Tanzania kuunga mkono upatikanaji amani Somalia

Lucy Samson 0942Hrs   Aprili 27, 2024 Habari
  • Tanzania itatoa mafunzo katika masuala ya ulinzi na usalama wa raia.
  • Itasaidia kuondoa zuio la upatikanaji wa silaha. 

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Tanzania itaunga mkono juhudi za upatikanaji amani wa Shirikisho la Jamhuri ya Somalia kwa kutoa mafunzo ya ulinzi na kuondoa zuio la ununuzi wa silaha.

Shirikisho la Jamhuri ya Somalia lililojiunga na Nchi Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) hivi karibuni ni miongoni mwa nchi zinazokumbwa na machafuko ya kisiasa mara kwa mara barani Afrika hali inayohatarisha usalama wa raia na mali zao.

Rais Samia aliyekuwa akizungumza na wanahabari baada ya kumpokea Dk Hassan Sheikh Mohamud Ikulu jijini Dar es Salaam leo Aprili 27, 2024 amesema Tanzania itaunga mkono jitihada za upatikanaji amani katika nchi hiyo. 

Ili kutekeleza adhma hiyo Rais Samia amesema Tanzania itakuwa tayari  kutoa mafunzo kwenye nyanja mbalimbali ikiwemo masuala ya ulinzi na usalama wa raia pamoja na kuondoa zuio la ununuzi wa silaha.

“Tumewahakikishia kwamba tutaendelea kusisitiza umuhimu wa kuondoa zuio la kununua silaha lilowekwa kwao na itakuwa hatua ya kuviwezesha vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali kutimiza wajibu wao na kujilinda wenyewe…

…Kama mnavyojua hali ya wenzetu haiko vizuri sana kwa hiyo tumewahakikishia kuwaunga mkono kwenye kujenga uwezo wa wao kama nchi kujilinda wenyewe,” amesema Rais Samia.


Soma zaidi:Rais Samia:Tuna kila sababu ya kujivunia Muungano wetu


Tanzania na Somalia pia zinatarajia kuimarisha uhusiano katika masuala ya kijamii, afya na uchumi ambapo mawaziri husika watakutana na kujadili ni maeneo ya kimkakati ya kuanza nayo. 

Kwa upande wake Rais wa Shirikisho la Somalia Dk Mohamud amesema ushirikiano baina ya nchi yake na Tanzania utazaa matunda baina ya nchi hizo mbili pamoja na kuzipa uwezo wa kutatua changamoto zinazowakabili.

“Usaidizi ambao Tanzania utaendelea kupeleka kule Somalia utatufaidisha na kuwa wa manufaa katika sekta ya ulinzi na usalama, uwekezaji na hata kwenye uhusiano wa mambo ya kikanda na kitaifa…

..Tunapenda kuishukuru Serikali yako na Watanzania kwa namna ambavyo wamesimama nasi katika ulinzi wa mipaka yetu hata katika wakati ambao tulikuwa na changamoto na majirani zetu kuhusu masuala ya mipaka,” amesema Rais Dk Mohamud. 

Hi ni mara ya kwanza wa  Rais wa Somalia kufanya ziara Tanzania tangu nchi hiyo ikubaliwe kujiunga na EAC Julai 2023.

Related Post