Tahadhari: Epuka tovuti hizi zinazopotosha kuhusu Corona

Mwandishi Wetu 0922Hrs   Mei 15, 2020 NuktaFakti
  • Tovuti hizo zimekuwa na taarifa za uzushi mara kadhaa kuhusu viongozi mbalimbali duniani ikiwemo Tanzania.
  • Chukua tahadhari ya kuthibitisha habari husika iwapo zimetoka katika tovuti hizo
  • Zote ni nje ambazo habari zake huvutia hata baadhi ya vyombo vya habari vya ndani kuripoti habari hizo za uzushi.

Dar es Salaam. Ugonjwa wa virusi vya Corona (COVID-19) siyo tu ni janga linalohatarisha afya na maisha ya watu bali linatumika kama kichocheo cha habari za uzushi hasa zile zinazosambazwa mtandaoni.

Baadhi ya watu wenye nia ovu wamekuwa wakisambaza taarifa zisizo za kweli kuhusu viongozi, watu wa kawaida na wagonjwa wa Corona kwa nia ya kuleta taharuki na kuzorotesha mapambano dhidi ya COVID-19.

Mathalan, mwezi Machi 2020 tovuti ya mcmnt.com ilichapisha taarifa ya uongo au famba ikiwa na kichwa cha habari “Tanzania confirms first case of Coronavirus” (Tanzania ya thibitisha kisa cha kwanza cha mgonjwa wa Corona)

Sehemu ya taaifa hiyo iiliyochapishwa kabla ya mgonjwa wa kwanza kugundulika Tanzania ilisema kuwa mgonjwa huyo ana miaka 36 ni mkazi wa Dodoma.Jambo ambalo wizara ya afya ilikuja kukanusha baadaye.

Pia tovuti hiyo imekuwa ikichapisha taarifa nyingine za uzushi ikiwemo iliyobeba kichwa cha habari “Vatican confirms Pope Francis and two aides test positive for Coronavirus” (Vatican wamethibitihsa kuwa Papa Francis na wasaidizi wake wa wili wakutwa na corona)

Nukta Fakti imebaini kuwa tovuti nyingine ambayo unatakiwa kuwa makini  pale unaposoma habari zake ni ya UCR World News (www.urtv.com) ambayo ilichapisha  taarifa ya uzushi kuwa Waziri wa Afya wa Tanzania amekutwa na virusi vya corona wakati haikuwa kweli.


Zinazohusiana:


Habari hiyo kutoka katika tovuti hiyo  iliandikwa kwa lugha ya  Kiingereza ikiwa na kichwa cha habari “Tanzania’s health minister test positive for coronavirus” (Waziri wa Afya wa Tanzania akutwa na virusi vya corona).

Historia ya kidijitali inabainisha kuwa tovuti hiyo ilianza kutengenezwa mwaka 2011 lakini haikuchapisha habari yeyote ya msingi hadi Machi 2020 ilipochapisha habari ya uzushi kuhusu Malikia Elizabeth ambapo sehemu kubwa ya habari zake zinahusu corona.

Tovuti nyingine ya habari ni ya cbn2.com ambayo nayo taarifa zake nyingi zimekuwa ni za kupotosha mathalani Machi 13, 2020 tovuti hiyo ilichapisha habari iliyosema “Breaking: Former President Kenneth Kaunda dead at age 95” (Rais wa zamani (wa Zambia) Kenneth Kaunda amefariki dunia akiwa na umri wa miaka 95).

Habari hiyo siyo ya kweli kwa sababu Kaunda bado yuko hai na umri wa miaka 96 na sio 95 kama ilivyoripotiwa na tovuti hiyo.

Pia tovuti hiyo ilichapisha habari yenye kichwa cha habari “Pope Francis Tests Positive For Coronavirus, Vatican Releases Report” (Baba Mtakatifu Francis ana ugonjwa wa Corona)

Ni kweli Baba Mtakatifu Francis alipimwa lakini hakukutwa na maambukizi ya ugonjwa wa Corona.

Ukweli ni upi sasa

Nukta Fakti imebaini kuwa tovuti hizo zimekuwa zikiandika habari lakini kwa upande mwingine zimekuwa zikichapisha habari za uongo au famba dhidi ya viongozi mashuhuri duniani hasa zinazohusu Corona .

Hivyo basi unatakiwa kama msomaji kuwa makini wakati unasoma habari mtandaoni. Kabla ya kufanya maamuzi au kutuma kwa watu wengine taarifa hizo ni vema uzithibitishe kama ni kweli zinatoka katika vyanzo sahihi.

Pia angalia vyombo vya habari vingine vinaongelea nini kuhusu habari husika. Hii itakusaidia kubaki salama dhidi ya taarifa za uzushi.

Endelea kusoma www.nukta.co.tz na kutufuata kwenye mitandao yetu ya Nukta Fakti kujua mbinu zaidi za kung’amua habari za uzushi.

Related Post