BoT yapandisha riba ya benki kuu hadi asilimia 6

Mwandishi Wetu 0326Hrs   Aprili 04, 2024 Biashara
  • Kimepanda kutoka kiwango cha asilimia 5.5 iliyotangazwa Januari 2024 kwa robo ya kwanza ya mwaka.
  • Lengo ni kukabiliana na mfumuko wa bei unaoweza kutokea kutokana na athari za uchumi wa dunia.

Dar es Salaam. Kamati ya Sera ya Fedha imeongeza kiwango cha riba ya benki kuu (Central Bank Rate) hadi asilimia 6 kitakachotumika katika robo ya pili ya mwaka 2024 kutoka asilimia 5.5 iliyotangazwa Januari ili kukabiliana na mfumuko wa bei unaoweza kutokea kutokana na athari za uchumi wa dunia. 

Riba ya benki kuu ni kiwango cha riba kinachotumika na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) kufanya biashara na benki za biashara nchini.

Gavana wa BoT Emmanuel Tutuba ameeleza katika mkutano na mabosi wa mabenki na wanahabari jijini Dar es Salaam kuwa kiwango hicho kipya kitatumika kuanzia Aprili hadi Juni 2024.

"Kamati imeona umuhimu wa kuongeza Riba ya Benki Kuu hadi asilimia 6, itakayokuwa na wigo wa asilimia 2 juu na chini, ili kukabiliana na ongezeko la mfumuko wa bei siku zijazo kutokana na athari za mwenendo wa uchumi wa dunia," amesema Tutuba. 

Hata hivyo, bosi huyo wa BoT amesema kuwa viashiria vya kiuchumi vya ndani vinatarajiwa kuendelea kuwa imara katika kipindi kilichosalia cha mwaka.

"Kuhusu mwenendo wa uchumi wa Tanzania, Kamati imeridhishwa na kuendelea kuimarika kwa uchumi, licha ya changamoto zilizotokana na mtikisiko katika uchumi wa dunia. Hali hii ya kuimarika kwa uchumi inatarajiwa kuendelea katika siku zijazo, hususan robo ya pili ya mwaka 2024," amesema. 

BoT inaeleza kuwa ukuaji wa uchumi wa Tanzania unakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 5.1 kwa mwaka 2023, kutoka asilimia 4.7 mwaka 2022.


Soma zaidi: BOT kununua dhahabu kwa wafanyabiashara, wachimbaji wa ndani


Katika robo ya pili ya mwaka 2024, kasi ya ukuaji wa uchumi inakadiriwa kuongezeka kufikia asilimia 5.1 katika robo ya kwanza ya mwaka 2024. 

Mwenendo huu, Tutuba amesema unatokana na uwekezaji unaofanywa na Serikali hususan katika ujenzi wa miundombinu unaolenga kuongeza uwekezaji kwa sekta binafsi. 

"Sekta binafsi imeendelea kuchangia katika kuimarika kwa uchumi kutokana na maboresho yanayoendelea katika kuimarisha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini. Hali hii inadhihirika kutokana na kuendelea kuongezeka kwa mikopo kwa sekta binafsi na uwekezaji kutoka nje ya nchi," amesema.

Kwa mujibu wa tathmini ya kamati hiyo, mfumuko wa bei umeendelea kuwa tulivu, kwa wastani wa asilimia 3.0 kwa robo ya kwanza ya mwaka 2024. 

Kiwango hicho, Tutuba amesema kilikuwa ndani ya lengo la nchi la mfumuko wa bei usiozidi asilimia 5 na vigezo vya kikanda kwa jumuiya ambazo Tanzania ni mwanachama. 

Hali hiyo ya mfumuko wa bei, amesema inatokana na utekelezaji wa sera madhubuti ya fedha na uwepo wa chakula cha kutosha nchini.

Related Post