Haya ndiyo magari 10 yanayopendwa zaidi na Watanzania

Rodgers George 0815Hrs   Machi 05, 2020 Biashara
  • Orodha ya 10 bora imetolewa na kampuni ya SBT ya nchini Japan inayoingiza magari yaliyotumika nchini Tanzania.
  • Kwa mujibu wa orodha hiyo, Watanzania wanapendelea “Brand” ya Toyota kwani kati ya aina 10 zilizoainishwa, Toyota zipo aina nane.
  • Kinachoiweka kila gari kwenye nafasi yake, ni idadi ya gari zilizoagizwa kutoka Japan tangu mwaka 1993.

Dar es Salaam.  Kama wewe ni mtumiaji wa mara kwa mara wa barabara hasa katika majiji makubwa Tanzania likiwemo la Dar es Salaam, basi ni rahisi kuona aina fulani ya magari ndiyo yanatawala barabara za maeneo hayo. 

Leo tunakuletea orodha ya magari 10 ambayo yanatumiwa zaidi na Watanzania katika shughuli mbalimbali za kiuchumi na kijamii iliyotokana na uchambuzi uliofanywa na Nukta (www.nukta.co.tz) kupitia kampuni ya Japan ya SBT inayojihusisha na usambazaji wa magari yaliyotumika katika nchi zaidi ya 40 duniani.

Kabla ya kufika kote huko, kama hufahamu maana ya “cc” basi chukua muda kufahamu ili tuendlee kuelewana.

Kwa lugha rahisi, “Cc” ni nguvu ya injini ambayo inapimwa kwa uwezo wake wa kutumia mafuta. Kadri cc ya injini inavyokuwa kubwa ndivyo injini hiyo hutumia mafuta mengi zaidi. 

Hii ndiyo orodha ya magari 10 yanayotumiwa zaidi na Watanzania.

10.Subaru Impreza

Ulihisi ni ipi? Kama jibu lako ni Subaru Impreza hakika uko sahihi. Gari hiyo ambayo imeshika nafasi ya 10, injini yake ina uwezo hadi cc2,212, bei ya chini ya kuagizia gari hiyo kwenye tovuti ya SBT ni Sh4.9 milioni huku gharammaza kodi zikiwa hazijahesabiwa.

9.Toyota Corolla Lumion

Kama umefikiria mbali na Toyota Corolla Lumion, jaribu kufikiria namba ijayo huenda utapatia. Lumion ambayo imeshika nafasi ya tisa, uwezo wa injini yake ni cc1,496 hadi cc1,797 inaagizwa kwa bei ya kuanzia Sh5.06 milioni. Kumbuka, bei hiyo haihusishi gharama za kodi,

8.Toyota Ractis 

Nafasi ya nane imeshikiliwa na gari fulani hivi. Siyo jingine ni Toyota Ractis ambayo injini yake ina uwezo  wa cc1,296 hadi cc1,496 na gharama yake nje ya kodi ikiwa ni kuanzia Sh4.5 milioni kwenye tovuti ya SBT. Ractis ina vizazi viwili. Cha kwanza ni cha mwaka 2005 hadi 2010 na cha pili ni mwaka baada ya 2010 hadi sasa.

Kama ilivyo kwa Toyota IST basi na Toyota Ractis imeingia kwenye 10 bora. Picha|Mtandao.

7.Subaru Forester

Uliwahi kufikiria kuwa Watanzania wanaweza wakaipenda Subaru Forester kiasi hicho? Forester ambayo ni gari ya pili kutoka kampuni ya Subaru kuingia kwenye orodha hii baada ya Subaru Impreza inapatikana kwa gharama ya kuanzia Sh4.5 milioni huku uwezo wa injini yake ukiwa ni cc1,994. Usisahau kuwa kodi haihusiki hapo.

