Necta yatangaza tarehe mtihani kidato cha sita 2025

January 20, 2025 4:44 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Itaanza Mei 5 na kutamatika Mei 26, 2025.
  • Ni muda wa wanafunzi kufanya maandalizi ya mwisho na muhimu kuelekea mtihani.

Dar es Salaam. Baraza la Mitihani la Taifa (Necta) limetoa ratiba rasmi ya mtihani wa kidato cha sita kwa mwaka 2025, ambapo watahiniwa wataanza mitihani yao Mei 5 mwaka huu na kuhitimisha Mei 26, 2025. 

Mtihani wa kidato cha sita ni hatua muhimu katika safari ya elimu kwa wanafunzi ambao  huashiria hitimisho la elimu ya sekondari ya juu na hutoa fursa kwa watahiniwa kuingia vyuo vikuu na taasisi za elimu ya juu. 

Ratiba inabainisha mtihani utaanza Jumatatu Mei tano 2025 kwa somo la Maarifa ya Jumla yaani (General Studies) ambao utaanza saa 2:00 asubuhi hadi saa tano.

Mchana watahiniwa watafanya mitihani ya masomo ya Kiingereza (English Language 1), Kemia (Chemistry 1), na Uchumi (Economics 1).

Jumanne, tarehe Mei 6, mitihani itaendelea kwa somo la Kiswahili 1 na Hesabu ( Basic Applied Mathematics 1 ) majira ya asubuhi, huku mchana  watahiniwa wakifanya mitihani ya Historia 1, Lugha ya Kichina (Chinese Language 1), na Biolojia 1.

Siku ya Jumatano, Mei 7 asubuhi, watahiniwa watafanya Kiswahili 2, Fizikia 1, Kilimo 1, Biashara 1, na Lishe ya Binadamu (Food and Human Nutrition 1) na mchana watahiniwa watakabiliana na mitihani ya Jiografia 1, Kifaransa 1, Elimu (Education).

Alhamisi, Mei 8, mitihani itaendelea na Historia 2, huku mchana  ikiwa ni zamu ya masomo ya Kiingereza 2, Kemia 2, na Biashara 2. Na Ijumaa, tarehe 9 Mei, watahiniwa watafanya mitihani ya Jiografia 2, Uhasibu 2 (Accountancy 2), na Lishe ya Binadamu 2 majira ya asubuhi.

Mchana wa siku hiyo watafanya mitihani ya Sanaa (Fine Art 1), Lugha ya Kichina (  (Chinese Language 2), Fizikia 2, pamoja na Uchumi 2.

Wiki ya pili ya mtihani itaanza Jumatatu, Mei 12 ambapo watahiniwa watafanya mitihani ya Kifaransa 2, Kilimo 2 (Vitendo), na Lishe ya Binadamu 3 (Vitendo). Jumanne, tarehe 13 Mei, masomo ya sanaa za ufundi (Fine Art) na Kemia 3A (Vitendo) yatafanyika. 

Mitihani ya vitendo itaendelea kwa wiki nzima kwa masomo ya sayansi kama Biolojia, Kemia, Kompyuta pamoja na Fizikia na ratiba itatamatika Mei 26 kwa kufanya mtihani wa vitendo wa Kemia 3C (Vitendo).

Umuhimu wa mtihani wa kidato cha sita

Kwa watahiniwa wengi, mtihani huu si tu fursa ya kufanikisha malengo yao ya kielimu, bali pia njia ya kujenga mustakabali wao wa maisha. kwa sababu hiyo, maandalizi thabiti ni muhimu ili kuhakikisha wanafanya vizuri.

Watahiniwa wanahimizwa kuipitia kwa umakini, kupanga ratiba zao za masomo, na kuhakikisha wanazingatia vipindi vyote vya mitihani yao. 

Wataalamu wa elimu wanashauri kuanza maandalizi mapema ikiwa imesalia takribani miezi minne kwa kutumia muda wao kwa ufanisi, kufanya mazoezi ya maswali ya mtihani wa miaka ya nyuma, na kujifunza mbinu za kusimamia muda wanapofanya mitihani.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks