Serikali kufumua sera za uwekezaji, viwanda Tanzania

Mwandishi Wetu 0700Hrs   Aprili 04, 2024 Biashara
  • Hatua hiyo itasaidia kuendana na mahitaji ya sasa na kuvutia wawekezaji.
  • Pia itaongeza miradi ya uwekezaji na ajira kwa wananchi.


Dar es salaam. Naibu Waziri Wizara ya Viwanda na Biashara Exaud Kigahe amesema kuwa Serikali imeanza kufanya mapitio ya sera, mikakati na sheria za kisekta zikiwemo za uwekezaji na viwanda ili ziweze kuendana na mahitaji na kuvutia wawekezaji nchini.

Kigahe ametoa kauli hiyo leo Aprili 4,2024 Bungeni jijini Dodoma alipokuwa akijibu maswali ya Mhandisi Mwanaisha Ulenge aliyetaka kujua ni lini Serikali itafanya maboresho ya sera na sheria za uwekezaji na viwanda nchini. 

“Sheria za kodi na sheria za uwekezaji hazisomani, kuna miradi mingi inafunguliwa lakini wawekezaji hawafanyi hivyo kwa sababu hakuna vivutio. Je, ni lini Serikali italeta hapa sheria hizo ili ziweze kupitiwa upya na ziweze kusomana?,” amehoji Ulenge.

Kigahe akijibu swali hilo amesema Serikali imeshaanza kupitia sera na sheria mbalimbali za taasisi na kuboresha sera ya uwekezaji ya viwanda na biashara.

“Ni kweli bado kuna changamoto kwenye baadhi ya sheria na sera za uwekezaji, mheshimiwa Naibu Spika, Serikali imeanza kupitia sera na sheria mbalimbali za taasisi zetu na za kodi lakini pia tumeanza kuhuisha na kuboresha sera mbalimbali,” amesema Kigahe.

Baadhi ya sera na sheria hizo ni Sera ya Taifa ya Uhamasishaji Uwekezaji ya mwaka 1996, Sera ya Maendeleo Endelevu ya Viwanda (SIDP, 1996-2020), Sera ya Maendeleo ya Viwanda Vidogo na Biashara Ndogo ya mwaka 2003).

Kigahe amesema pia Serikali inaendelea na mikakati ya kuendelea kuvutia wawekezaji wapya, kujenga viwanda vipya na kufufua vya zamani na kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji nchini.

“Serikali inaendelea na mikakati mbalimbali ya kufufua viwanda vilivyokufa ikiwemo Mkoa wa Tanga kwa kutoa ushauri wa kitaalam kwa wamiliki wa viwanda vilivyo binafsishwa wenye nia ya kuviendeleza, kuvirejesha Serikalini na kuvitangaza upya kwa njia ya zabuni ya wazi,” amesema Kigahe.

Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka 2024/25 unaitaka Serikali kuendelea kuongezeka ushiriki wa Serikali za Mitaa, sekta binafsi na wadau wa maendeleo katika uendelezaji wa maeneo ya uwekezaji na miundombinu ili kuvutia uwekezaji.

Pia inasisitiza halmashauri kutenga maeneo kwa ajili ya uwekezaji mahususi.

Machi 11, 2024 Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji Kitila Mkumbo alisema miradi inayosajiliwa katika Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) imeongezeka kutoka miradi 293 iliyosajiliwa mwaka 2022 hadi kufikia miradi 526 iliyosajiliwa mwaka 2023.


(Habari hii imeandikwa na Sayuni Kisige na kuhaririwa na Daniel Samson)

Related Post