Biashara ya juisi inavyowatoa kimaisha wasomi waliokataa kuajiriwa

TULINAGWE MALOPA 0029Hrs   Novemba 12, 2018 Maoni & Uchambuzi
  • Ni wale waliomaliza vyuo vikuu wakiwa na ndoto za kufanya ujasiriamali na kuachana na fikra za kuajiriwa. 
  • Juisi hiyo hutengenezwa kwa matunda ya asili na kuuzwa kwenye vibanda vilivyopo katika vituo vya mafuta.
  • Waatalam wa biashara wapendekeza kuboreshwa kwa mazingira ya kufanyia biashara hiyo.

Dar es Salaam. Biashara ni ubunifu sio tu wa kutengeneza bidhaa bora bali ni uwezo wa kuweka bidhaa hizo katika mazingira yanayowavutia wateja wengi. 

Wauzaji wa juisi ya matunda maarufu kama sharubati wamegundua njia rahisi ya kuwafikia wateja wao. Ni kuweka vibanda vya juisi hizo katika vituo vya mafuta (sheli) ili kuwapata watu wanaoingia na kutoka kununua mafuta kwa ajili ya magari.

Dereva halazimiki tena kuzunguka maeneo mbalimbali kufuata huduma lakini kwenye kituo cha mafuta anaweza kufanya miamala ya kifedha, kununua bidhaa mbalimbali  kwenye ‘minisupermarkets’. Wakati akisubiri huduma nyingine, juisi ya matunda ya asili itamuhusu.

Shurabati hizo hutengenezwa kwa matunda mbalimbali kama embe, karoti, stafeli, tende, nanasi, ukwaju, machungwa na mapapai. Juisi hizo huongezwa viungo na ladha tofauti tofauti ikiwemo tangawizi ili kumuongezea mnywaji hamu ya kunywa kwa kiwango kinachohitajika. 

Kutokana na umaarufu wake imevutia idadi kubwa ya vijana jijini hapa ambao wanatumia kama fursa ya kujiajiri na kuingiza kipato kwaajili ya kuboresha maisha.

Katika matembezi, Nukta imebaini uwepo wa vibanda vya juisi katika sheli zilizopo maeneo mbalimbali ya Jiji la Dar es Salaam hasa Tabata, Sinza, Mikocheni, Mwenge na Mbezi na kukutana na baadhi ya wamiliki wa vibanda vya juisi asilia ya matunda.

Natalia Alia, mhitimu wa Chuo cha Usimamizi wa Fedha (IFM) ni mwanadada  aliyethubutu kufanya biashara hii ya juisi akiwa na lengo la kujipatia kipato kama mjasiriamali ambaye hakutaka kuajiriwa baada ya kumaliza masomo yake. 

Alianza kufanya biashara hiyo akiwa chuoni ambapo alikuwa akiwauzia wanafunzi wenzake na kusambaza katika maeneo ya karibu.

Kwasasa ana ofisi yake kubwa inayojulikana kama “Zanana Juice Box” katika mgahawa wa Tripple 7 Mikocheni unahudumia watu mbalimbali wanaotumia sheli zilizo karibu na eneo hilo.

Ili aendelee kuwahudumia wateja wake inafanya juhudi kuzikabili changamoto za malighafi na matunda kwasababu hupatikana kwa msimu kulingana na kiwango cha uzalishaji.

“Mwanamke ni bidhaa, usipojipanga ukiwa na umri mdogo unajitengenezea mazingira magumu. Ukiwa mdogo na mchanga pambana kujikwamua kiuchumi bila kumtegemea mtu,” anasema Natalia.

Dogo Janja naye ni mdau muhimu wa Zanana Juice. Picha| deskgram.net

Biashara hiyo imewavutia pia vijana wa kiume ambao wameweka kando usomi wao na kujitosa kuuza juisi ya matunda ili mkono uingie kinywani na maisha yazidi kusonga mbele.

Kibanda kingine cha “Mak Juice” kilichopo katika sheli ya Oilcom, Sinza Africa Sana kinaendeshwa na kijana Makoye Philbert ambaye alikuwa mwajiriwa wa benki kabla ya kufanya biashara mbalimbali  ikiwemo ya kuuza chipsi na baadaye kujikita katika kuuza juisi.  

Bado hakuona kama biashara hiyo inamfaa, mpaka alipofanya uchunguzi kutoka kwa watu wa karibu na jamii yake kwa ujumla na kupata wazo la kuanzisha kibanda cha juisi kutokana na kutokuwepo kwa vibanda hivyo kwa wakati huo.

“Hakuna kitu ambacho ni rahisi, nimeanzia mbali sana na kupitia mengi ila kwa kutia juhudi na kumshirikisha Mungu kila kitu kitakwenda sawa” anasema Makoye.

Wateja wengi anaowapata katika ofisi yake ni wasanii, marafiki zake na jamii inayomzunguka huku biashara hiyo ikimpatia faida lukuki katika kuendeleza maisha yake.


Zinazohusiana:


Lakini sio vijana wote wenye uthubutu wa kuanzisha biashara kama hizi za kujikimu na siku ukiachilia mbali vikwazo wanavyopitia katika biashara katika maisha yao ya kila siku. 

Kibanda cha Mak Juice nacho kimejipatia umaarufu mkubwa katika maeneo ya Sinza Africa Sana. Picha| clipzui.com

Kennedy Mlawa ni kijana mwingine mjasiriamali kutoka Chuo Kikuu cha Tumaini (TUDARCO) ambaye kitaaluma ni mwanasheria amejitosa katika biashara ya juisi akiamini ni njia sahihi ya kumuingizia kipato. 

Kibanda chake cha “G Juice” kinapatikana Tabata sheli ambapo amefanikiwa kujipatia wateja wengi wanaotoka maeneo mbali ya Tabata na Segerea.  Kinachompa matumaini ya kuendelea kuwepo katika biashara hiyo ni bidii, uvumilivu na ushirikiano anaoupata kutoka kwa familia yake.

 

Kwanini biashara hiyo imewekwa sheli?

 Mtaalamu wa maswala ya biashara na ujasiriamali, Charles Nduku anasema umaarufu wa vibanda vya juisi katika vituo vya mafuta unatokana na utashi wa mtu katika kuwapata wateja popote walipo.

“Cha muhimu ni Target customers (watejwa walengwa) ambayo mtu anaamini wateja anaowalenga watapatikana kwa urahisi,” anasema Nduku.

Anasema kanuni za ujasiriamali zinaeleza kuwa kinachomvutia mteja ni mpangilio mzuri wa bidhaa na usafi katika eneo la biashara na mambo mengine ikiwemo sehemu zenye mkusanyiko wa watu wengi.

“Lazima mazingira, mpangilio wa biashara na watu wanaohudumu katika biashara hiyo wawe katika hali inayovutia wateja ili kuvutia watu,” anasema Nduku.

Hata hivyo, anaamini kuwa biashara ya juisi inaweza kufanyika katika maeneo mengine na ikazalisha faida kubwa ikiwa tu mfanyabiashara atafanikiwa kuwapatia wateja wake bidhaa bora zinazoendana na thamani ya pesa

Related Post