Rais Samia: Posho ya kufundishia kwa walimu ni mzigo kwa Serikali

Daniel Samson 0339Hrs   Mei 02, 2023 Maoni & Uchambuzi
  • Asema “inaongeza mzigo mzito kwenye kapu la Serikali”
  • Aahidi Serikali kulitazama suala hilo.
  • Wadau wasema posho hiyo ilikuwa inatoa motisha na ari kwa walimu.

Dar es Salaam. Rais Samia Suluhu Hassan amesema posho ya kufundishia kwa walimu ni mzigo kwa Serikali lakini atakaa na watendaji wake kuona namna ya kushughulikia suala hilo. 

Miaka ya nyuma Serikali ilikuwa ikiwalipa walimu nchini posho zao za kufundishia ambayo ilikuwa ikijumuishwa kwenye mishahara yao ya kila mwezi.

Posho hii kwa mujibu wa wachambuzi wa elimu ilisaidia kumpunguzia makali ya maisha mwalimu sambambamba na kumuongezea ari ya kufanya kazi na moyo wa kujituma katika kazi.

Hata hivyo, Serikali ilifuta posho hiyo na tangu wakati huo walimu na wadau wa elimu wamekuwa wakikumbushia katika majukwaa mbalimbali.

Pia katika sherehe ya maadhimisho ya Siku ya Wafanyakazi Duniani zilizofanyika kitaifa mkoani Morogoro jana Mei Mosi 2023, suala hilo lilibuiliwa tena na Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Tumain Nyamhokya.

Nyamhokya wakati akimkaribisha Rais Samia kuzungumza na wafanyakazi alisema ameona moja ya bango lililobebebwa na walimu likiuliza kuhusu teaching allowance (Posho ya kufundishia).

“Kuna neno dogo nimeliona wameliweka hapa nami limekuwa likinipa shida, kuna kitu kinaitwa “teaching allowance” wamekiweka kwenye mabango yao, kilikuwepo siku za nyuma, katikati hapo kikapotea, kikafifia leo wametukumbusha Mheshimiwa Rais ikikupendeza katika maneno utakayozungumza basi usiwasahau watumishi walimu katika hayo,” alisema Rais huyo.


Soma zaidi: 


Huu ndiyo msimamo wa Serikali

Rais Samia akizungumza na wafanyakazi jana amesema suala la teaching allowance Serikali imelichukua na itaenda kulifanyia kazi kulingana na uwezo wa nchi. 

“...tumelichukua tutakwenda kuliangalia, uwezo wa nchi halafu tuone tutafanya nini kwenye hili,” amesema Rais Samia.

Kiongozi huyo mkuu wa nchi amesema posho ya kufundishia inaweza kuwa mzigo kwa Serikali kwa sababu kada ya ualimu ina watumishi wengi.

“Walimu na sekta ya afya ni jeshi kubwa, kwa hiyo allowance za walimu hata zikiwa ndogo ukiziweka kwa pamoja ni mzigo mkubwa kwa Serikali, inaongeza mzigo mzito kwenye kapu la Serikali,” amesisitiza Rais.

Wizara ya Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) inaeleza kuwa hadi Februari, 2023 kulikuwa na walimu wa shule za msingi na sekondari 260,564.

Walimu waliopo ni sawa na upungufu wa zaidi ya nusu ya mahitaji halisi ya walimu 536,821.

“Suala la motisha kwa walimu ni muhimu, naomba turudishe posho ya kufundisha kwa walimu, tunazungumzia kitu kidogo Sh4,000 kwa siku, hii itahamasisha walimu kufanya kazi na hili wamekuwa wakiomba kwa muda mrefu,” alisema Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo bungeni Mei 10, 2022. 


Related Post