Safari ya kutokomeza uhaba wa madarasa Tanga
- Wakazi wa Wilaya ya Pangani huchangia fedha na nguvu kazi katika kupunguza uhaba wa miundombinu shuleni.
- Walimu waeleza uhaba huo unapunguza ufasini katika utoaji wa elimu bora Tanzania.
Pangani, Tanga. Katika moja ya vyumba vya Shule ya Msingi Bushiri, walimu watatu wapo ofisini wakiendelea kusahihisha kazi za wanafunzi wao.
Wanafunzi wachache hapa wanaingia na kutoka na kurundika madaftari katika meza ya kwanza baada ya kuingia mlangoni. Watoto hao waliopo shuleni, miongoni mwao ni wale wa darasa la pili na la saba wanaotarajia kuhitimu mwaka huu.
Katika kujifunza, wanafunzi hawa wanapeana zamu wengine wanaingia shule asubuhi na wengine wanaingia mchana kutokana na uhaba wa madarasa.
Nje ya ofisi ya walimu, mita chache kutoka kwenye majengo makuu ya shule hiyo kuna darasa la miti kuukuu huku baadhi ya madawati yakiwa yameanguka kutokana na kuvunjika miguu.
Si tatizo jipya
“Tatizo la madarasa linajulikana,” anasema Seleman Kichuzi, mwalimu wa Shule ya Msingi Bushiri iliyopo katika Wilaya ya Pangani mkoani Tanga.
Kichuzi anasema kwa sasa shule hiyo inahitaji madarasa mawili zaidi ili kukidhi mahitaji ya wanafunzi kwa sasa wanaoongezeka kila mwaka.
Wakati tunaitembelea Februari 16, shule hiyo ilikuwa na wanafunzi zaidi ya 400, idadi ambayo huenda imeongezeka baada ya kukamilisha usajili wa watoto wa darasa la awali na la kwanza.
“Wanafunzi wanapeana ‘shift’ (zamu). Darasa la pili wanakuja mchana ila la kwanza, la tatu hadi la saba wanakuja asubuhi. Darasa la pili wanapeana ‘shift’ na darasa la kwanza,” anasema.
Katika kuhakikisha watoto wote wanatimiza ndoto zao za kielimu, walimu wa shule hii wanaofundisha darasa la kwanza na la pili hulazimika kubaki mpaka jioni kutimiza mahitaji ya vipindi.
Darasa la awali lililopo katika Shule ya Msingi Bushiri, Wilaya ya Pangani mkoani Tanga. Wanafunzi katika shule hiyo husoma kwa kupokezana ili kukabiliana na uhaba wa madarasa. Picha| Suleman Mwiru.
Labda kesho hali itakuwa bora
Pamoja na uhaba unaowakabili sasa, Kichuzi ana matumaini huenda siku moja wanafunzi wake watakuwa wakisoma wote asubuhi bila kubanana huku mwalimu akiwa na uwezo wa kupita kutoka dawati moja kwenda jingine kama ilivyo kwenye shule zenye madarasa mengi.
“Mkuu wa wilaya alikuja kututembelea na kuona hilo darasa la awali, hili darasa halina ufanisi kwamba wanafunzi wakae wasome lakini kulingana na upungufu wa miundombinu imebidi watoto wasomee humo,” anasema Kichuzi akionyesha darasa la awali la miti lililoezekwa na mabati ambayo yameanza kuchakaa.
“Alichukua picha na alisema atafanyia kazi. Ila hatujajua kuwa itakuwa lini.”
Mwalimu Kichuzi anasema mbali na uhaba wa madarasa shule yao pia inakabiliwa na uhaba wa nyumba za walimu.
“Hii shule ni kongwe lakini tuna nyumba moja ya walimu,” anasema huku akionekana kunung’unika akibainisha kuwa baadhi ya walimu wanajibana katika nyumba hiyo iliyopo eneo la shule.
Ahueni kwa shule nyingine
Wakati Bushiri wakilia na uhaba wa madarasa, wenzao wa Shule ya Msingi Mwera iliyopo umbali wa takriban kilomita 20 wamejengewa madarasa mapya matano miaka ya hivi karibuni yakiwemo yaliyojengwa kupitia Mpango wa Lipa Kulingana na Matokeo (EP4R).
