Wanaoumwa kipindupindu Mwanza wafikia 80

Mariam John 0902Hrs   Januari 16, 2024 Afya & Maisha
  • Waongezeka kutoka 34 walioripotiwa wiki moja iliyopita.
  • Jamii yaonywa kuzingatia kanuni za afya, kuacha dhana potofu.

Mwanza. Licha ya juhudi za kukabiliana na ugonjwa wa kipindupindu zinazoendelea mkoani Mwanza, idadi ya watu wanaougua ugonjwa huo imeongezeka na kufikia 80, tangu ugundulike kuwepo jiji hilo la Kanda ya Ziwa Januari 4, 2024.

Hii ni mara ya tatu kwa visa vya ugonjwa huo kuongezeka kwa kuwa Januari 10, 2024, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza Dk. Thomas Rutachunzibwa alitangaza idadi ya wagonjwa kufikia 34 ambaao waliongezeka kutoka saba walioripotiwa awali.

Kwa mujibu wa Waziri wa Afya Ummy Mwalimu mpaka Januari 12, 2023 mikoa 6 ya Mwanza, Shinyanga, Ruvuma, Tabora, Simiyu na Kagera tayari ilikuwa inakabiliwa na ugonjwa huo.


Soma zaidi : Unavyoweza kuepuka ugonjwa wa ‘red eyes’


Pamoja na hatua za kiafya zilizochukuliwa ikiwa ni pamoja na kuzuia matanga ya muda mrefu,  Dk. Rutachunzibwa ametoa wito kwa vyombo vya habari kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusiana na namna ya kujikinga na ugonjwa huo ili kuepukana na maambukizi zaidi.

“Kwa sasa tunatazama zaidi mikusanyiko ya misiba kwa kuwa ndipo kwenye chanzo cha maambukizi hayo na tunashauri unapotokea msiba ni vyema jamii ikashiriki kwenye mazishi pekee na kusambaa,” amesema Dk. Rutachunzibwa.

Mikakati mingine inayotekelezwa ni pamoja na kuhamasisha jamii kula chakula cha moto, pamoja na kunywa safi maji yaliyochemshwa au kutibiwa kwa kidonge kinachosambazwa cha Aquatabs.

“Kidonge hiki kimoja kinatumika kutibu ndoo ya lita 10 na viwili kwa ndoo ya lita 20, na kidonge hichi kinatakiwa kuhifadhiwa sehemu isiyokuwa na mwanga mkali kwa kuwa kikiachwa hapo kinaweza kusababisha madhara mengine ya kiafya,” amesema Dk. Rutachunzibwa.

Maji yaliyogandishwa hayaui vimelea

Renald Mlyakado ambaye ni Mratibu wa Elimu ya Afya kwa Umma, aliyekuwa akitoa elimu kwa waandishi wa habari, ameitaka jamii kuondoa dhana potofu kuwa, kuweka maji kwenye jokofu  au kuyaacha kwenye ndoo kwa muda mrefu yanasababisha wadudu kuganda na kufa.

Mlyakado amedai dhana hiyo sio ya kweli badala yake, wadudu husinyaa tu kwa muda na iwapo mtu atatumia maji yenye vimelea yaliyokaa muda mrefu atakuwa hatarini kupata kipindupindu.

“Kwahiyo tusidanganyike kuwa kuweka maji kwenye friji kunaua wadudu hao hapana, tunachoshauri ni mtu kuchemsha maji na kuyahifadhi vizuri kabla ya kuyatumia,” amesema Mlyakado

Related Post