Chakula shuleni kinavyochochea ufaulu Tanga
- Serikali yakiri kuwa shule zinazotoa chakula zina ufaulu mzuri kuliko zisizotoa.
- Wazazi wafurahia utulivu wanaopata watoto wao katika masomo
- Wanafunzi wataka chakula chenye lishe zaidi ukiachana na “ugali maharage”.
Pangani, Tanga. Wakati wenzao wakiumiza vichwa namna ya kupata chakula muda wa mapumziko utakapofika, wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bushiri wao wametulia darasani wakiendelea na vipindi.
Nje ya shule hiyo iliyopo wilayani Pangani hakuna wauza vyakula wanaowinda watoto wa kuwauzia kama ilivyo kwa baadhi ya shule zisizotoa chakula shuleni katika mkoa huo wa Tanga.
Ramadhan Adam, mwanafunzi wa kidato cha nne katika Shule ya Sekondari ya Bushiri anasema uwepo wa chakula shuleni kwao umemsaidia kufanya vizuri kwenye masomo kiasi cha kumpa matumaini kuwa atafanya vizuri zaidi katika mtihani wa mwisho mwaka huu.
Ahueni baada ya dhiki tele
“Nilikuwa napata tabu sana kipindi nipo madarasa ya shule ya msingi kwa kuwa nilikuwa nashinda tangu asubuhi hadi jioni bila kula,” anasema Ramadhan akionyesha ugumu wa kusoma bila chakula shuleni.
“Lakini huku hakuna athari nilizopata shule ya msingi, ‘naperform well’ (nafanya vizuri) masomo yangu na hata sisinzii tena darasani,” anaongeza.
Chakula anachokula Ramadhan na wenzie katika shule hii ni matokeo ya wazazi kujitoa kuchangia ili kusaidia watoto wao waweze kuepuka karaha za kusoma na njaa.
Utaratibu huu umezidi kushika kasi miaka ya hivi karibuni ikiwemo mwaka jana kutokana na wakazi wa wilaya ya Pangani kuhamasisha wengine kupitia waraghbishi kutatua changamoto hiyo inayoyakumba maeneo mengi Tanzania.
Watoto wengi wanaosoma shule zisizotoa chakula shuleni hujikuta dhaifu darasani kiasi cha kupunguza ufanisi wao katika kujifunza.
Ramadhan anasema alipokuwa shule ya msingi ambako hakukuwa na chakula alikuwa anapewa Sh200 kwa siku na ikishaisha asubuhi anabaki siku nzima na njaa.
Mmoja wa wapishi wa shule ya Sekondari Bushiri ya Pangani mkoani Tanga akiendelea na upishi wa chakula kwa ajili ya wanafunzi wa shule hiyo. Picha| Nuzulack Dausen.
Bila chakula ni taabani
“Mchana mwili ulikuwa unaishiwa nguvu hata mwalimu akifundisha humwelewi lakini ahueni kubwa kwa sasa ni chakula cha mchana,” anasema Ramadhan anayeishi nyumbani kwao.
Shirika la Chakula na Kilimo Ulimwenguni (FAO) linaeleza kuwa mpango wa kuwalisha chakula wanafunzi shuleni unaongeza ulinzi wa kijamii, chakula na lishe kwa wanafunzi.
Upatikanaji wa chakula shuleni umefanya watoto wa kike nao waendelee kupambania ndoto zao kwa kuwa ni moja ya makundi yenye vikwazo lukuki katika kuisaka elimu bora.
Judith Shayo (15), mwanafunzi wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Bushiri anasema uwepo wa chakula na mabweni katika shule hiyo umekuwa chachu ya kuendelea vema na masomo.
Hata hivyo, ukosefu wa chakula tofauti tofauti unafanya baadhi ya watoto kuhitaji vyakula ambavyo wanasema vitasaidia kuwapatia lishe bora na si kula pekee.
“Nyumbani kunakuwa na vyakula tofauti kuliko hapa shuleni…angalau kule kuna vyakula vingi kama tambi na ndizi,” anasema Judith.
Soma zaidi:
- Maumivu yalivyochochea wanakijiji kutunza miundombinu ya maji Simiyu
- Mikakati ya kuboresha upatikanaji wa maji Maswa
- Binti wa miaka 22 anayepambana kuung’oa umaskini Kanda ya Ziwa
Lishe zaidi yatakiwa vyakula vya shule
Shule hiyo huwapatia wanafunzi ugali maharage, ugali nyama, wali maharage na wali nyama ambacho ni kiwango cha mwisho kujitoa.
Hata hivyo, binti huyo anasema ukilinganisha na shule zisizokuwa na vyakula ni “Bora sisi kwa sababu sisi tunacho hicho hicho lakini wao hawana kabisa.”
Uongozi wa shule hiyo unasema wakati wa masika na kipindi ambacho si kikame sana huwa wana bustani ya mbogamboga ambayo husaidia wanafunzi hao kupata chakula zaidi chenye lishe kwa kuongeza mboga ya majani.
