Hiki ndicho chanzo kikuu cha maumivu ya mgongo

Joshua Sultan 0352Hrs   Aprili 25, 2020 Maoni & Uchambuzi

Chanzo cha maumivu ya mgongo ni uwiano usiofaa wa misuli ya mwili ambao husababishwa na aina za kazi zinazofanywa, ukaaji mbaya, ubebaji mbaya wa vitu au ulegevu. Picha|Mtandao.


  • Watu wengi hupatwa na maumivu ya mgongo walau mara moja katika kipindi chote cha utu uzima wao.
  • Husababishwa na uwiano usiofaa wa misuli ya mwili ikiwemo aina ya ukaaji wa mtu. 

Dar es Salaam. Ni wikiendi nyingine ya kuzungumzia afya zetu. Leo tunaangazia tatizo la maumivu ya mgongo ambalo kwa sasa linawatesa watu wengi. 

Katika kazi zangu za kila siku, nimegundua kuwa maumivu ya mgongo ni moja ya tatizo linaloongoza kwa idadi kubwa ya wagonjwa kwenda hospitali kutibiwa. 

Ni dhahiri kuwa watu wengi hupatwa na maumivu ya mgongo walau mara moja katika kipindi chote cha utu uzima wao. Chanzo hasa ni nini?

Chanzo cha maumivu ya mgongo ni uwiano usiofaa wa misuli ya mwili ambao husababishwa na aina za kazi zinazofanywa, ukaaji mbaya, ubebaji mbaya wa vitu au ulegevu. 

Kwa kiwango kidogo ajali, magonjwa ama uvimbe huwa chanzo cha maumivu sugu ya mgongo. Leo nataka tuangazie chanzo kikuu ambacho ni kukosekana kwa uwiano wa misuli.

Mwili wa binadamu umejengwa na misuli ambayo imejishikiza kwenye mifupa. Misuli hii hukaza na kulegea ikizalisha nguvu inayofanya mwili wa binadamu utembee na kushughulisha maungio ya mwili.

Hivyo hivyo, eneo la mgongo lote hadi kwenye nyonga ni muunganiko wa misuli ambayo imejishikiza maeneo tofauti ikiwemo mifupa ya uti wa mgongo ambayo imezoeleka kuitwa pingili za mgongo. 

Baina ya pingili moja na nyingine kuna tishu mfano wa duara ambazo ni kama mpira uliozunguka kimiminika. Hizi huitwa diski za uti wa mgongo. Kazi yake kubwa ni kupunguza mkazo na mgandamizo baina ya pingili moja na nyingine. 

Hizi pia zinachakaa kuendana na umri na mabadiliko ya kimwili na hivyo ufanisi wa kazi yake hupungua.


Zinazohusiana:


Mgongo kitaalamu umegawanyika katika sehemu ya shingo (cervical), kifua (thoracic), kati na kiuno (lumbar) na mkia (sacral and coccygeal). Sehemu ya chini ambayo ni kiuno, pingili zake pamoja na diski huwa  ni pana na hii ni kwa sababu zinabeba uzito mkubwa katika eneo hili.

Pia mgongo haujanyooka. Una mikunjo yake ambayo kibaiomekaniki sasa husaidia kusawazisha na kuleta uwiano wa mgandamizo kutoka kichwani hadi chini na ile kutoka chini kurudi juu (ground reaction forces)

Uwiano wa mgongo pia huathiriwa na kiuno na nyonga. Ukaaji mbaya eneo la nyonga hupelekea mabadiliko ambayo huelekea moja kwa moja hadi kwenye mgongo. Mtu akikaa vibaya kwenye nyonga basi mabadiliko huja mpaka kwenye mgongo.

Hali hiyo inaweza kusababisha maumivu ya mgongo. 

Katika sehemu ya pili ya makala ijayo tutaangazia undani wa mabadiliko na namna husababisha maumivu ya mgongo.

Dk Joshua Lameck Sultan ambaye kitaaluma ni daktari wa mafunzo ya mazoezi tiba ni Mshauri katika taasisi ya Nakua na Taifa Langu (NTL) na Mkurugenzi wa Indigo Afya. Hufanya semina mbalimbali kuhusu masuala ya afya akijikita katika magonjwa yasiyoambukiza (NCD) pamoja na yale yanayoendana na mtindo maisha. Anapatikana kwa namba: +255 789 311 481, Baruapepe: joshualameck9@gmail.com.

Related Post