TCU yaanika sifa za wanafunzi kujiunga vyuo vikuu Tanzania
- Sifa hizo ni pamoja na kuwa ufaulu mazuri wa masomo unaohitajika katika udahili wa kozi husika.
- Yawataka wanafunzi kutuma maombi moja kwa moja kwenye vyuo.
- Waliomaliza kidato cha sita, stashahada wawekewa vigezo vyao.
Dar es Salaam. Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) leo imefungua dirisha la udahili wanafunzi wa elimu ya juu kwa mwaka 2019/2020 huku ikianisha sifa zinazohitajika ili kuwawezesha waombaji kupata nafasi ya kusoma katika vyuo vikuu mbalimbali nchini.
Udahili wa kujiunga na shahada ya kwanza utahusu waombaji waliohitimu wa kidato cha sita; wenye Stashahada (Ordinary Diploma); na waliomaliza programu ya ‘Foundation’ ya Chuo Kikuu Huria cha Tanzania (OUT).
Kwa mujibu wa taarifa ya TCU iliyotolewa Julai 13, 2019 na Katibu Mtendaji wa TCU, Profesa Charles Kihampa inaeleza kuwa dirisha hilo limefunguliwa leo Julai 15 na litafungwa Agosti 10, 2019.
Katika kuhakikisha waombaji wanafanikiwa kupata nafasi ya kujiunga katika elimu ya juu, wanatakiwa kuzingatia sifa mbalimbali ambazo zimegawanyika katika makundi manne ya waombaji.
Kundi la kwanza linawahusu wanafunzi waliomaliza kidato cha sita kabla ya mwaka 2014 ambao wanatakiwa kuwa na ufaulu wa jumla wa pointi nne kwa masomo mawili ambayo yanahitajika katika programu husika wanayokwenda kusomea.
Kundi lingine ni la wanafunzi waliohitimu kidato cha sita kati ya mwaka 2014 na 2015 ambapo wanatakiwa wawe wamefaulu kwa alama C na kuendelea wakiwa na pointi nne ambazo zinahitajika kwa programu husika.
Wanafunzi wa kundi la tatu ni wale waliomaliza kidato cha sita hadi mwaka huu ambapo wao wanatakiwa kuwa na ufaulu wa jumla wa pointi nne kwa masomo mawili kwa programu husika ya udahili kwenye vyuo vikuu.
Zinazohusiana:
- Safari bado ndefu kufikia 50 kwa 50 elimu ya juu Tanzania
- TCU wafungua dirisha dogo la usajili kwa wanafunzi wa vyuo vikuu
- TCU yaacha maumivu vyuo vikuu, ikivifuta vituo viwali.
Kundi la mwisho ni la wanafunzi waliohitimu programu ya Foundation ya OUT na kupata angalau daraja C kutoka masomo sita katika makundi mahususi ya Sanaa, Sayansi na Biashara.
Wanafunzi hao wanatakiwa kuwa na cheti cha kumaliza elimu ya sekondari (CSEE) au stashahada kutoka chuo kinachotambulika.
Ukokotoaji wa pointi na alama hutofautiana kulingana na mwaka ambao mwanafunzi amehitimu kidato cha sita ambapo waombaji wanashauriwa kupitia mwongozo wa uombaji vyuo ambao wameweka masharti kwa kila programu na chuo.
Kwa wale wenye cheti cha stashahada ambao wanataka kusoma shahada ya kwanza wanatakiwa wawe angalau wamefaulu masomo manne kwa kupata alama D na zaidi katika ngazi ya sekondari (O’Level) au alama zinazotambulika na Baraza la Mitihani la Tanzania (Necta) au Mamlaka ya Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).
Hata hivyo, TCU imewataka wanafunzi wanaofanya maombi ya kujiunga katika vyuo kutuma maombi ya udahili moja kwa moja vyuoni kupitia mifumo ya kielekroniki iliyowekwa na vyuo husika.
Pia wanatakiwa kuwasiliana na vyuo moja kwa moja kupata taarifa za kina kuhusu programu za masomo ili kujiridhisha kabla ya kutuma maombi.
“TCU inawaasa wananchi wasikubali kupotoshwa na watu wanaojiita mawakala au washauri wanaodai wanatoa huduma ya jinsi ya kujiunga na vyuo vya elimu ya juu hapa nchini,” imeeleza taarifa hiyo.