Njia za kuepuka ugonjwa wa “mchafuko wa damu”

Rodgers George 0912Hrs   Julai 06, 2021 Maoni & Uchambuzi
  • Ni pamoja na kufuata kanuni za afya ikiwemo kunawa mikono kwa maji tiririka na sabuni.
  • Pia unashauriwa kutokupuuza dalili zinazohusiana na ugonjwa huu.
  • Endapo ugonjwa huu utapuuuziwa, unaweza sababisha madhara makubwa ikiwemo figo kufeli.

Dar es Salaam. Neno “damu chafu” bila shaka siyo geni masikioni mwa watu. Wapo ambao huenda hospitali na kuambiwa kuwa damu yao imechafuka. Na hivyo kupatiwa tiba kwa ajili ya kuirudisha damu katika hali ya usafi wake.

Kitaalamu kuchafuka kwa damu ni “Sepsis” au wataalamu wengine wanaweza kuiita “blood infection” ambayo hutokea baada ya kinga ya mwili kusababisha ongezeko la kemikali kwenye damu wakati wa kupambana na maambukizi yanayoweza kusababishwa na vijimelea.

Vijimelea vya bakteria ndiyo maarufu zaidi kwa kusababisha maambukizi yanayosababisha mchafuko wa damu lakini vimelea vingine kama virusi na fangasi pia vina mchango wake.

Tovuti ya afya ya healthline imeandika kuwa, hali hiyo ni maarufu kwa watu ambao kinga yao ya mwili imedhoofu kutokana na magonjwa kama Ukimwi na saratani. Matumizi ya dawa za kulevya pamoja na dawa za kuongeza nguvu (steroids) nacho kinaweza kuwa chanzo.

Watu wengine waliowahi kuandika rekodi ya kugundulika na damu chafu ni wajawazito, wazee, watu waliofanyiwa upasuaji mkubwa na watu wenye kisukari,

Mchafuko wa damu unaweza kusababisha athari kwa figo, mapafu na ubongo. Picha| DW.


Dalili za kuwa una mchafuko wa damu

Healthline imeandika kuwa, mchafuko wa damu unaweza kutokea sehemu mbalimbali za mwili na hivyo na hutofautiana kati ya mtu mmoja hadi mwingine.

Kati ya dalili ambazo mtu anaweza kuziona ni pamoja na homa, kushuka kwa joto la mwili, kupungua kwa kiwango cha kutoa haja ndogo, kuongezeka kwa mapigo ya moyo, kuhisi kichefu chefu na kutapika.

Dalili zingine za kuangalia ni pamoja na kuharisha, uchovu wa mwili, mwili kupoteza rangi yake asilia, kutoa jasho jingi pamoja na maumivu makali ya mwili.

Endapo dalili hizi zitapuuzwa na mtaalamu wa afya hatohusishwa, mchafuko wa damu unaweza kusababishwa kufeli kwa figo, athari kwenye mapafu, moyo na ubongo na pia inaweza kusababisha baadhi ya sehemu za mwili kukatwa ikiwemo mikono na miguu.

Njia za kujikinga na mchafuko wa damu

Waswahili wanasema kinga ni bora kuliko tiba na tahadhari ni heri kuliko hospitali. Ili kujiepusha na ugonjwa huu unaoweza kuharibu bajeti yako kwa gharama za matibabu inashauriwa kuendana na kanuni za usafi.

Kauni hizo ni pamoja na kunawa mikono yako kwa maji safi tiririka na sabuni mara kwa mara na hasa kama umeshika uchafu na kupata matibabu mara unapohisi maambukizi ya ugonjwa wowote.

“Unapopata jeraha ambalo limekata ngozi yako, safisha haraka iwezekanavyo na hakikisha sehemu hiyo ni safi mara zote. Uonapo dalili yoyote ya maambukizi katika sehemu hiyo, onana na mtaalamu wa afya,” imeshauri webmd.

Related Post