6.Toyota Corolla Spacio

Hizi nazo zipo nyingi ati! Toyota Corolla Spacio imeshika nafasi ya sita huenda ni kwasababu ya sifa ya kuwa na nafasi ndani ya gari na hivyo kufaa kwa matumizi ya familia. Spacio inayouzwa kuanzia Sh4.7 milioni injini yake ina cc1,496 hadi cc1,794.

5. Toyota Premio

Je ni Benzi? Hapana ni Toyota Premio ambayo bei yake ya chini ya kuagizia ni Sh5.4 milioni huku uwezo wa injini yake ukiwa ni cc1,496 hadi cc1,998. Wadau wa Nukta wamesema wale wote waliopenda Toyota sprinter na matoleo ya kale ya aina ya gari za Saloon, wataifurahia hii pia.

4.Toyota Alphard 

Huenda unadhani ni Toyota Rav4 au gari lingine lakini hapa imekaa Toyota Alphard ambayo gharama yake ni kuanzia Sh6.9milioni huku uwezo wa injini yake ukiwa ni cc2,362 hadi cc3,456. Gari hii iko nafasi ya nne inafaa kwa matumizi ya familia na ofisi kwani ina nafasi kubwa na muonekano wa kifahari kwa aina ya gari za “mini van”.


Zinazohusiana


3. Toyota Harrier

Ndinga aina ya Toyota Harrier ambayo injini yake ina uwezo wa kuanzia cc1,986 hadi cc3,456 inasifika kwa kuinuka na uwezo wake wa kupita kwenye kila aina ya barabara. Zaidi gari hizi ni imara. 

Toyota Harrier katika nafasi ya tatu katika tovuti ya SBT inapatikana kwa gharama ya kuanzia Sh10.6 milioni huku muonekano wake ukikosha mioyo ya Watanzania wanaoweza kuimudu.

2. Toyota Crown

Kama ulitegemea gari  tofauti na Toyota Crown basi fikiria upya. Gari hiyo ambayo inaagizwa kwa kima cha chini cha Sh4.5 milioni bila kuhusisha kodi muonekano wake wa ndani unaweza kukusahaulisha shida za dunia.

Crown ambayo wamiliki wake hujiita “Royalty” yaani wanafamilia wa ukoo wa kifalme ina injini yenye uwezo wa cc1,988 hadi  cc2,997.

Toyoya IST ndiyo gari inayotumiwa na idadi kubwa ya Watanzania katika shughuli zao za usafiri. Picha|mtandao.

1.Toyota IST

Kama hujaweza kubaini hadi sasa hakika unahitaji mapumziko ya muda mrefu. Nafasi hii ya dhahabu imeenda kwa Toyota IST ambayo sifa yake ya kutumia mafuta kiasi imefanya gari hizi kutumika kwa usafiri wa “Uber”.

Gari hiyo ambayo uwezo wa injini yake ni kuanzia cc1,298 hadi cc1,797 inaweza kuagizwa kwa Sh4.8 milioni kama bei ya chini zaidi kwenye tovuti ya SBT. Bei hiyo haijajumuisha kodi.

Kama uliweza kubashiri hata gari moja, wewe ni noma! 

Mratibu wa biashara za kimataifa wa kampuni ya SBT kutoka Japan Muzzamil Ihsan ameiambia Nukta (www.nukta.co.tz) kuwa orodha ya gari yanayopendwa na Watanzania imetolewa kwa mujibu wa taarifa za gari zilizoingizwa nchini Tanzania tangu kampuni hiyo ianze biashara na Tanzania 1993.

“Orodha hii imetolewa kwa kuangalia idadi ya magari yaliyoagizwa kutoka Japan hadi Tanzania tangu SBT ianze kufanya kazi nchini Tanzania,” amesema Ihsan.

Pia magari hayo yananunuliwa kwa wingi kwa sababu wananunuzi wanahimili gharama zake, urahisi wa upatikanaji wa spea, na matumizi mazuri ya mafuta.

Habari hii imeboreshwa leo Machi 6, 2020.

Related Post