“Kuna wanajamii katika kijiji hiki wakati wa msimu wa matunda huwa wanatoa msaada wa machungwa ambayo huwa tunayachukua na kuwapatia watoto chakula chenye matunda,” anasema Mzee Mohammed, Makamu Mkuu wa Shule ya Sekondari Bushiri iliyopo pembezoni mwa barabara ya Pangani – Muheza.
Utoaji wa chakula shuleni umesaidia ufaulu wa shule hiyo kuongezeka ikilinganishwa na miaka ya nyuma ambapo haukuwa mzuri sana.
Mzee anasema katika ngazi ya kidato cha nne, ufaulu mwaka 2020 ulikuwa asilimia 82 lakini umepanda hadi kufikia asilimia 87.6 mwaka 2021. Hali hiyo inafanana na ufaulu wa kidato cha pili ambapo uliongezeka kutoka asilimia 88 mwaka 2020 hadi asilimia 91 mwaka jana.
Kila mzazi Sh15,000 kwa mwezi
Kutokana na faida hiyo baadhi ya wazazi huwakumbusha walimu pale wanaposahau kueleza masuala ya chakula wanapojiunga na shule hiyo.
“Mzazi kwa mwezi huchangia Sh15,000 kwa mwezi kwa ajili ya chakula sawa na Sh700 kwa siku. Hii ina maana Sh500 ya chakula na sh200 ya mpishi,” anasema Mohammed.
Wazazi wa wilaya hii wanafurahi kuona utoaji wa chakula shuleni unaowaongezea watoto wao muda wa kujifunza na kuwaepusha na njaa wakati wa masomo.
“Utoaji wa chakula unanifanya nijisikie fahari kwa kuwa unampunguzia tabu mtoto kutoka shule kufuata chakula nyumbani…hii inamfanya afikirie masomo tu, linanifurahisha sana,” anasema Ally Haji, Mkazi wa Kijiji cha Bushiri.
Baadhi ya wanafunzi wa Shule ya Sekondari Bushiri wakifutilia maelekezo ya mwalimu wao (hayupo pichani). Wanafunzi hao wanasema chakula kinachotolewa shuleni hapo kimewaongezea ufanisi katika masomo yao darasani. Picha|Nuzulack Dausen.
Bado wapo wazazi vichwa ngumu
Licha ya mafanikio hayo, si wazazi wote wanatoa michango hiyo ya chakula kiasi cha kuwapa mzigo zaidi walimu wa shule hiyo yenye wanafunzi 615.
Hadi sasa watoto 32 walikuwa hawajatoa chakula hadi katikati mwa Februari mwaka huu huku mwalimu huyo akielezea kuwa hali hiyo inatokana na ugumu wa kipato kwa wazazi wa watoto hao.
Kuwarahisishia maumivu hayo, anasema huwa wanawaelimisha kuwa wapambane angalau wawachangie debe la mahindi na kuachana na fedha ambazo hawawezi kumudu.
Si Bushiri tu inayotoa chakula, zipo pia baadhi ya shule za msingi ambazo angalau zinatoa uji shuleni kuwasaidia watoto kujifunza wakiwa na utulivu zikiwemo Shule za Msingi Bushiri na Shule ya Msingi Mwera.
Baadhi ya wanafunzi wanalazimika kusafiri kwa miguu au baiskeli umbali wa kilomita 24 kwenda na kurudi shuleni wakiwa na njaa.
Tangazo:
Serikali: Chakula shuleni na ufauli na mapacha
Baadhi ya wanajamii katika wilaya hii wanahamasishana kuchangia chakula shuleni kupitia uraghbishi ulioanza kushika kasi mwishoni mwa mwaka jana.
Mraghbishi katika Kijiji cha Msaraza wilayani Pangani, Asia Clemence anasema kwa sasa wanajivunia mwitikio wa wazazi kuchangia chakula shuleni na iwapo kuna changamoto wazazi, kamati ya shule na walimu hujadili namna ya kuitatua ili wanafunzi waendelee kula shule.
Serikali inasema utoaji wa chakula shuleni una manufaa katika makuzi ya mtoto na hatua za kujifunza vema masomo.
Sophia Kihedu, Mratibu wa Afya Shuleni katika Halmashauri ya Wilaya ya Pangani ameiambia Nukta Habari (www.nukta.co.tz) kuwa wanawaelimisha wazazi kuwa pamoja na uwepo wa sera ya elimu bila malipo bado wana jukumu la kuchangia chakula kwa ajili ya watoto wao.
Katika wilaya hiyo, Kihedu anasema mwitikio umekuwa mkubwa japo si wote wanaitikia ipasavyo kama ilivyo kwa Bushiri kutokana na umaskini jambo linalofanya Serikali ishirikiane na wanajamii na asasi za kiraia kuwahamasisha zaidi na kutafuta mbinu zaidi za kufanikisha mpango huo.
“Chakula na taaluma ni mapacha,” anasema Kihedu. “Shule ambazo zinatoa chakula zinafanya vizuri kwenye masomo kuliko zile ambazo hazitoi chakula licha ya kuwa huwa kuna wanafunzi wachache wenye ‘IQ’ (uwezo mkubwa wa kuelewa mambo) kubwa.”