Rais Samia:Tuna kila sababu ya kujivunia Muungano wetu

Mwandishi Wetu 0819Hrs   Aprili 26, 2024 Habari
  • Asema Muungano ni chanzo cha maendeleo ya kiuchumi
  • Sherehe za Muungano zafaana, zafanyika kwa mara ya kwanza baada ya miaka 8 uwanja wa Uhuru.


Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema Watanzania  wana kila sababu ya kujivunia Muungano kati ya Tanganyika na Zanzibar kutokana na manufaa yaliyopatikana ikiwemo kukua kwa uchumi.

Maadhimisho ya Muungano kwa mwaka huu yamefanyika kwa mara ya kwanza katika uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam baada ya kusitishwa ama kuhamishwa katika mikoa mingine kwa miaka nane.

Mara ya mwisho maadhimisho hayo kufanyika katika uwanja wa Uhuru ilikuwa mwaka 2015 chini ya Rais wa awamu ya nne Dk. Jakaya Kikwete kabla ya kusitishwa kutokana na sababu mbalimbali mwaka 2016, 2019, 2020 na 2021 chini ya uongozi wa Hayati Dk. John Magufuli na Rais Samia Suluhu.

Miaka ya 2017, 2018 na 2022 maadhimisho hayo yalifanyika mkoani Dodoma na mwaka 2023 kufanyika katika ngazi ya mikoa kote nchini.


Akizungumza katika sherehe ya maadhimisho hayo Rais Samia amesema licha ya changamoto zilizopo Watanzania wanatakiwa kujivunia Muungano huo ambao umekuwa mfano wa kuigwa barani Afrika.

“Tuna kila sababu ya kijivunia muungano wetu..kupitia muungano tumejenga umoja na muungano wa kitaifa, tumeimarisha udugu na bila shaka tumepiga hatua kubwa ya za maendeleo kiuchumi, kisiasa na kijami pamoja na kudumisha mila na desturi zetu,” amesema Rais Samia.

Mbali na wito huo Rais Samia amewataka Watanzania kufanya kazi kwa bidii ili kukuza tija na na ustawi wa Taifa katika nyanja mbalimbali ikiwemo ya uchumi ambao umeendelea kuimarika hata kufikia uchumi wa kati wa chini.

“Tunafahari kuwa nchi yetu imefika hadhi ya uchumi wa kati ngazi ya chini na tathimini zote zinaonesha kuwa kuna mwelekeo mzuri wa kuimarika na kuweza kufikia uchumi wa kati ngazi ya juu hivyo tuendelee kudumisha amani ili tujenge uchumi na ustawi zaidi kwa wannanchi wetu,” ameongeza Rais Samia.


Soma zaidi:Vifo vinavyotokana na mafuriko vyafikia 155, kaya 51,000 zikiathirika


Awali Rais wa Zanzibar Dk. Husein Mwinyi aliwaahidi Watanzania kuendelea kuulinda Muungano kwa manufaa ya kizazi cha sasa na baadae.

“Kwa niaba ya wananchi wa Zanzibar tunawaahidi watanzania wenzetu tutaendelea kuwa waumini wa dhati wa muungano wetu tutahakikisha unadumu, unaendelea na unazidi unaimarika kwa faida ya kizazi cha sasa na wale wanaokuja baada yetu,” amesema Dk. Mwinyi.

Mbali na viongozi wa kitaifa maadhimisho ya Muungano kwa mwaka huu yamehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kimataifa kutoka ndani na nje ya bara la Afrika pamoja na wabia wa maendeleo.

Miongoni mwa waliohudhuria ni pamoja na Rais wa Burundi  Everist Ndayishimiye, Rais wa Zambia Hakainde Hichilema , Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo Felix Tshisekedi, Rais wa Kenya William Ruto na Rais wa Namibia Nangolo Mbumba.

Related Post