Kanda ya ziwa yatikisa matokeo darasa la saba 2019

Mwandishi Wetu 0556Hrs   Oktoba 15, 2019 Habari
  • Yaingiza shule zote 10 katika orodha ya shule 10 zilizofanya vizuri kitaifa. 
  • Mwanza yaingiza shule huku Shinyanga ikiingiza shule tatu.
  • Dar es Salaam yashika nafasi ya kwanza ufaulu kimkoa.  

Baraza la Mtihani la Taifa (Necta) limetangaza matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka 2019 na kusema ufaulu umeongezeka kwa asilimia 3.78 huku shule za mikoa ya kanda ya ziwa zikitawala orodha ya 10 bora kitaifa.  

Katibu Mtendaji wa Necta, Dk Charles Msonde aliyekuwa akitangaza matokeo ya darasa la saba leo (Oktoba 15, 2019) amesema kuwa katika matokeo hayo asilimia 81.5 ya watahiniwa 933,369 waliofanya mtihani huo wamefaulu.

Amezitaja shule 10 zilizofanya vizuri katika matokeo hayo kuwa ni Graiyaki ya Mara ikifuatiwa na Twibhoki ya Mara, Kemebos ya Kagera, Little Treasures (Shinyanga) na Musabe (Mwanza). 

Nyingine ni Tulele ya mkoani Mwanza, Kwema Modern (Shinyanga), Peaceland (Mwanza), Mugini (Mwanza) na Rocken Hill ya Shinyanga. 

Kwa matokeo hayo ya mpangilio wa ufaulu kwa shule kitaifa, kanda ya ziwa ndiyo imeibuka kinara kwa kutoa shule zote zilizoingia 10 bora huku mkoa wa Mwanza ukiongoza kwa kutoa shule nne ukifuatiwa na Shinyanga ulioingiza shule tatu.

Licha ya Dar es Salaam kushika nafasi ya kwanza haijaweza kuingiza shule hata moja katika orodha ya 1o bora kitaifa. 


Zinazohusiana:


Dar es Salaam yaongoza kimkoa

Katika mpangilio wa ufaulu kimkoa, Jiji la Dar es Salaam limeshika nafasi ya kwanza likifuatiwa na Arusha, Iringa, Kagera, Katavi, Kilimanjaro, Mbeya, Simiyu, Njombe na Pwani. 

Wakati Dar es Salaam ikishika nafasi ya kwanza, Halmashauri ya Jiji la Arusha imeshika namba moja katika mpangilio wa ufaulu wa Halmashauri nchini ikifuatiwa na Ilemela, Kinondoni na Mwanza Jiji.

Halmashauri zingine ambazo zimeingia kwenye orodha hiyo ya dhahabu ni Ilala Manispaa, Moshi Manispaa, Bukoba Manispaa, Iringa Manispaa, Biharamulo na Arusha. 

Related Post