HESLB kutoa majina waliopata mikopo awamu ya kwanza Oktoba 17

Mwandishi Wetu 0256Hrs   Oktoba 17, 2019 Habari
  • Itatangaza majina hayo ya waliopata mikopo awamu ya kwanza leo saa saba mchana.
  • Imesema mfumo wake wa kielektroniki utaendelea kuwa wazi, kwa waombaji kuendelea kuomba wakiwa vyuoni.

Dar es Salaam. Wakati mioyo ya baadhi ya waombaji wa mikopo ya elimu ya juu kutoka Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) ikiwa juu kusubiri hatma yao, bodi hiyo inatarajia kutoa orodha ya awamu ya kwanza ya majina ya waliofanikiwa kupata mkopo kwa mwaka wa masomo 2019/2020, leo saa 7:00 mchana.

Hatua hiyo, imekuja baada ya Heslb kuaihirisha mara mbili kutangaza majina hayo. 

Awali, majina hayo yalitakiwa kutolewa Oktoba 6, 2019 lakini bodi haikutoa ili kuwapa fursa waombaji ambao fomu zao zilikuwa na mapungufu kurekebisha kasoro zao. 

Wakati huo, tarehe rasmi ya kuwatangaza waliochomoza kwenye orodha ya wanufaika wa mkopo huo wa elimu ya juu, ilisogezwa tena mbele hadi Oktoba 15 lakini hata ilivyofika siku hiyo hayakutangazwa tena. 

“Tutatangaza orodha ya awamu ya kwanza waliopata mkopo Alhamis (Oktoba 17),” inasomeka sehemu ya taarifa ya Heslb iliyotolewa Oktoba 15, 2019. 


Zinazohusiana


Heslb imesema imepokea jumla ya maombi 87,747 ambapo kati ya maombi hayo, ni maombi 82,043 sawa na asilimia 93.4 yalikuwa yamekidhi vigezo vya maombi. 

Hata hivyo, imesema baada ya kutoa orodha ya kwanza ya majina ya waliopata mikopo, haitafunga mfumo wake wa kielektroniki ili kutoa fursa kwa waombaji ambao hajakamilisha maombi wakamilishe wakifika vyuoni.

Bodi hiyo imesema katika awamu ya kwanza wanatarajia kuwatunuku mikopo hiyo wanafunzi takriban 55,000 watakaonza elimu ya juu katika mwaka wa masomo wa 2019/20 unaonza mwishoni mwa mwezi huu katika sehemu kubwa ya vyuo nchini.

Mikopo hiyo husaidia wanafunzi kuweza kumudu gharama za masomo na maisha wakati akisaka elimu hiyo ya juu. 

Wangapi watatoboa kwenye orodha ya awamu ya kwanza ya Heslb? Usikose kufuatilia habari za Heslb katika tovuti ya www.nukta.co.tz na mitandao.

Related Post