Saa janja kutumika utambuzi, ufuatiliaji wa Uviko-19

Davis Matambo 0334Hrs   Oktoba 06, 2022 NuktaFakti
  • Watafiti wakuna vichwa kurahisisha ufuatiliaji wa ugonjwa huo kwa mtu binafsi.
  • Waanza kufanya majaribio ya saa janja kupima dalili za Uviko-19. 

Dar es Salaam. Tangu kuanza kwa janga la Uviko-19 tafiti mbalimbali zimekuwa zikifanyika kuongeza matumizi ya teknolojia kuwakinga watu na ugonjwa huo.

Kwa sasa, saa janja zinaweza tumika kutambua na kufuatilia dalili za ugonjwa huo.

Utafiti huo umefanywa na kampuni ya kielektroniki ya Fitbit iliyochambua viwango vya upumuaji vya usiku kwa maelfu ya watumiaji wa vifaa vyao ili kuelewa ikiwa hatua hii inaweza kusaidia utambuzi wa Uviko-19.

Waligundua kuwa ndani ya kipindi cha siku saba (kutoka siku moja kabla ya dalili kuanza, au siku moja kabla ya kipimo chanya kwa washiriki bila dalili), sehemu ya watu walio na Uviko-19 walionyesha kiwango cha juu cha upumuaji kinachohusiana na maambukizi ya Uviko-19.

Japokuwa utafiti huu umefanyika kwa watu wachache, wagonjwa na wasio na maambukizi, unaweza kuwa ni njia mpya ya kugundua uwezekano wa maambukizi ya Uviko-19 na kufanya majaribio kwa haraka zaidi.

Hata hivyo, utafiti huo bado haujathibitishwa na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Utafiti wa awali wa Juni wa kampuni ya Whoop inayohusika na teknolojia ya kufuatilia mazoezi uliangazia uwezo wa vifaa vyao kuchanganua mabadiliko katika kiwango cha kupumua ili kutabiri hatari ya maambukizi ya Uviko-19.

Data kuhusu kasi ya upumuaji na viashirio vingine vya utendaji kazi wa moyo kutoka kwenye kundi la watu walio na Uviko-19 zilitumiwa kutoa mafunzo kwa kanuni (algorithm) za kutabiri maambukizi.

Kulingana na kiwango cha upumuaji wakati wa kulala, teknolojia hiyo iliweza kutambua asilimia 20 ya watu walioambukizwa Uviko-19 ndani ya siku mbili kabla ya dalili kuanza, na asilimia 80 ya kesi kufikia siku ya tatu ya dalili.


Soma pia:


Matumizi mengine ya vifaa vya teknolojia yanahusisha kifaa cha Ava ambacho kwa sasa kinatumika hasa kwa ufuatiliaji wa uzazi, na kutambua virusi wakati wa awamu za awali kabla ya dalili kwa kuchunguza mabadiliko ya kimwili.

Kifaa hicho hupima mawimbi ikijumuisha kasi ya kupumua, mapigo ya moyo, halijoto ya ngozi na msukumo wa damu, pamoja na kiwango cha usingizi. Data kutokana na wagonjwa walioambukizwa Uviko-19 ilitumika vile vile kufahamisha kanuni ya ung’amuzi (algorithm) kwa mashine.

Uchunguzi kupitia kifaa hicho kinachoweza kuvaliwa mkononi ulibaini asilimia 68 ya kesi chanya siku mbili kabla ya dalili za maambukizi kuwa dhahiri.

Vifaa vyote hivi hutumia akili bandia kuchanganua kwa kina kiasi kikubwa cha data kwenye uwezo wake wa kugundua maambukizi ya Uviko-19 kwa kuangazia mabadiliko ya mwili.

Hata hivyo, matumizi ya akili bandia katika ulimwengu halisi unaweza kukumbwa na changamoto kutokana na tofauti kati ya tabia za wagonjwa na mifumo ya mawimbi ya kibaiolojia.

Licha ya kuwa vifaa hivyo havijathibitishwa na WHO kupima maambukizi lakini vitumikapo kwa kuvaliwa sambamba na teknolojia nyingine za kidijitali hutoa tahadhari ili kusaidia kuzuia Uviko-19 na magonjwa mengine ya kuambukiza.

Related Post