Walimu wa kujitolea wanavyookoa jahazi la elimu Tanzania
- Mwalimu wa kujitolea kutoka Pangani anasema katika mazingira ya sasa vijana hawana budi kujitolea kuokoa jahazi.
- Serikali yasema itaajiri walimu 9,800 katika mwaka wa fedha wa 2021/22.
- Wabunge waitaka Serikali kuwapa kipaumbele walimu wa kujitolea wakati wa ajira.
Pangani, Tanga. Licha ya muda wa masomo kuisha, watoto watatu wakiwa na mavazi ya nyumbani wanamkimbilia baada ya kumuona akitoka ofisini.
Baada ya dakika chache za mazungumzo pembezoni mwa madarasa ya Shule ya Msingi Mwera wilayani Pangani anaongozana nao kuelekea katika makazi yake yaliyopo mita 10 hivi kutoka shuleni.
Nje ya nyumba anayoishi mwalimu Esther Ndahani (33) anaanza kuwahoji masuala kadhaa ya masomo aliyofundisha siku za nyuma kama sehemu ya mazungumzo yao.
Licha ya kutoka katika madarasa tofauti wanafunzi hao wameshajenga imani na mwalimu Esther kiasi cha kumfuata mpaka nyumbani bila woga.
Tofauti na walimu wengine 10 waliopo katika shule hiyo, Esther ana takriban miezi minne tu tangu aanze kazi ya kufundisha kwa kujitolea.
Mwokozi wa elimu Pangani
Esther ni miongoni mwa walimu watatu wanaojitolea katika shule hii ili kuchochea maendeleo ya elimu katika wilaya hii mkoani Tanga, Kaskazini mwa Tanzania.
“Nafundisha madarasa matatu hapa…darasa la tatu nafundisha soma la Uraia na Maadili, darasa IV Kiswahili na katika darasa la V nafundisha Kiswahili na Stadi za kazi,” anasema Esther ambaye alikuwa akijishughulisha na biashara ndogo ndogo za kuuza nguo kwa mkopo.
Badala ya kusubiria madeni na wateja katika shughuli zake za ujasiriamali, Esther mwenye Stashahada ya Ualimu wa awali, anasema aliona ni vema kutumia muda huo kutoa elimu katika wilaya hiyo.
“Nimeamua kujitolea kama mzazi ili niweze kuwasaidia hawa watoto… walimu waliniambia kuna upungufu wa walimu na kwamba wanahitaji usaidizi na mimi nikaamua kuja kuwasaidia,” anasema Esther ambaye amepatiwa chumba cha kukaa karibu na shule hiyo kupunguza gharama za maisha.
Esther anasema vijana wengine waliosemea ualimu hawana budi kujitolea kuokoa jahazi huku akiiomba Serikali kuajiri walimu wengi zaidi kuondoa uhaba kuboresha elimu.
Hatua ya Esther kujitolea katika shule hii yenye miaka 74 tangu kuanzishwa kwake ilikuja baada ya kupoteza kazi katika hoteli ya kitalii mkoani Mwanza kutokana na madhara ya Uviko-19.
Pamoja na kufanya shughuli zake za ujasiriamali za kuuza nguo aliona ni vema akajitolea muda na ujuzi wake katika kufundisha wanafunzi wa kata hii ya Mwera.
Soma zaidi:
- Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu
-
Chakula shuleni kinavyochochea ufaulu Tanga
- Binti wa miaka 22 anayepambana kuung’oa umaskini Kanda ya Ziwa
Walimu wa kujitolea wanavyookoa jahazi
Shule hii ina wanafunzi zaidi ya 970 lakini ina walimu 11 huku wanane wakiwa wameajiriwa na Serikali kwa mujibu wa Kaimu Mwalimu Mkuu, Omari Shehe.
Idadi hiyo ya walimu wanane waliojiriwa na Serikali, bila kujumlisha wanaojitolea inafanya, mwalimu mmoja kufundisha wastani wa wanafunzi 121, mara mbili zaidi ya kiwango kinachopendekezwa na Serikali cha mwalimu mmoja kufundisha wanafunzi wasiozidi 45.
“Kwa hili la walimu, hali ni ngumu,” anasema Shehe.
Uwepo wa walimu wa kujitolea unafanya uwiano wa mwalimu kwa mwanafunzi uwe mwalimu mmoja anafundisha watoto 88 ikiwa ni ahueni kwa wanafunzi 33 takriban darasa zima.
Hali si hali Pangani
Takwimu za Ofisi ya Rais-Tamisemi inabainisha kuwa mwaka 2021 Pangani ilikuwa na wanafunzi 12,579 katika shule za umma huku kukiwa na walimu 217 wenye sifa na wawili wasio na sifa.
Kwa takwimu hizo za Tamisemi, mwalimu mmoja anafundisha wanafunzi 57 kwa hesabu za walimu wote wakiwemo wasio na sifa kiwango ambacho bado kipo juu kidogo ya wastani wa watoto 45 kwa mwalimu mmoja kinachopendekezwa na Serikali.
Iwapo hesabu itapigwa kwa kujumuisha walimu wenye sifa pekee, mwalimu mmoja anafundisha wastani wa wanafunzi 58.
