Wizara ya Katiba na Sheria yaomba kuidhinishiwa Sh441.2 bilioni mwaka 2024-25

Sayuni Kisige 0853Hrs   Aprili 29, 2024 Habari
  • Yaongezeka kwa Sh57 bilioni sawa na asilimia 12.
  • Bajeti ya maendeleo yapungua kwa Sh4 bilioni.
  • Miongoni mwa vipaumbele vya wizara ni pamoja na kutayarisha Sera ya Haki Jinai na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo.


Dar es salaam. Wizara ya Katiba na Sheria imeomba Bunge la Tanzania liidhinishe jumla ya Sh441.2 bilioni kama matumizi ya wizara hiyo katika mwaka wa fedha 2024/25 ikiwa imeongezeka kwa zaidi ya Sh57 bilioni.

Waziri wa Katiba na Sheria Balozi Dk. Pindi Chana aliyekuwa akisoma bajeti ya wizara yake leo Aprili 29, 2024 bungeni jijini Dodoma amewaambia wabunge kuwa kati ya fedha inayooombwa, Sh 335 bilioni zitatumika kwa ajili ya mishahara ya kawaida na matumizi mengineyo.

“Ili kufanikisha utekelezaji wa vipaumbele vilivyoainishwa, wizara inaomba kuidhinishiwa jumla ya Sh441.2 bilioni kwa ajili ya matumizi ya kawaida na miradi ya maendeleo,” amesema Balozi Dk.Chana.

Hata hivyo, licha ya ongezeko hilo la asilimia 12 ya bajeti nzima bajeti ya miradi ya maendeleo imepungua kwa Sh4 bilioni kutoka Sh 109.6 bilioni iliyopitishwa mwaka 2023/24 hadi Sh105.6 bilioni kwa mwaka utaoanza Julai 2024.

Kwa mujibu wa bajeti ya wizara hiyo Sh45.6 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya ndani na Sh60 bilioni ni kwa ajili ya miradi ya maendeleo ya nje.

Vipaumbele 2024/25

Aidha kwa mwaka 2024/25 wizara hiyo inakusudia kutekeleza vipaumbele 27 ikiwemo kutayarisha Sera ya Haki Jinai na Mkakati wa Utekelezaji wa Sera hiyo, kuandaa na kutekeleza mkakati wa kulinda haki za binadamu na watu pamoja na  kuandaa taarifa za utekelezaji wa mikataba miwili ya haki za binadamu ambayo Serikali imeridhia.

Vipaumbele vingine ni kuratibu mfumo wa umoja wa mataifa wa haki za binadamu wa mapitio katika kipindi maalum (UPR), kutekeleza kampeni ya msaada wa kisheria ya mama Samia na kuanzisha na kuratibu madawati ya huduma za msaada wa kisheria ngazi ya kitaifa na kijamii.

“Kushughulikia maombi ya kuongezewa muda wa kufungua mashauri ya madai nje ya muda wa ukomo mahakamani, kuandaa mikataba ya kuwarejesha wahalifu watoro kwenye nchi walikofanya uhalifu, kuratibu tafsiri ya Sheria 161 kutoka lugha ya Kiingereza kwenda lugha ya Kiswahili,” amesema Balozi Dk. Chana.

Related Post