Magufuli mbioni kufungua vyuo, michezo Tanzania

Nuzulack Dausen 0732Hrs   Mei 17, 2020 NuktaFakti
  • Amesema amepanga kufungua vyuo iwapo mwenendo wa kushuka wagonjwa wa corona utaendelea wiki inayoanza Mei 18.
  • Aagiza watu wote wanaofariki hata kwa corona kuzikwa kwa heshima.
  • Amesema mwanae mmoja alipata corona, alipona kwa kujifukiza, malimao.

Dar es Salaam. Rais John Magufuli amesema wagonjwa wa Corona Tanzania wanazidi kupungua na kwamba iwapo mwenendo huo utaendelea kuanzia wiki ya Mei 18 amepanga kufungua vyuo ili wanafunzi waendelea na masomo yao.

Katika hotuba yake ya salamu kwa Taifa alizozitoa katika kanisa la KKKT Usharika wa Chato leo (Mei 17, 2020) amesema kuwa taarifa alizopewa kuwa idadi ya wagonjwa wa ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) imepungua japo hakutaja idadi kamili ya wagonjwa waliopo nchini.

“Katika hali halisi Mungu amesikia sara zetu kwa taarifa za leo nilizoeletewa wagonjwa wamepungua sana hata katika hospitali zetu,” amesema Rais Magufuli. 

Mkuu huyo wa nchi amesema hospitali ya Amana jijini Dar es Salaam ambayo ilikuwa inalaza watu 198 leo walikuwepo watu 12 tu huku Hospitali ya Mloganzila ikiwa na wagonjwa sita tu wakati ilikuwa inalaza watu 30.

Huko Kibaha mkoani Pwani kwenye kituo cha Lulanzi chenye uwezo wa kubeba wagonjwa zaidi ya 50, Rais Magufuli amesema hadi leo wamesalia wagonjwa 22 ambao afya zao zipo vizuri ila bado vipimo vinaonyesha wana virusi vya corona.

“Kwenye hospitali ya Aga Khan nako wamepungua wamebaki 31, Hindu Mandar 16, Regency 17, TMJ saba, Rabininsia  kule Tegeta wapo 14. Kwa hiyo unaweza kuona trend (mwenendo) ya majibu ya bwana Mungu wetu yalivyofanya kazi,” ameeleza Rais Magufuli.

Dk Magufuli amesema hata kwenye vituo vya mikoani kama Mwanza, Arusha na Dodoma idadi ya wagonjwa wa COVID-19 wameendelea kupungua huku baadhi ya vituo vilivyopo Ukerewe, Buchosya na Sengerema vikiwa havina wagonjwa.

Kutokana na mwenendo huo, Rais Magufuli amewataka Watanzania kuendelea kuchukua tahadhari na kumuomba Mungu kuhakikisha ugonjwa huo hauendelei kusambaa.

“Kwa ‘trend’ (mwenendo) hii ninavyoiona kama wiki hii tunayoianza kesho (Mei 18) itaendelea hivyo nimepanga kufungua vyuo ili wanafunzi wetu waendelee na masomo. Lakini nimepanga pia sisi kama Taifa kuruhusu michezo iendelee kwa sababu michezo ni sehemu ya burudani kwa Watanzania,” amesema Rais Magufuli.


Soma zaidi: 


Kwa miezi miwili sasa wanafunzi wa shule za awali, msingi, Sekondari na vyuo vikuu Tanzania wamekuwa majumbani baada ya Serikali kuzifunga taasisi hizo katikati mwa Machi ili kudhibiti kusambaa kwa COVID-19.

Hii ni mara ya pili Rais Magufuli anaelezea uwezekano wa kufungua shughuli za michezo baada ya hotuba yake mapema mwezi huu kudokeza kuwa alikuwa akisubiria ushauri wa wataalamu ili afungue ligi kuu ya soka.

Dk Magufuli amesema Watanzania wanatakiwa kupunguza hofu dhidi ya ugonjwa huo.

“Mimi napozungumza nina mtoto wangu alipata corona, mtoto wa kumzaa mimi, amejifungia kwenye chumba, akaanza kujitibu, akajifukizia, akanywa malimao na tangawizi amepona yupo mzima sasa anapiga ‘push ups’,” amesema Dk Magufuli.

“Huu ndiyo ukweli na siwezi kusema uwongo mbele ya madhabahu hapa. Kwa sababu ninamheshimu Mungu wangu na nampenda Mungu na nampenda Yesu wangu,” ameongeza.

Kwa mujibu wa Kituo cha Kudhibiti Magonjwa cha Afrika (AfricaCDC) tangu ugonjwa huo uingie Tanzania katikati mwa Machi mwaka huu hadi leo Saa 3 asubuhi kulikuwa na wagonjwa 509, vifo 21 na watu 167 wameshapona. 


Aagiza waliofariki kwa corona kuzikwa kwa staha

Rais Magufuli pia ameagiza madaktari na wizara ya afya kuhakikisha watu wote watakaofariki hata kwa ugonjwa wa corona wanatakiwa kuzikwa kwa heshima na kushirikisha ndugu zao akieleza kuwa “katika mpango wa kupambana na Corona kuna mambo ya hovyo yameingiziwa humu ndani.”

“Wapo watu wamekuwa wakifariki, amefariki kwa ugonjwa mwingine kwanza wanang’ang’ania kumpima. Wewe ameshafariki unampima ufanye nini? Nguvu za kumpima wanazo lakini za kumuhudumia mpaka afariki hawana na akipimwa kila kitu kinaandikwa corona na wanamzuia asiende kuzikwa na ndugu zake...sasa kama umempima unaogopaje kumruhusu ndugu zake waende wakamzike mahali walipo,” ameeleza.

Related Post