Hata hivyo, baadhi ya shule kama Mwera hali ni mbaya zaidi wakati wastani wa kitaifa wa uwiano wa mwalimu kwa wanafunzi mwaka 2021 ulikuwa mwalimu moja wanafunzi 62.
Esther Ndahani akiwasikiliza baadhi ya wanafunzi waliokuwa wamemfuta nyumbani kwake Februari 18, 2022. Esther anajitolea kufundisha wanafunzi katika Shule ya Msingi Mwera wilayani Pangani. Picha| Nuzulack Dausen.
Maisha ya kuunga unga
Esther na walimu wenzie ili kumudu gharama za maisha katika kipindi wanafundisha shuleni hapa wanategemea mwitikio wa wazazi kuchangia angalau Sh100 kwa wiki kwa mujibu wa uongozi wa Shule ya Msingi Mwera.
Kinachopatikana kwa mwezi, Shehe anasema huwagawia walimu hao na baadhi ya gharama kama za chai walimu waajiriwa hulazimika kuwachangia kidogo kusukuma maisha.
Kwa hesabu hizo, katika shule yenye wanafunzi 970 iwapo wazazi wote watachangia Sh400 kwa mwezi maana yake uongozi utakusanya Sh388,000.
Kiasi hicho iwapo kitagawiwa kwa walimu watatu wa kujitolea kwa uwiano sawa kila mmoja atapata Sh129,330 kwa mwezi. Kiwango hiki ni chini ya nusu ya kima cha chini cha mshahara kwa mwezi kwa watumishi wa Serikali cha Sh310,000.
“Hawa walimu wakujitolea wamesaidia sana kwa sababu kuna kipindi mzigo ulikuwa mkubwa sana,” anasema Mwalimu Shehe.
“Unakuta mwalimu mmoja ana vipindi 30 hadi 35 kwa wiki na bado hapo una mzigo wa daftari za kusahihisha 100 lakini baada ya ujio wa walimu hawa kama Esther tuna wastani wa vipindi 20 hadi 22 kwa wiki,” anaongeza na kubainisha kuwa kwa sasa ufaulu shuleni hapo pia umeongezeka.
Wadau wahaha kuokoa jahazi
Kushawishi vijana wenye maarifa ya kufundisha kujitolea wakati Serikali inatafuta rasilimali ili iwaajiri siku zijazo si jambo rahisi.
Baadhi ya wadau wa elimu wilayani Pangani wanasema wanachofanya ni kuwashawishi vijana au kuwaunganisha na shule zenye uhaba mkubwa wa walimu ili kuchochea upatikanaji wa elimu bora.
Bakari Kishada, Mkurugenzi wa Shirika la Pangani Coastal Paralegals Organisation (Pacopa) anasema huwaunganisha walimu wa kujitolea na shule za msingi na sekondari zilizopo wilayani hapo ili kupunguza maumivu wa ukosefu wa walimu.
“Hivi karibuni walikuja vijana waliotaka kujitolea kufundisha ilinilazimu niwapeleke kwenye moja ya shule hapa wilayani, uongozi uliona vyeti vyao lakini sasa baada ya hapo sijajua walikubalianaje,” anasema Kishada.
Tangazo:

Serikali isikwepe wajibu wake
Hata hivyo, Kishada anasema Serikali yapaswa kuwajibika kwa kuhakikisha shule zote zina walimu na miundombinu na vifaa muhimu vya kutosha kuhakikisha watoto wa Tanzania wanajifunza ipasavyo.
Kwa mara kadhaa Serikali imekuwa ikieleza kuwa itaajiri walimu lakini kasi yake huenda isitimize mahitaji siku za hivi karibuni na si walimu wote wanaojitolea hupata fursa za ajira zinapotokea.
Mei 6 mwaka huu Serikali ilisema itaajiri watumishi 9,800 wa kada za elimu katika mwaka wa fedha wa 2021/22 unaoishia Juni 30 ili kupunguza uhaba wa watumishi hao muhimu katika ukuaji wa sekta ya elimu.
Bunge laivaa Serikali walimu wa kujitolea
Kumekuwepo na msukumo mkubwa miongoni mwa wadau wa elimu na wabunge wa kuitaka Serikali kutoa kipaumbele kwa walimu na watumishi wengine wanaojitolea.
Naibu Waziri wa Ofisi ya Rais-Tamisemi Dk Festo Dugange aliliambia Bunge mapema Mei 6 kuwa Serikali hutoa kipaumbele wa ajira kwa watumishi wanaojitolea kwenye vituo vya afya na shule nchini.
“Wakurugenzi hutupa orodha ya waliojitolea kupitia halmashauri na ambao walikuwa hawajitolei nao tunawapa ‘priority’ (kipaumbele) kwa kuwa wapo waliomba kujitolea lakini hawakupata fursa hiyo,” alisema.
Hata hivyo, Naibu Spika Mussa Zungu alisema kipaumbele kinachosemwa kiuhalisi kipo kwenye maneno na wapo wanaojitolea kazi kwa miaka minne au mitano zinapofika fursa za ajira hupatiwa watu wengine.
“Hilo jambo (watumishi wanaojitolea) lizingatiwe,” Zungu aliiagiza Serikali.
Latest