Si kweli: Maji yaliyo gandishwa yanua vijidudu vya kipindupindu

Mariam John 0845Hrs   Januari 17, 2024 NuktaFakti
  • Wataalamu wa afya wasema vijidudu vya kipindupindu huzaliana zaidi vikiwa kwenye maji ya baridi au yaliyoganda.
  • Wananchi watakiwa kuchukua tahadhari.

Mwanza. Ikiwa wewe ni miongoni mwa watu waliodhani kuwa kugandisha maji ya kunywa kunaua vijidudu vinavyosababisha ugonjwa wa kipindupindu, jambo hilo si kweli.

Vijidudu vinavyosambaza kipindupindu vinavyofahamika kwa jina kitaalamu la ‘ Vibrio cholerae’ haviwezi kufa katika maji baridi au yaliyoganda bali huzaliana zaidi.

Renald Mlyakado Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma mkoani Mwanza, aliyekuwa akitoa elimu kwa waandishi wa habari kuhusu ugonjwa wa kipindupindu Januari 16, 2024, ameitaka jamii kuondoa dhana hiyo potofu. 

“Kwahiyo tusidanganyike kuwa kuweka maji kwenye friji kunaua wadudu hao hapana, tunachoshauri ni mtu kuchemsha maji na kuyahifadhi vizuri kabla ya kuyatumia,” amesema Mlyakado.

Kwa mujibu wa Afisa huyo, dalili za mtu mwenye ugonjwa huo huanza kuonekana ndani ya masaa 24 hadi siku tano toka vijidudu hivyo viingie mwilini kupitia  kunywa maji yasiyochemshwa, kugusana na mgonjwa au kula chakula, matunda na mboga mboga zisizoandaliwa katika mazingira ya usafi.

Naye Emmanuel Mnkeni, mtaalamu wa afya kutoka Wizara ya Afya Dodoma amewataka wananchi kuhakikisha wanasafisha mazingira yao vizuri huku akiziomba Mamlaka ya Maji Safi na Usafi wa Mazingira mkoani Mwanza (Mwauwasa) kuangalia mifumo yao ya maji ili kusaidia kudhibiti tatizo hilo.


Zinazohusiana:Wanaoumwa kipindupindu Mwanza wafikia 80


Fanya haya kujikinga na kipindupindu

Ili kujikinga na ugonjwa wa kipindupindu Mlyakado ameshauri wananchi kutumia chakula cha moto na kunawa maji ya moto na sabuni kila wanapotoka chooni njia ambayo itasaidia kuua vijidudu vinavyosababisha ugonjwa huo.

"Vijidudu vya ugonjwa wa kipindupindu vinatoka kwenye kinyesi kibichi na vinasambazwa na mtu mwenye ugonjwa huo, hivyo ili kuepuka tunashauri kila mtu kuzingatia usafi suala ambalo linaenda sambamba na kula chakula kikiwa cha Moto.

Pamoja na njia hizo Shirika la  Afya Duniani (WHO) linashauri utolewaji wa matibabu ya haraka kwa mgonjwa aliyeambukizwa kipindupindu ili kuokoa maisha yake pamoja na wanaomzunguka.

Related Post