Binti wa miaka 22 anayepambana kuung’oa umaskini Kanda ya Ziwa

Nuzulack Dausen 0029Hrs   Machi 03, 2022 Ripoti Maalum
  • Katika kijiji chao amekuwa mstari wa mbele kuhamasisha kilimo cha kisasa.
  • Viongozi wa vijiji wasema ni adimu kwa vijana wa sasa kujitoa kama yeye.
  • Ni miongoni mwa waraghbishi katika wilaya ya Maswa mkoani Simiyu. 

Maswa, Simiyu. Akiwa na miaka 22 tu, amekuwa ni moja ya mabinti mashuhuri kijijini kwao. 

Umashuhuri wa binti huyu si kwa sababu ya masuala ya kujinakshi mtandaoni kama baadhi ya wenzie hasa waishio mijini wanavyofanya bali kwa kazi za kuchochea maendeleo katika kijiji chao kilichopo Kusini mwa wilaya ya Maswa mkoani Simiyu. 

Pamoja na majukumu yake ya kilimo na ujasiriamali, Grace Jiduma hutenga muda kila wiki kwa ajili ya kuwahamasisha vijana wenzie na wakazi wengine wa Kijiji cha Gula kushiriki kikamilifu katika shughuli za maendeleo. 

Kilichomshawishi kufanya kazi hii, anasema, ni kuisaidia jamii yake ili iwe huru na kuweza kujisimamia yenyewe na isiwe na utegemezi. 

“Jamii yetu kwa sasa ina utegemezi fulani, kila mkisema mfanye jambo fulani kijijini utasikia kwamba tuisubiri kwanza Serikali...watu wanaona hawawezi kufanya wenyewe jambo ambalo si kweli,” anasema Grace huku akionyesha kujiamini. 

Grace pamoja ni mmoja wa wajumbe 9 wa kamati ya wananchi ambao kazi yao ni kushirikiana na wakazi wa kijiji hicho katika kuibua, kuchambua na kutekeleza au kutoa suluhu kwa matatizo yanayowakabili. 

Jambo hilo analofanya na mwenzie huitwa uraghbishi yaani kuwachochea wananchi katika kuibua vipaumbele vyao na kushiriki katika kuvichambua na kuvitekeleza ikiwa ni moja ya njia zinapigiwa upatu zaidi kwa sasa katika kuongeza uwajibikaji nchini. 

“Hadi sasa ndani ya miezi mitano tumefanikiwa kuanzisha mashamba darasa ya kilimo cha pamba kwa kila kitongoji kijijini kwetu ili wanajamii wajifunze hapo, waongeze tija na mapato ya kumudu maisha yao,” anaeleza Grace huku akibainisha maofisa ugani wamewasaidia sana kufikia mafanikio hayo. 

Grace akionesha namna walivyotumia mbinu za kisasa katika shamba darasa la pamba katika kijiji cha Gula wilayani Maswa hivi karibuni. Picha| Nuzulack Dausen.

Kujitoa kwa Grace hakuonekani tu katika kijiji chao. Mwishoni mwa Februari alifunga safari hadi Maswa mjini katika mkutano wa kufanya tathmini ya kazi ambazo wamekuwa wakizifanya kwa miezi mitano sasa. 

Mkutano huo ulikuwa umeandaliwa na asasi ya kiraia ya Kasodefo ambayo imekuwa ikijikita katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo katika halmashauri hiyo ya kanda ya ziwa kwa ushirika na wadau mbalimbali likiwemo Shirika la Twaweza Afrika Mashariki.   

Tofauti na washiriki wengine zaidi 30 hapa, Grace ana mtoto mdogo wa miezi miwili tu anayetakiwa kumhudumia mara kwa mara. 

Kwa wazazi wengi, huenda isingekuwa rahisi kutoka ndani ya nyumba yake asafiri umbali wa kilomita 42 eti tu kwa sababu ya kwenda kutathmini hatua za kimaendeleo zinazofanyika kijijini kwao. Lakini si kwa Grace. 

Wakati wote wa mkutano wa tathamini niliobahatika kushiriki, Grace alionekana mchangamfu, mdadisi na mwenye kuchangia hoja zile zilizoonekana kugusa maisha ya wengi.

Nje ya ukumbi wanaofanyia mkutano yupo mama mmoja anayemhudumia mwanaye barabara. Huyu ni Yasinta Mlaswa, Mama wa Grace. 

Mama huyo naye licha ya majukumu yake ya kilimo aliyonayo msimu huu wa masika ameamua kumuunga mkono mwanaye kile anachofanya. Katika siku za kawaida, Mlaswa huenda shamba wakati wa asubuhi, hurejea kupika mchana na kisha kwenda tena jioni. 


