Wafanyakazi wengi hawajui haki zao: Ripoti

Zahara Tunda 0749Hrs   Agosti 16, 2018 Habari
  • Ripoti yapendekeza vyama vya wafanyakazi kutetea haki za wanachama wao.
  • Mikataba ya kazi iwekwe katika lugha nyepesi kuwapa wafanyakazi muda wa kuielewa.

Dar es Salaam. Imebainika kuwa wafanyakazi wengi nchini bado wanakabiliwa na changamoto ya uelewa mdogo wa haki zao wakiwa kazini jambo linalofanya baadhi kufanya kazi saa nyingi kupita kiasi na kupewa malipo duni.

Ripoti mpya ya utafiti ya Haki za Binadamu na Biashara mwaka 2017 iliyozinduliwa leo (Agosti 16, 2018) na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC) jijini Dar es Salaam inaeleza kuwa wafanyakazi wanakabiliwa na changamoto za malipo duni, kufanya kazi saa nyingi, utata wa mikataba na udhalilishaji wa kijinsia hasa kwa walemavu na wanawake.

Ripoti hiyo iliyohusisha mikoa 15 na kampuni 55  inaeleza kuwa takriban robo tatu (asilimia 74) wana mikataba ya ajira ya maandishi lakini ina lugha wasiyoilewa ikiwemo Kiingereza au haina makubaliano kati ya mwajiri na mwajiriwa. Watu zaidi ya 1,000 waliohojiwa katika utafiti huo.

"Tatizo la mikataba iliyoandaliwa bila makubaliano ya pamoja liliendelea kuwa changamoto kubwa kwa mwaka 2017. Tatizo hili lilionekana katika mikoa mbalimbali ikiwemo Iringa, Kilimanjaro, Dodoma na Njombe," inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 


       Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga (kulia) akipokea ripoti ya Utafiti wa Haki za Binadamu na Biashara mwaka 2017 kutoka kwa Mjumbe wa Bodi LHRC Felister Mahuya  (kushoto). Picha|Zahara Tunda.

Kutokana na mikataba yenye utata, wafanyakazi wamekuwa wakipewa ujira mdogo na kunyimwa malipo ya ziada na likizo ambayo ni haki zao za msingi, inasema ripoti hiyo.

"Malalamiko ya mishahara duni yalitolewa na wafanyakazi katika mikoa yote 15 iliyotembelewa hasa Mbeya, Morogoro na Tanga," inaeleza sehemu ya ripoti hiyo. 

Akiwasilisha ripoti hiyo, Afisa Msaidizi Programu wa LHRC, Tito Magoti amesema hata pale wafanyakazi wanapodai haki zao ikiwemo kuomba likizo na ongezeko la mshahara wamekuwa wakipata vitisho na kufukuzwa kazi.

“Utafiti unaonyesha wafanyakazi wengi wanahofia kuomba likizo au kudai maboresho ya mkataba kwa kuhofia kufukuzwa kazi,” amesema Magoti.  

                            Tito Magoti akielezea kuhusu utafiti wa Ripoti ya Haki za Binadamu na Biashara picha| Zahara Tunda

Licha ya wafanyakazi kutokujua haki zao, ripoti hiyo inaeleza kuwa bado mazingira wanayofanyia kazi ni ya kuridhisha isipokuwa katika baadhi ya mikoa ambayo ina changamoto ya upatikanaji wa vifaa muhimu vya kazi na jambo hilo linachochewa na ufuatiliaji mdogo wa Mamlaka ya Usalama na Afya Mahali pa Kazi (OSHA).

“Utafiti unaonyesha mikoa kama Iringa, Manyara, Mtwara, Mwanza na Njombe wafanyakazi wamedai kuwa hawalipwi fidia pindi wakiumia kazini,” amesema Magoti.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa LHRC, Anna Henga amesema uelewa mdogo wa sheria za kazi na ajira kwa wafanyakazi ndio msingi wa haki zao kukiukwa na wale ambao wanapaswa kuzitoa. 

“Wafanyakazi wengi hawana uelewa kuhusu Waraka wa Serikali kuhusu Viwango vya Mshahara wa mwaka 2013 kati ya watu 10 tuliowauliza basi watatu ndio wanauelewa kuhusu huo waraka," amesema Henga.

Ili kuhakikisha wafanyakazi wanafurahia haki zao, baadhi ya wadau waliochangia ripoti hiyo wameeleza kuwa mfumo wa sheria na mahakama nchini ueshimiwe ili kuhakikisha kila mtu anatimiza wajibu wake kuboresha maisha ya wafanyakazi.

“Vyama vya wafanyakazi vipo kisheria na vina katiba zao, tatizo wengine hawasimamii katiba zao,” amesema Thomas Sabai kutoka Chama Cha Wafanyakazi Migodini, Nishati na Ujenzi (Tamico) na kuongeza kuwa wafanyakazi watumie vyama vyao kutafuta haki zao.

Hata hivyo, bado kumekuwa na changamoto ya masuala ya unyanyasaji wa kingono katika maeneo ya kazi japo hayaripotiwi kwa kiasi kikubwa na kupelekea kutokufahamika kwa urahisi.

      Siti Ngwali kutoka Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) akichangia mjadala baada ya kutolewa ripoti ya utafiti picha| Zahara Tunda.

Akichangia mada kuhusu haki za wafanyakazi na kwa kiasi gani matukio ya kunyanyaswa hayasemwi au hayaongelewi kwa wazi, Siti Ngwali mwakilishi kutoka Mtandao wa Wanafunzi Tanzania (TSNP) ameeleza kuwa ni wajibu wa wafanyakazi kuripoti masuala hayo kwa maofisa wa ustawi wa jamii ili yaweze kufuatiliwa.

Hata hivyo, baadhi ya wadau wameeleza kuwa hatua iliyopo sasa ni kujikita kutoa elimu kwa wafanyakazi na wananchi nchini ili kuhakikisha wanajua haki zao na wanashiriki kikamilifu katika uzalishaji.

“Sisi tutajikita katika elimu kuhusu masuala ya umiliki hasa ardhi ili waweze kupata haki ya kukopa na kujiendeleza katika biashara zao, hasa kwa wanawake wanaofanya biashara katika sekta zisizo rasmi” amesema Shamira Mshangama, Mkurugenzi kutoka Shirika la Wanawake na Uongozi.

Rose Gordian kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Sayansi, Elimu na Utamaduni (Unesco) amesema ni vyema kuimarisha afya na usalama maeneo ya kazi kama haki ya mfanyakazi bila kusahau kuzingatia afya ya akili.

Related Post