Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu

Nuzulack Dausen 0041Hrs   Machi 08, 2022 Ripoti Maalum
  • Pamoja na baadhi ya vituo vya maji kuwa porini hakuna kilichoharibiwa.
  • Kila mwanakijiji hutakiwa kulipia Sh50 kwa ndoo ya lita 20 kugharamia uendeshaji.
  • Baadhi ya wakazi wasema ni “kichaa” tu anaweza kuharibu miundombinu ya maji na kurejea kwenye shida.

Maswa, Simiyu. Ili kupata maji ya kunywa na kutumia nyumbani ilimlazimu wakazi wa Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa kwenda kuteka maji usiku wa manane. 

Kwa wale ambao walikuwa wakichelewa kuamka ilikuwa ni ngumu kupata huduma hiyo muhimu kwenye maisha ya binadamu. 

“Tulikuwa tunachota mbali sana maji kulikuwa na kisima tulichokuwa tunaenda kuchota lakini ni saa nane au saa saba ya usiku. Ukichelewa huwezi kupata chochote,” anasema Neema Jilala (34), mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza. 

Hata hapo kisimani wakati huo wa usiku wa manane, kwa mujibu wa wakazi wa kijiji hiki, iliwalazimu kupanga foleni kubwa ili kuweza kuyapata kwani kila mtu alikuwa akijaribu kijinusuru na kiu. 

Katika safari ya kuyasaka maji, baadhi ya wakazi wa kijiji hiki walikuwa wakikoswa koswa na wanyama wakali kama fisi jambo lililowaogopesha wengine kutoka usiku na kuwaacha wakitaabika zaidi na kusaka huduma hiyo. 

Mwaka mmoja baadaye wakazi wa kijiji hiki wameanza kusahau shida za kuamka usiku baada ya Serikali kuwajengea mradi wa maji kijijini kwao kupitia Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (RUWASA). 

Katika kijiji hiki kilichopo mkoani Simiyu kuna vituo vya maji vitano ambavyo vimewekwa ili kufikia sehemu kubwa ya watu, licha ya kuwa kaya nyingi hapa zinaishi umbali mrefu kutoka kaya moja hadi nyingine. 

Maumivu waliyopata wanakijiji hawa yamewafanya kutunza vema miundombinu na kugharamia gharama nyingine za kuhakikisha mradi huu hauharibiki na kuwarudisha kwenye maisha ya dhiki. 

Moja ya vituo vya  maji katika Kijiji cha Mwamihanza wilayani Maswa ambacho wamekuwa wakikitumia kujipatia maji safi na salama kwa matumizi ya nyumbani. Picha| Nuzulack Dausen.

Utunzaji wa vituo hivyo vya maji, vilivyozungushiwa wavu wa waya na kuachwa wazi bila mlango, ni tofauti kidogo na maeneo mengine ambayo baadhi ya waharifu huaribu miundombinu zikiwemo koki na kuiba vifaa vingine. 

Hapa licha ya vituo vingine vya maji kuwa porini kukidhi mahitaji ya wakazi wanaokaa umbali mrefu kutoka mmoja na mwingine, hadi sasa kwa mujibu wa uongozi wa watumiaji wa maji kata ya Isulilo, hakuna kituo kilichoharibiwa. 

Ndirana Jijungu (43), mkazi wa Kijiji cha Mwamihanza anasema ni “kichaa” pekee ataharibu bomba za maji kwa kuwa wametaabika sana hadi kupata huduma hiyo ya maji safi na salama. 

“Usione kituo kipo porini lakini kinatunzwa. Kuna mtu ambaye tukitaka kuteka maji tunamwita na tunampatia Sh50 kwa ndoo ya lita 20...huyu anakaa jirani na kituo,” anasema.

Kila mkazi wa kijiji hiki ni mlinzi wa mradi huu wa maji ambao ni sehemu ya mradi mkubwa unaohudumia vijiji vitatu vya Mwamihanza, Ngongwa na Isulilo. 

“Katika ulinzi tuliitisha mkutano wa kijiji, wananchi wakaambiwa kuwa huu mradi ni kwa faida yao na siyo ya Serikali na wote lazima tuwe walinzi. Hadi sasa hakuna hata mtu aliyewahi kujitokeza kung’oa koki,” anasema Maria Laurent, Katibu wa Jumuiya ya Watumiaji wa Maji Kata ya Isulilo wilayani Maswa mkoani Simiyu. 

