Upimaji wa kitaifa wa darasa la pili kuanza Novemba 18, 2025
- Upimaji huo unafanyika kwa lengo la kupima na kutathmini kiwango cha umahiri wa stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu maarufu kama (KKK).
Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetoa ratiba ya upimaji wa kitaifa wa darasa la pili kwa mwaka 2025 ambapo watahiniwa wataanza upimaji Novemba 18, 2025.
Upimaji wa kitaifa wa darasa la pili ni ni mchakato wa kupima na kutathmini kiwango cha umahiri wa stadi za msingi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu maarufu kama (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la pili kote nchini.
Upimaji huo huwa na lengo la kubaini maendeleo yao ya kujifunza mapema na kutoa mrejesho kwa walimu, wazazi na watunga sera ili kuboresha ujifunzaji.
Kwa mujibu wa ratiba iliyotolewa na Necta, upimaji utaanza siku ya Jumanne ya Novemba 18, 2025 ambapo saa 2:00 mpaka saa 2:40 asubuhi watahiniwa watapimwa kwa kuandika Stadi za Msingi za Lugha ya Kiingereza (Basic Engilsh Language Skills) na baadaye kufuatiwa na mapumziko ya lisaa limoja.
Saa 3:40 mpaka saa 4:30 watahiniwa watamaliza siku yao kwa kupimwa Stadi ya Kuhesabu (Arithmetic Skills).
Upimaji utaendelea kwa siku ya Jumatano, Novemba 19, 2025 na kumalizika siku ya Alhamisi, Novemba 20, 2025 ambapo kwa mujibu wa ratiba siku zote mbili watahiniwa watapimwa Stadi ya Kusoma kwa muda wa saa tatu kuanzi saa 2:00 mpaka saa 5:00 asubuhi.
Hii si mara ya kwanza kwa wanafunzi wa darasa la pili kufanyiwa upimaji.
Necta lilianza kufanya upimaji wa stadi za Kusoma, Kuandika na Kuhesabu (KKK) kwa wanafunzi wa darasa la pili mwaka 2015.
Upimaji huo ulifanyika kwa sampuli ukizingatia kanda za kielimu na ukijumuisha sampuli ya shule zinazotumia lugha ya Kiswahili na Kiingereza kufundishia.
Kuanzia mwaka 2019 upimaji ulihusisha shule za Serikali pekee zinazotumia lugha ya Kiswahili kufundishia ambazo ziliteuliwa kwa kutumia njia ya sampuli nasibu kutoka katika kila halmashauri.
Kutokana na maboresho yaliyofanyika kwenye Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014 toleo la mwaka 2023 na mitaala iliyoboreshwa, ilisisitizwa kuimarisha upimaji na tathmini ya maendeleo ya mwanafunzi na hivyo kufanya Necta kuamua upimaji kwa wanafunzi wote kitaifa ngazi ya shule kuanza kufanyika kuanzia mwaka 2025.