Tanzania inavyokabiliana na ongezeko la kina cha maji bahari ya Hindi

Sayuni Kisige 0522Hrs   Aprili 05, 2024 Habari
  • Itatunga sera mpya ya uchumi wa buluu.
  • Inatafuta fedha kujenga kuta katika maeneo ya fukwe.
  • Hatua hizo zitasaidia kupunguza athari za ongezeko la kina cha maji.



Dar es salaam. Serikali ya Tanzania imesema imejipanga kukabiliana na athari za kuongezeka kwa kina cha maji katika bahari ya Hindi ikiwemo kuja na sera mpya ya uchumi wa buluu ili kuhakikisha usalama wa wananchi na miundombinu.

Waziri wa Nchi (Muungano na Mazingira) Dk Selemani Jafo aliyekuwa akizungumza leo Aprili 5, 2024 Bungeni jijini Dodoma, amesema kina cha maji cha bahari ya Hindi hapa Tanzania kinaongeza kwa sababu ya kuongezeka kwa joto na kuyeyuka kwa barafu duniani.

“Kwa mujibu wa tafiti na vipimo vilivyopo maji ya bahari ya Hindi katika pwani ya Dar es salaam yameongezeka kwa milimita sita kwa mwaka tangu mwaka 2002,” amesema Jafo.

Amesema ongezeko hilo limeathiri fukwe za bahari na miundombinu kama barabara, makazi, upotevu wa mikoko na nyasi za bahari na visima vya maji baridi kuingia chumvi.

Waziri Jafo alikuwa akijibu swali la Profesa Patrick Ndakidemi aliyetaka kujua mpango wa Serikali kukabiliana na athari hizo na kuyalinda maeneo mbalimbali ya kuzunguka bahari ya Hindi.

“Kwa kuwa Serikali imekiri kwamba kuna ongezeko la kina cha maji baharini je, Serikali ina mpango gani wa kuyalinda maeneo haya ili yasije yakazama kwenye maji” …

...ni tatizo la kidunia je, Serikali inashirikianaje na wadau mbalimbali wa kimataifa ili kukabiliana na changamoto hii?,” amehoji Prof Ndakidemi.


Soma zaidi: Serikali kufumua sera za uwekezaji, viwanda Tanzania


Serikali yatoa mwelekeo mpya

Waziri Jafo amesema Serikali inatambua athari zinazoendelea maeneo mbalimbali ikiwemo kisiwa cha Pemba. hivyo inakuja na sera mpya ya uchumi wa buluu ambayo inalenga shughuli endelevu za kiuchumi za baharini na kuangalia korido zote za bahari na jinsi ya kuzilinda.

Ameongeza kuwa Serikali itashirikiana na wananchi wanaoishi karibu na bahari kutoa elimu ya kuyalinda maeneo yao ikiwemo uhamasishaji wa upandaji wa miti ili kukabiliana na athari hizo.

“Serikali ina mahusiano mazuri na UNEP (Shirika la Mazingira la Umoja wa Mataifa), FAO (Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Taifa ), UNDP (Programu ya Maendeleo ya Umoja wa Mataifa) lakini sasa hivi tunafanya mchakato mkubwa wa kujiunga na shirika kubwa la GGI kule Korea kwa lengo la kupata fedha kuweza kusaidia shughuli za maendeleo katika nchi yetu,” amesema Waziri Jafo.

Waziri Jafo amebainisha kuwa Serikali inaendelea kutafuta fedha kwa ajili ya ujenzi wa kuta katika maeneo ya fukwe kukabiliana na athari tajwa.

“Kuna uwezekano mkubwa kwamba 2024 utakuwa mwaka wa joto zaidi katika rekodi, Umoja wa Mataifa (UN) umesema siku ya Jumanne. 

"Hatuwezi kusema kwa uhakika," lakini "ningesema kuna uwezekano mkubwa kwamba mwaka 2024 utavunja tena rekodi ya mwaka 2023," Omar Baddour wa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) amesema wakati wa uwasilishaji wa ripoti ya kila mwaka ya hali ya hewa Machi 19, 2024.  

Related Post