Katika kuhakikisha mradi haukwami iliamriwa katika mikutano ya kijiji kuwa wakazi hao wanatakiwa kuchangia kiasi cha fedha ili kupata mfuko utakaoweza kukarabati miundombinu na kuwalipa maofisa wanaosimamia mradi huo. 

Wakazi wa kijiji hiki wanaeleza kuwa hawana kinyongo kuchangia maji kwa kuwa ni wajibu wao kutunza miundombinu na rasilimali hizo ili wasirudie kwenye hali ya zamani. 


Soma zaidi:


Miaka ya nyuma Kijiji cha Mwamihanza kwa mujibu wa Wizara ya Maji kiliwaji kuwa na mradi wa maji ambao ulikufa kutokana na wananchi kushindwa kuuendesha kutokana na gharama kubwa za uendeshaji na matengenezo.

Hali hiyo ilisababisha bwawa la maji nalo lilokuwepo katika eneo hilo tangu mwaka 1970 kujaa mchanga kutokana na shughuli za kibinadamu za mifugo na kilimo na kusababisha uhaba wa maji zaidi kijijini hapo. 

Wizara ya Maji inaeleza kuwa bwawa hilo lilikuwa linahudumia wakazi wa Mwamihanza na vijiji jirani zaidi ya 1,500 na mifugo 3,578. 

Miaka miwili iliyopita wakazi wa Kijiji cha Mwamihanza walikuwa wakiona vituo hivi vya maji wanapokuwa wameenda Maswa Mjini kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali za kijamii na kiuchumi. Kuwa na kituo cha maji kama hiki kilichopo Mwamihanza Centre ilikuwa ni kama filamu. Picha|Nuzulack Dausen. 

Ili kudhibiti hali hiyo isitokee tena Serikali na wakazi wa kijiji hiki kupitia jumuiya ya watumiaji wa maji wamekubaliana kuchangia Sh50 kwa lita 20 na kufanya matengenezo mara kwa mara pale tatizo linapotokea. 

Ni wachache zaidi kama Ndirana anayetaka gharama zishushwe hadi Sh25 kwa lita 20. 

Laurent, ambaye pia ni Kaimu mhasibu wa mradi huo, anasema mwitikio wa watu kuchangia maji ni mzuri hata baada ya kupandisha mchango kutoka Sh25 kwa ndoo hadi Sh50.

“Tulipandisha kidogo gharama kwa ndoo kwa sababu gharama zilianza kuwa kubwa wakati mapato ni kidogo. 

“Mhasibu anapaswa kulipwa, fundi anatakiwa kulipwa na kuna matatizo mengine ambayo yakitokea kama kuvuja mabomba ardhini ni lazima mtengeneze haraka,” anasema Luarent na kuongeza kuwa gharama hizo ni ahueni ikilinganishwa na gharama ya kutembea kilomita tano au kuamka usiku kusaka maji. 

Laurent, ambaye alikuwa kinara wa kupigania upatikanaji wa maji safi na salama kijijini hapo, anasema utayari wa wakazi hao kuchangia maji ili kuendesha mradi umesaidia kupunguza maumivu zaidi kwa wanawake wa kijiji hicho. 

Kwa sasa tangu mradi huo uanze mapema mwaka 2021, Laurent anasema wana uwezo wa kukusanya mapato hadi wastani Sh700,000 hadi Sh900,000 kwa mwezi kutoka katika vijiji vitatu vinavyohudumiwa na mradi vya Mwamihanza, Ngongwa na Isulilo. 

Fedha hizo huwasaidia kununua vifaa kwa ajili ya matengenezo, kulipa watumishi wanaohudumia mradi wakiwemo wale wanaosimamia vituo vya maji katika kijiji chao. 

Mtandao wa maji umeanza kusambaa kijijini hapo lakini kutokana na ukata unaowakabili wakazi hao ni kaya moja tu ambayo imevuta bomba binafsi licha ya kuwa gharama za kuunganishwa huduma hiyo ni Sh30,000.

Laurent anaamini kadri vipato vinavyoongezeka na watu wanavyoona faida ya maji, wengi watavuta mabomba ya maji hadi majumbani kwao. 

Related Post