Utaoa, utaolewa lini: Jinsi unavyoweza kukabiliana na msukumo wa nje wa ndoa

Mwandishi Wetu 0422Hrs   Januari 07, 2018 Maoni & Uchambuzi
  • Hofu ya umri kututupa mkono na maswali ya tutatoa au kuolewa lini yamefanya wengi waingie kwenye ndoa zenye matatizo.
  • Ndoa ni matokeo ya msukumo wa ndani na siyo wa nje.
  • Kuoa au kuolewa siyo fasheni ni baraka kutoka kwa Mungu.
  • Mwenza mzuri atakufanya uwe mahiri kila nyanja ya maisha ikiwemo ujasiriamali.

Na Bachela Mkuu

maoni@nukta.co.tz 

Kama ni mwanaume au mwanamke uliofikia umri wa kuoa au kuolewa na haujafanya hivyo hapana shaka umshakumbana na maswali lukuki ya “utaoa au kuolewa lini?” Kama ndiyo kwanza umeingia katika umri huo, huenda ukawa unashangaa zaidi.

Lakini kwa mabachela wa kitambo hili ni swali la kawaida na tumeshalizoea kabisa. Siyo kuwa tunapenda kuulizwa hivyo la hasha. Kuoa au kuolewa siyo suala kama elimu kwamba ni lazima mtoto akifika miaka saba lazima aanze darasa la kwanza. Wala siyo chakula au maji kuwa lazima mtu ale au anywe ili aishi.

Ndoa ni baraka kutoka kwa Mungu. Ndoa ni matokeo ya uhusiano mwema wa baina ya wanaotaka kuoana. Ni msukumo wa nguvu kutoka ndani ya wapendana nao na siyo nguvu kutoka nje. Msukumo wowote wa nje huathiri uhusiano kwa kuwa siyo halisi.

Msukumo wa ndani ni pamoja na uwezo wa kujitambua kuwa sasa unafaa kuingia kwenye ndoa, kuwa na upendo thabiti na mwenza wako toka moyoni kwa kuvumilia mapungufu yake, ustahimilivu na utayari ya kuishi wawili hadi kifo kitakapowatenganisha.

Msukumo wa ndani huushinda ule wa nje ambao mara nyingi ni tamaa za ngono, kuchoka kukaa pekee yako, tamaa ya mtoto, mbwembwe za kuonekana upo kwenye ndoa, msukumo kutoka kwa marafiki na majamaa wenye maswali ya kama “utoa au kuolewa lini?” au “umeshapata mchumba?” na mengineyo.

Inawezekana kweli umri unakutupa mkono au kuna msukumo wa wewe kuingia kwenye ndoa lakini umempata mtu anayekufaa? Kati ya watu uliowahi kuwa na mahusiano nao uliwachambua ukaona yupo angalau unaendana naye kwa asilimia 50?

Haupo pekee yako

Kama bado vuta pumzi. Usijali. Haupo pekee yako. Kuna mamilioni ya watu duniani bado wanawatafuta wanaowafaa. Kuwa mvumilivu, endelea kuomba na kumtafuta anayekufaa. Fanya upembuzi yakinifu kwa unayemtafuta ili usije kutengeneza majanga.

Kumpata mtu mnayeendana angalau kwa asilimia 60 ambaye ni zaidi ya rafiki siyo kazi rahisi. Inahitaji imani, uvumilivu, nguvu ya Mungu, nia na uthubutu.

Ukikata tamaa kwa kuwa mahusiano ya awali hayakuzaa matunda huenda ukakataa tamaa pia ya maisha. Kumpata mtu wa kuishi nae maisha yote ya uhai wako ni mtihani mkubwa kuliko hata kutafuta kibarua cha kukuingizia kipato. Kibarua unaweza kuacha kisipokupa maslahi lakini mke wako wa ndoa hususan kwa wakirstu ni vigumu kumwacha.

Hivyo ni vyema kufanya yafuatayo ili kuishi bila msongo wa mawazo juu ya msukumo wa kuingia kwenye ndoa.

Zishinde nguvu za nje

Siku zote unayeoa au kuolewa ni wewe na sio hao wanaotaka kufanya hivyo. Tafuta maneno mazuri ya kuwajibu na wala usiwadharau kwa kuwa nao wanakutakia mema ndiyo maana wanakuuliza.

Utamaduni wetu ni kwamba mtu mwenye umri huo hutakiwa kuingia kwenye ndoa lakini hata hivyo mambo kwa sasa yamebadilika. Hakikisha maswali yao au msukumo hautawali akili yako kiasi cha kukupa msongo wa mawazo wakati ukimtafuta anayekufaa.

 

Ndoa ni agano la kuishi milele baina ya mume na mke mpaka kifo kitakapowatenganisha. Ni zaidi ya urafiki wa kawaida. Picha na psych2go.net.

Thubutu kutafuta anayekufaa

Kukataa tamaa kwa sababu ya kutofanikiwa katika mahusiano yaliyopita hakusaidii. Kama mwanaume endelea kutafuta unayeona anafaa na rusha ndoano yako. Komaa naye mpaka ufikie mwisho wa safari.

Kwa mwanamke vivyo hivyo jitahidi kutazama kwa makini na uchague mwanaume anayekufaa kati ya wanaume wanaokufuata. Hata kama tayari una mtoto bado una nafasi ya kumpata mume bora kwa kuwa wapo wanaume waliotayari kukuoa na mapungufu yeyote ulionayo. Na huo ndiyo upendo.

Kuwa mvumilivu

Yote hayo ya juu hayawezi kufanikiwa iwapo siyo mvumilivu. Katika harakati za kumpata ‘Mrs right’ au ‘Mr right’ lazima uthubutu na uvumilivu viende kwa pamoja.

Kwa wajasiriamali uvumilivu tunaouonyesha katika kuanzisha au kuendesha biashara zetu ndiyo tunapaswa kuunyesha wakati tunatafuta. Utakatishwa tamaa wakati wa kutongoza na inaweza kuchukua miezi au mwaka ila kama umeona anafaa pambana na hali yako hadi ufanikiwe. Siku zote vinavyosumbua kupatikana huwa ni vizuri na tulivu baadaye.

Kila mtu anapenda kuoa au kuolewa ili aishi vyema na familia yake. Lakini hakuna mtu anayependa akiingia kwenye ndoa awe analia kila siku kwa maumivu kwa kuwa hakuchagua aliyesahihi baada ya kupewa msukumo na watu wa nje.

Ndiyo nitaoa lakini msubiri nimpate anayenifaa baada ya msukumo wa ndani kunisukuma na si vinginevyo. Nitaoa muda ukifika.

Una maoni juu ya mtazamo wa Bachala Mkuu. Tupe maoni kwenye kurasa zetu za Facebook: @NuktaTanzania au Twitter: @NuktaTanzania.

Related Post