33 wafariki kwa maafa ya mafuriko Rufiji, Morogoro

Sayuni Kisige 1103Hrs   Aprili 12, 2024 Afya & Maisha
  • Ni kutonana na mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha.
  • Wakazi 1,114 waokolewa Rufiji.
  • Nyumba 1,035 zabomolewa na 6,874 zazingirwa na maji.


Dar es salaam. Watu 33 wameripotiwa kupoteza maisha katika mikoa ya Pwani na Morogoro, kutokana na mafuriko yalityochangiwa na mvua za El Nino zinazoendelea kunyesha katika maeneo mbalimbali nchini, mamlaka zimebainisha.

Msemaji Mkuu wa Serikali Mobhare Mahinyi, aliyekuwa akizungumza na wanahabari leo Aprili 12, 2024 jijini Dar es salaam amesema mvua kwa mujibu wa tathmini iliyofanyika mpaka leo jumla ya watu watano wamepoteza maisha wilayani Rufiji huku watu 28 wakipoteza maisha mkoani Morogoro.

“Kwa ujumla kata 12, kati ya 13 za Wilaya ya Rufiji na kata tano kati ya kata 13 katika Wilaya ya Kibiti na kata moja katika Wilaya ya Kisarawe zimeathirika, na takribani watu 1,114 wameokolewa katika Wilaya ya Rufiji peke ake,” amesema Matinyi.

Matinyi ameongeza kuwa uharibifu mwingine uliotokea ni wa mazao ya chakula kama mahindi, mpunga, ufuta mihogo, mtama na pamba pamoja na miundombinu ikiwemo makazi, madaraja ,nguzo za umeme, barabara na kituo cha afya cha kijiji cha Muhoro wilaya ya Rufiji kimesombwa na maji.

Aidha, mkoani Morogoro pamoja na vifo 28  mafuriko hayo yamesababisha maafa katika halmashauri 8 za mkoa huo kwaa kubomoa nyumba 1,035 na nyingine 6,874 zimezingirwa na maji.

Kwa mujibu wa Matinyi  jumla ya hekari 34,970 za mazao mbalimbali zimeathirika pamoja na mifugo inayofikia jumla ya 1,466 na miundombinu mbalimbali kama reli ya TAZARA, barabara makalvati, madaraja vimeathiriwa na mafuriko hayo.

Hata hivyo, Matinyi amekanusha madai ya uhusiano kati ya mafuriko hayo na kufunguliwa kwa maji katika bwawa la kufua umeme la Mwalimu Nyerere akisema bwawa hilo limefanya kazi kubwa ya kuzuia mafuriko hayo ambayo yangeanza tangu mwezi Oktoba mwaka 2023.

Misaada kuendelea kutolewa

Matinyi amebainisha kuwa  kamati za wilaya na mkoa zinazosimamia maafa zinaendelea na kazi ya kufanya tathmini juu ya uharibifu na kuangalia mahitaji yanayohitajika ili Serikali kuu itoe msaada.

“Misaada imeanza kuwasili kutoka kwa wadau mbalimbali na imekuwa ikipokelewa na kufikishwa kwa wahusika”…

…Dawa za tiba ya maji kuhakikisha maji yanakuwa salama, huduma za afya chakula,malazi, uokozi, usalama, ushauri nasaha na askari maalumu wa maliasili wakusaidia kupambana na tatizo la mamba wanaokuja na maji vyote vimefikishwa katika maeneo ya waathirika,” amesema Mahinyi.

Ikumbukwe kuwa Agosti 26, 2023 Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) ilitoa taarifa ya uwezekano wa kuwapo kwa mvua kubwa za El-Nino kuanzia Oktoba 2023 hadi Februari 2024. 

Baadaye TMA ilisema  mvua hizo zitaendelea na kuungana na mvua za masika na kuendelea hadi Mei

Related Post