Mwalimu Omari Shehe anasema madarasa kwake yanajitosheleza kumudu mahitaji ya wanafunzi wake ambao hadi Februari 17 mwaka huu walikuwa ni zaidi ya 970.
“Kwenye suala la madarasa, sina hali mbaya kama wenzetu. Madarasa yapo yanajitosheleza,” anasema mwalimu Shehe.
Soma zaidi:
- Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu
-
Chakula shuleni kinavyochochea ufaulu Tanga
-
Vita mbichi: Wakazi wa Pangani wanavyohamasishana kupata chanjo ya Uviko-19
Shule ya Msingi Mwera ni moja ya shule kongwe mkoani Tanga ikiwa na miaka 74 tangu kuanzishwa kwake.
Wadau wa elimu wanasema watoto wanahitaji mazingira bora ya kujifunzia ili kuelewa vizuri masomo yatakayowasaidia kukabiliana na changamoto ya dunia ya sasa.
Wakazi waachana na tabia ya kusubiria Serikali
Katika maeneo mengi ya wilaya ya Pangani, wazazi wanachangia ujenzi wa madarasa ukiachana na mengine yaliyojengwa mwishoni mwa mwaka jana kupitia fedha za mkopo wa masharti nafuu wa kukabiliana na madhara ya kiuchumi ya ugonjwa wa Uviko-19 zilizotolewa na Shirika la Fedha Duniani (IMF).
Mkazi wa Kijiji cha Mkwaja Mustapha Omari anasema wakazi wa kijijini kwao huwa wanahamasishana kuchangia maendeleo ya elimu ikiwemo ujenzi wa madarasa hadi ngazi ya lenta na Serikali humalizia kazi hiyo.
Omari, anasema iwapo asipojituma kupigania maendeleo ya kijijini kwao kwa kuchangia fedha na nguvu kazi kwenye kuboresha miundombinu ya elimu ya msingi na sekondari hana uhakika iwapo viongozi wanaokaa mbali na eneo lao watakikumbuka kijiji chao.
Katika kukabiliana na uhaba huo wa madarasa, Serikali inaendelea kujenga miundombinu ya shule ikiwemo kujenga shule shikizi na kuongeza madarasa wilayani humo, anasema Mwalimu Hassan Nyange, Katibu Tawala wa Wilaya ya Pangani.
Baadhi ya madarasa yaliyopo katika Shule ya Msingi Mwera mkoani Tanga. Licha ya madarasa hayo kuchakaa, shule hiyo inakabiliwa na uhaba wa madarasa, jambo linalowafanya wanafunzi wapate usumbufu wakati wa kujifunza. Picha| Suleman Mwiru.
Fedha za Uviko-19 zaokoa jahazi
“Sasa hivi hatuna upungufu wa madarasa upande wa shule za Sekondari, tuna upungufu wa madarasa kwenye shule chache katika shule za msingi ambazo kwenye fedha za tozo zinazofuata tunakwenda kusolve hilo tatizo,” anasema Nyange.
Kwa muda mrefu Serikali imekuwa ikikosolewa vikali na wadau wa elimu kuwa haiwekezi ipasavyo katika uboreshaji wa miundombinu na walimu katika shule za msingi nchini licha ya takwimu kuonyesha idadi ya udahili wa watoto inaongezeka mwaka hadi mwaka.
Hata hivyo, mwaka jana Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ilielekeza sehemu ya mkopo kutoka IMF kujenga madarasa, mabweni na shule shikizi.
Takwimu za Ofisi ya Rais-Tamisemi zinabainisha kuwa mamlaka za Serikali za Mitaa zilipatiwa Sh304 bilioni kujenga vyumba vya madarasa 12,000 katika Shule za Sekondari, vyumba vya madarasa 3,000 katika vituo shikizi na mabweni 50 kwa ajili ya wanafunzi wenye mahitaji maalum.
“Hadi Februari, 2022 vyumba vya madarasa 11,988 kati ya vyumba 12,000 vya Shule za Sekondari vimejengwa na kukamilika sawa na asilimia 99.99,” Innocent Bashungwa, Waziri wa Ofisi ya Rais – Tamisemi alilieleza Bunge mapema mwezi uliopita.
Tangazo

Latest