makuu ya biashara zilizotolewa leo Machi 4, 2026, na Wizara ya Viwanda na Biashara, bei ya jumla ya gunia la kilo 100 la maharage imeendelea kuwa Sh400,000 katika soko la Mwananyamala, jijini Dar es Salaam sawa na bei iliyorekodiwa mapema wiki hii.
Kubaki juu kwa zao hilo kwa chakula kutaendelea kuwa mzigo kwa mlaji wa mwisho, huku wafanyabiashara wakinufaika na viwango hivyo vya juu.
Hata wakati Dar es Salaam wakinunua zao hilo kwa bei ya juu, Njombe wao ndo wananunua maharage kwa bei ya jumla ya chini zaidi nchini ambapo gunia la kilo 100 linauzwa kwa Sh110,000. Bei hiyo ya Njombe ni ya chini takriban mara 4 ya ile ya Dar es Salaam na imeendelea kubaki kama ilivyokuwa mwanzoni mwa wiki.
Aidha, bei hizo hazijaonyesha mabadiliko katika mkoa wa Kigoma, ambapo zinaendelea kutumika kama zilivyokuwa Jumatatu.
Tanga waendelea kutoboa mifuko bei ya mahindi

Kununua gunia la mahindi la kilo 100 mkoani Tanga itakulazimu kulipia Sh140,000 ambayo ni mara 2 na nusu ya bei ya chini iliyorekodiwa mkoani Njombe ya Sh55,600 kwa gunia la kilo 100.
Wakati wakazi wa mkoa huo wakilia na bei hiyo, hali ni tofauti kwa wakazi wa mkoani wa Dar es Salaam ambao wananunua gunia la kilo 100 za viazi mbatata/ mviringo kwa Sh60,000 ambayo ni ahueni kwa mara 3 zaidi ya ile iliyorekodiwa mkoani Tanga ya Sh180,000.
Ufaulu kidato cha nne unavyopanda na kushuka Tanzania
- Takwimu zinaonesha ufaulu unashuka na kuongezeka mwaka hadi mwaka katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) limetangaza matokeo ya mitihani ya kidato cha nne iliyofanyika Novemba, 2025, ambapo ufaulu umeongezeka kidogo kulinganisha na miaka iliyopita.
Katibu Mtendaji wa Baraza hilo, Dk. Said Mohamed aliyekuwa akitangaza matokeo hayo jijini Dar es Salaam leo Januari 31, 2026 amesema kuwa ufaulu wa wanafunzi kwa kidato cha nne kwa mwaka 2025 ni asilimia 92.37.
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari unaonyesha kuwa ufaulu wa kidato cha nne umekuwa ukipanda na kushuka kwa miaka tofauti katika kipindi cha miaka mitano kuanzia mwaka 2021.
Takwimu zinaonyesha kiwango cha ufaulu kiliongezeka kwa asilimia 0.67 na kufikia asilimia 87.79 mwaka 2022 kutoka asilimia 87.30 iliyorekodiwa mwaka 2021. Hata hivyo, ufaulu huo ulishuka kwa asilimia 0.32 na kufikia asilimia 87.65 mwaka 2023.
Ongezeko thabiti la matokeo ya kidato cha nne limeonekana kuanzia mwaka 2024 ambapo ufaulu uliongezeka kwa takriban asilimia 4.72 na kufikia asilimia 92.37.
Aidha, katika kipindi cha miaka mitano wavulana ndio wanaongoza kwa kuwa na ufaulu wa juu zaidi ya wasichana wakiwa na wastani wa ufaulu wa asilimia 92.75 wakiwaacha mbali wasichana wenye wastani wa asilimia 90.71.







