Akaunti feki ya Twitter ilivyotumika kupotosha madhara ya kujifukiza

Daniel Mwingira 0954Hrs   Mei 05, 2020 NuktaFakti
  • Iliweka ujumbe na picha ya mtu aliyeungua mgongo ikidai ni madhara ya watu kujifukiza.
  • Tumebaini kuwa picha hiyo ilipigwa Kenya na Siyo Tanzania katika tukio la mwanaume mmoja kumwagiwa maji moto.
  • Tunathibitisha kuwa picha hiyo ni uzushi na inalenga kupotosha kuhusu madhara ya kujifukiza.

Dar es Salaam. Mwishoni mwa mwezi Aprili, 2020 zilizagaa taarifa kwenye mitandao ya kijamii zinazoelezea kuhusu faida na madhara ya kujifukuzia ili kujikinga na ugonjwa wa Corona (COVID-19).

Taarifa hizo zilizagaa baada ya Rais John Magufuli kuwataka wataalam wa Wizara ya Afya kuwaelekeza wananchi namna ya kutumia baadhi ya dawa za asili ambazo wanaweza kujifukiza ili kujikinga na COVID-19.

Hata hivyo, baadhi ya watu wenye nia ovu walitumia agizo hilo kusambaza taarifa za uzushi kuhusu kujifukiza au maarufu kama kupiga “nyungu”.

Moja ya taarifa ya uzushi iliyowekwa Twitter na baadaye kuchukuliwa kama picha na kusambazwa mtandaomi ikiwemo WhatsApp ilikuwa na maelezo ya kitabibu huku ikiambatana na picha inayoonyesha  mtu aliyeungua kuanzia mkono wa kulia hadi mgongoni ikidai ni matokeo ya kujifukuza.

Ujumbe uliombatana na picha hiyo unasomeka “Jamani tusikikizeni sisi wataalamu wa afya, tunaumia sana kuona haya unajifukuza then unapata burn injury (majereha ya kuungua) ya namna hii, na omba Mungu usipate inhalation burn injury ya airway  upate laryangeal edema kama utafika hata hospitali’’

Picha ambayo imekuwa ikisambazwa kwenye mitandao ya kijamii kuwa ni madhara ya kujifukiza lakini imebainika kuwa siyo kweli. Picha|Mtandao.

Ujumbe na picha hiyo iliyokuwa ikisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii hasa WhatApp ulikuwa ikionyesha madhara ya kujifukiza.

Hata hivyo, hiyo picha inaacha maswali mengi ya ukweli kuhusu madhara yatokanayo na kujifukiza? Ni kweli majeraha ya kuungua ya mwanaume aliyepo kwenye picha yametokana na kujifukiza?



Huu ndiyo ukweli wa ujumbe huo

Utafiti uliofanywa na timu ya Nukta Fakti umebaini mambo mbalimbali ambayo yanaweza kuthibitisha bila shaka kuwa ujumbe na picha hiyo ni uzushi na zinalenga kupotosha watu.

Nukta Fakti imegundua kuwa akaunti ya Twitter ya 
@doktamathew iliyotumika kuweka ujumbe huo haipo na haipatikani katika mtandao huo.

Hata hivyo, tumebaini kuwa jina la akaunti hiyo ya Twitter pia inatumika Instagram ikiwa na jina kama hilo la doktamathew 
.

Mmiliki wa akaunti hiyo ya Instagram aliyejitambulisha kwa jina Dk Gaudence Mathew ameiambia NuktaFakti kuwa hana mahusiano na akaunti hiyo ya Twitter na wala hana akaunti katika mtandao huo. 

Picha inayo onyesha kuwa akaunti ya Twitter ya @doktamathew haipo mtandanaoini.Picha | Mtandao.

Kwa mantiki hiyo akaunti hiyo yenye jina la @doktamathew ni famba au uzushi.

Kama akaunti ni famba je kuna ukweli wowote wa kitabibu katika maneno yaliyoandikwa?

Dk Mathew anayehudumu katika hospitali ya Decca Poliyclic iliyopo jijini Dodoma, licha ya kuwa siyo mmiliki wa akaunti hiyo ya Twitter iliyotumika kupotosha umma, ameeleza kuwa ujumbe uliochapishwa kwenye akaunti una mantiki ya kitabibu lakini akatoa angalizo kuwa watu waendelee kufuatilia  maelekezo yote na elimu inayotolewa na wataalam wa Wizara ya Afya na si vinginevyo.


Zinazohusiana.



Picha nayo utata mtupu

Utafiti wa awali uliofanywa na NuktaFakti imegundua picha iliyoambatanishwa kwenye akaunti hiyo feki ya Twitter ni tukio la kweli lakini madhara katika picha hiyo hayajatokana na kujifukuza kama ilivyoelezwa.

Kwa kutumia zana za uthibitishaji picha za Google, tumebaini kuwa picha hiyo ilichapishwa kwa mara ya kwanza nchini Kenya na siyo Tanzania kama inayoelezwa na haina uhusiano wowote na madhara ya kujifukiza.

Mtu huyo anayeonekana ameungua ni tukio linalodaiwa kuwa lilisababishwa na kuunguzwa  na mke wake na maji ya moto kutokana na tuhuma za kutokuwa mwaminifu kwenye ndoa yake.

Picha hiyo ya mwanaume aliyeungua inapatikana katika ya ukurasa wa Facebook wa ZED Headlines. 

Kwa vigezo hivyo, picha hiyo inayosambazwa katika mitandao ya kijamii siyo ya kweli bali ni uzushi na inalenga kupotosha watu.

Endelea kujikinga na uwakinge wengine dhidi ya virusi vya ugonjwa wa corona kwa kunawa mikono mara kwa mara kwa sabuni na maji tiririka, kuvaa barakoa, na kujizuia na safari na mikusanyiko isiyokuwa ya lazima. Sambaza habari au taarifa sahihi. 

Related Post