Soma zaidi:


Hii ina maana kuwa isingekuwa kuwa anaunga mkono shughuli za Grace katika kuhamasisha ushiriki na maendeleo kijijini kwao wakati tunakutana naye alitakiwa kuwa shamba akihudumia miche ya pamba. 

“Anajituma sana katika kukabiliana na changamoto lukuki zinazotukabili kijijini kwetu, amekuwa ni binti mzuri wa kuigwa,” anasema mama huyo mwenye miaka 52. 

Grace na kundi lao wanaelimisha wakazi kijijini kwao umuhimu wa kushiriki katika masuala ya maendeleo ikiwemo namna ya kupanda pamba kwa mstari na mbinu nyingi za kisasa ambazo zinanisaidia na mimi kwenye shughuli za kilimo. 

Mlaswa anasema kwa sasa mwanaye amekuwa mstari wa mbele katika kuhimiza matumizi ya mbinu za kisasa za kilimo cha pamba kijijini kwao kwa kushirikiana na mabwana shamba wa kata yao ya Lalago.

Hata tulipowatembelea nyumbani kwao kijijini Gula, mama huyo anaonekana kufuatilia kwa karibu na kuunga mkono kazi za binti yake jambo linalompa faraja Grace kuendelea na vita ya kuung’oa umaskini na kuongeza uwajibikaji. 

Grace anasema kuna mambo mengine wanaendelea kuyapigania ili kuboresha maisha yao kama upatikanaji wa uhakika wa huduma za afya na maji safi na salama. 

“Katika suala la maji tulikaa na wananchi wenzetu na tukakubaliana kuwa wakishamaliza kuvuna tutaanza kuchangia mradi wa maji ili na sisi tupate maji safi na salama,” anasema Grace. 

Si rahisi sana kuwavuta vijana wenye mambo mengi kufanya shughuli za kijamii zisizokuwa na malipo kama anazofanya binti huyu ambaye ana shamba la ekari mbili la pamba linalomhitaji muda wake mwingi. 

Kwa umri wake na majukumu ya kifamilia aliyonayo, Mwenyekiti wa waraghbishi wilaya ya Maswa Maduhu Jilingisila anasema Grace ameonyesha kuwa vijana ni chachu ya maendeleo Tanzania iwapo watapewa fursa na kutambua wajibu wao. 

“Hii kazi ni moyo na Grace amedhamiria kufanya bila kujali mazingira anayofanya kazi lengo likiwa ni kuisaidia jamii yake  kwa kuwabadilisha mtazamo kupitia elimu itakayoboresha maisha yao kwa kuboresha elimu bora, miundombinu na afya bora,” anasema Jilingisila. 

Grace akiwa nyumbani baada ya kumaliza shughuli za uraghbishi katika Kijiji cha Gula. Hutumia sehemu ya muda wake kujitolea kuchochea maendeleo ikiwemo kilimo na kupambania upatikanaji wa maji safi na salama.  Picha| Nuzulack Dausen.

Katika kumsaidia majukumu ya kijamii wakati anamhudumia mwanaye, Jilingisila anasema waraghbishi wengine katika kijijini hicho au vya jirani hushika majukumu hadi anaporejea katika kazi zake za uraghbishi.  

Viongozi wa kijiji anachoishi binti huyo wanasema kuwa amekuwa msaada mkubwa katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika maendeleo hasa kwenye masuala ya kilimo cha kisasa. 

Jackson Butigu, Mtendaji wa Kijiji cha Gula anasema hamasa anayotoa Grace na wana kamati wenzie imesaidia kupunguza mzigo kwa viongozi wa vijiji hasa katika kuhamasisha ushiriki wa wananchi katika shughuli za maendeleo. 

“Katika kilimo Grace na wenzie wamehamasisha sana karibu kila kitongoji na wameweka shamba darasa ambapo wananchi wa eneo lile wanashiriki kupanda shamba la mkulima mmoja ili kila mmoja ajifunze kilimo bora,” anasema Butigu. 

Pamoja na mazingira anayofanyia kazi wakati mwingine kuwa na changamoto ikiwemo mwitikio mdogo wa wananchi katika kushiriki katika maendeleo yao, Grace anasema huu ni mwanzo tu wa kazi hiyo.

“Natarajia kuendelea kufanya kazi ya uraghbishi mpaka kifo changu,” anasema huku akibainisha kuwa mume wake anamuunga mkono katika kazi hizo za kujitolea.

Related Post