Vifo vinavyotokana na mafuriko vyafikia 155, kaya 51,000 zikiathirika

Mwandishi Wetu 1002Hrs   Aprili 25, 2024 Habari
  • Ni kutoka mikoa 19 nchini.
  • Waziri Majaliwa atoa maagizo kwa wananchi kukuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA pamoja na viongozi wao.

Dar es salaam. Mvua zinazoendelea kunyesha nchini Tanzania zimesababisha vifo ya watu 155, majeruhi 236 huku kaya zaidi ya 51,000 zikiathirika.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliyekuwa akitoa tathmini ya athari za mvua hizo  leo (Aprili 25, 2024) katika kipindi cha maswali na majibu Bungeni amewaambia wabunge kuwa mpaka sasa tayari mikoa 19 nchini imeathirika.

“Maeneo yaliyoathirika ni pamoja na Rufiji na Kibiti mkoani Pwani, Malinyi, Mlimba, Kilosa, Manispaa ya Morogoro na Ifakara (Morogoro), Ilala, Kinondoni, Ubungo, Kigamboni na Temeke (Dar es Salaam), Same, Hai na Moshi (Kilimanjaro), Mbarali, Kyela na Halmashauri ya Jiji la Mbeya (Mbeya), Manispaa ya Kigoma Ujiji na Kakonko (Kigoma), Iringa Vijijini (Iringa), Manispaa ya Tabora (Tabora)...

…Mengine ni Bahi (Dodoma), Lindi Manispaa, Kilwa, Liwale, na Nachingwea (Lindi), Masasi (Mtwara), na Jiji la Arusha, Monduli na Karatu (Arusha), Muleba, Manispaa ya Bukoba (Kagera), Manispaa ya Shinyanga (Shinyanga), Geita Mji, Nyangh'wale na Chato (Geita), Mbozi na Momba (Songwe), Nkasi, Sumbawanga na Kalambo (Rukwa), Hanang' (Manyara),”amesema Waziri Majaliwa.


Soma zaidi:Ripoti: Afya ya akili chanzo cha watu kujiua, kuua Tanzania


Mbali na athari hizo Waziri Majaliwa ameeleza kuwa watu 200,000 wameathirika huku nyumba zaidi ya 10,000 na miundombinu mingine ikiwemo barabara na madaraja ikiharibika.

Mapema mwezi April mwaka huu Jeshi la Polisi Tanzania liliwaataarifu Watanzania kuwa kati ya Aprili 1 hadi 7 watu 15 walipoteza maisha kutokana na mvua zinazoendelea kunyesha nchini. 

Vifo hivyo ni vile vilivyorekodiwa katika mikoa ya Rukwa, Lindi, Njombe, Tanga, Pwani, Manyara, Mbeya, na Geita, 

Athari za vifo pamoja na uharibifu wa miundombinu zinazoendelea kuripotiwa nchini ni sehemu ya tahadhari ya mvua kubwa iliyotolewa Februari, 2024 na Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ikitoa muelekeo wa mmvua hizo kwa kipindi cha Machi hadi Mei mwaka huu.

Mbali na taarifa hiyo, TMA imeendelea kutoa taarifa za hali mbaya ya hewa mara mara ikiwatahadharisha wananchi juu ya mvua kubwa zinazoweza kusababisha mafuriko, uharibifu wa mali na miundombinu.

Kwa siku ya leo TMA imetoa angalizo la mvua kubwa inayotarajiwa kunyesha kwa siku nne hadi Aprili 29, 2024 katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo mikoa ya Dar es Salaam,Tanga,  Lindi, Mtwara, Visiwa vya Mafya, Unguja na Pemba.

Tahadhari hiyo inahusisha mvua kubwa, upepo mkali unaoweza kufika kilomita 40 kwa saa na mawimbi makubwa yanayoweza kufika mita mbili.

Waziri Majaliwa atoa maagizo mazito

Ili kudhibiti madhara zaidi yanayoweza kujitokeza katika kipindi ambacho mvua zinaendelea kunyesha Waziri Majaliwa ametoa maelekezo mbalimbali kwa Serikali na wananchi ikiwemo kuchukua tahadhari na kufuatilia taarifa zinazotolewa na TMA pamoja na viongozi wao.

"Ninawasihi sana wananchi kuwa na subira pindi wanapoona maji mengi yanapita hususan barabarani ili kuepusha ajali zinazoweza kuepukika," amesema Majaliwa.

Kwa upande wa Serikali Majaliwa amezitaka Kamati za Maafa za Wilaya na Mikoa kuendelea kuchukua hatua stahiki ikiwemo kutoa tahadhari kwa wananchi na kusaidia wananchi kwa wakati maafa yanapojitokeza.

Maagizo mengine ni kwa Jeshi la Polisi kupitia Kikosi cha Usalama Barabarani kutoa tahadhari kwa madereva na watumiaji wengine wa barabara wakati wa mvua na Wizara ya Afya kutoa elimu ya afya ya jamii ili kudhibiti magonjwa ya mlipuko pamoja na kuhakikisha upatikanaji wa tiba.

Related Post