Heslb yaanika kozi zitakazopewa kipaumbele mikopo elimu ya juu 2019-2020

June 4, 2019 11:32 am · Daniel Samson
Share
Tweet
Copy Link

Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru. Picha|Mtandao.


  • Kozi zitakazopewa kipaumbele zaidi ni pamoja na ualimu wa sayansi, programu za uhandisi na sayansi ya afya.
  • Watakaosomea sayansi za msingi na sayansi ya ardhi nao hawataachwa nyuma.
  • Shahada zingine zote ambazo hazikutajwa kwenye kundi la kwanza, la pili au la tatu zitajumuishwa katika kundi la tatu.

Dar es Salaam. Ikiwa wewe ni mhitimu wa kidato cha sita na diploma unayetarajia kujiunga na chuo kikuu katika mwaka wa masomo 2019/2020, bodi ya mikopo imetangaza makundi matatu ya kozi zitakazopewa kipaumbele katika utoaji wa mikopo mwaka huu ikiwemo programu za uhandisi na ualimu wa sayansi.

Makundi hayo matatu yameanishwa katika mwongozo wa utoaji mikopo na ruzuku kwa mwaka wa masomo 2019/2020 ambao umetangazwa leo (Juni 4, 2019) na Mkurugenzi Mtendaji wa Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB), Abdul-Razaq Badru jijini Dar es Salaam.

Mwongozo huo unatoa mwelekeo na mambo ya msingi ya kuzingatia katika dirisha la maombi ya mikopo ya elimu ya juu ambalo litakuwa wazi kuanzia Juni 15, 2019 na kufungwa Agosti 15, 2019. 

Katika mwongozo huo, kundi la kwanza la wanafunzi ambao watapewa kipaumbele linajumuisha kozi za ualimu sayansi (Fizikia, Kemia na Baiolojia) na ualimu wa hisabati na masomo ya biashara na Shahada ya uzamili katika Uhandisi wa Ndege na matengenezo. 

Pia kozi za sayansi za afya ikiwemo udaktari, upasuaji meno, madawa ya mifugo, ufamasia, uuguzi na ukunga; programu za uhandisi; jiolojia ya petroli nakemia ya petroli; kilimo, misitu, sayansi ya wanyama na usimamizi wa uzalishaji yatapewa kipaumbele. 

Kundi la pili la wanafunzi ambao watanufaika na mikopo hiyo ni  wale ambao kozi zao zitajikita katika programu za msingi za sayansi ambazo zinajumuisha, “shahada ya sayansi kwa ujumla katika wanyama, mimea, kemia, fizikia, baiolojia, baiolojia ya viumbe vidogo, baiolojia ya mifugo na baioteknolojia, uvuvi na mifugo. 

Kozi nyingine zitakazopewa kipaumbele katika mwaka ujao wa masomo ni “Sayansi ya mazingira na uhifadhi, matibabu, hisabati na takwimu, sayansi ya mazingira na usimamizi, afya na mazingira, baioteknolojia na maabara, Wanyamapori na uhifadhi, na Kompyuta); Tehama, vipimo na mizani, mazingira na maendeleo ya miji.

Kundi la pili pia lina programu ya sayansi ya ardhi (Ubunifu majengo, Ubunifu mandhari nje ya majengo, usanifu ndani ya majengo, uchumi ujenzi, mipango miji na vijiji, usimamizi na uthaminishaji ardhi, jiospasho na teknolojia katika usanifu).


Zinazohusiana: 


Akianisha kundi la tatu na la mwisho la kozi, Badru amesema ni la wanafunzi wanaokusudia kusoma programu za biashara na uongozi, sayansi za jamii, sanaa, sheria, lugha, fasihi na masomo ya uandishi wa habari na mawasiliano. 

“Programu zingine zote ambazo hazijaorodheshwa katika makundi mengine zitaangukia katika kundi hili la tatu. Shahada zingine zote ambazo hazikutajwa kwenye kundi la kwanza, la pili au la tatu zitajumuishwa katika kundi la tatu,” unaeleza mwongozo huo.

Amesema zoezi la kusoma mwongozo huo linaanza leo na litadumu mpaka Juni 25, 2019, ikiwa ni hatua ya kuwapa wanafunzi muda mzuri wa kusoma na kuelewa masharti ya mkopo ili kuepuka makosa wakati wa kufanya maombi. 

Licha ya kutoa mwongozo huo, Badru amesema wanakusudia kutembelea kambi za Jeshi la Kujenga Taifa (JKT) ambazo zinapokea wahitimu wa kidato cha sita ambao wanapata mafunzo kijeshi na stadi za maisha kwa muda wa miezi mitatu. 

“Kwa hiyo utaona jitihada kubwa zinafanyika kuhakikisha wanafunzi wanaelewa na hii itasaidia kupunguza idadi ya wanafunzi waliokuwa wanafanya makosa,” ameeleza Badru.

Enable Notifications OK No thanks