Kwanini ATM zinapungua Tanzania?
- Wakati ATM zinapungua idadi ya mawakala wa benki na thamani ya miamala inaongezeka.
- Haimaanishi kwamba huduma za kibenki zinapungua bali ni mabadiliko jinsi sekta hiyo inamfikia mteja.
Dar es Salaam. Huenda leo ukipita mtaani usione tena ATM ambayo miaka michache iliyopita ilikuwa sehemu ya kawaida ya huduma na uliwahi kuitumia kutoa fedha.
Badala yake vibao vya wakala wa benki kwenye maduka ya rejareja, vibanda na biashara ndogo karibu kila kona ya miji na hata vijijini vimekuwa sehemu ya kawaida ya maisha ya kila siku ya Mtanzania.
Hii si bahati mbaya na wala haimaanishi kwamba matumizi ya huduma za kibenki yamepungua bali ni mabadiliko makubwa yanayoendelea ndani ya sekta ya benki nchini Tanzania.
Ripoti ya mwaka 2025 ya Usimamizi wa Sekta ya Benki inayotolewa na Benki Kuu ya Tanzania (BoT) inaonyesha kuwa idadi ya mashine za kutolea fedha (ATM) imeendelea kushuka kwa mwaka wa pili mfululizo.
Takwimu zinaonyesha ATM zilipungua kutoka 2,209 mwaka 2023 hadi 2,174 mwaka 2024, kabla ya kushuka zaidi hadi 1,981 mwaka 2025, ikiwa ni upungufu wa ATM 228 ndani ya miaka miwili, sawa na zaidi ya asilimia 10.
Hata hivyo, wakati idadi ya ATM iikipungua upande wa pili wa sarafu unanyesha sura tofauti.
Katika kipindi hicho, idadi ya mawakala wa benki iliongezeka kwa asilimia 29.1, kutoka 145,430 mwaka 2024 hadi 187,692 mwaka 2025.
Wakati huo huo, idadi ya miamala ya kuweka fedha iliongezeka kwa asilimia 7.9 na kufikia miamala 113,493,467, huku miamala ya kutoa fedha ikiongezeka kwa asilimia 13.8 na kufikia miamala 68,604,105, jambo linaloonyesha kwamba wananchi wanaendelea kutumia huduma hizo kwa kiwango kikubwa.
‘Benki zinapunguza gharama, si huduma’
Kwa mtazamo wa kawaida, ATM inaweza kuonekana kama huduma rahisi kwa mteja lakini kwa benki, ATM ni moja ya miundombinu yenye gharama kubwa zaidi kuiendesha.
Mtaalamu wa uchumi na fedha kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM) Profesa Abel Kinyondo anaeleza kuwa kila ATM inahitaji uwekezaji mkubwa tangu mwanzo inaponunuliwa.
Profesa Kinyondo ameiambia Nukta Habari kuwa mbali na gharama ya kununua mashine, benki hulazimika kulipia eneo la kuiweka, umeme, huduma ya intaneti inayofanya kazi saa 24, ulinzi, matengenezo ya mara kwa mara pamoja na usafirishaji wa fedha kila mashine inapomaliza fedha.
“Kila ATM ni kama tawi dogo lisilo na wafanyakazi, lakini bado linahitaji gharama nyingi ili liendelee kufanya kazi kila siku,” anaeleza Profesa.
Anasema tofauti na ATM, wakala tayari anakuwa na mtaji wake, duka lake, eneo lake la biashara pamoja na baadhi ya miundombinu muhimu jambo linalozifanya benki kutoingia gharama kubwa kuanzisha kituo kipya cha huduma.
Kwa lugha rahisi ni kwamba wakala anasaidia benki kupunguza gharama za uendeshaji wakati akiendelea kutoa huduma zilezile kwa wateja.
Benki zinatafuta faida zaidi
Mabadiliko ya mabenki kuhama kutoka kwenye utoaji huduma kupitia ATM kwenda kwa mawakala yanakuja wakati ambapo benki zinaendelea kuboresha ufanisi wa matumizi.
Ripoti ya BoT inaonyesha sekta ya benki iliendelea kuongeza faida na kufikia faida ya Sh 2.23 trilioni mwaka 2025 huku uwiano wa gharama dhidi ya mapato ukishuka kwa asilimia 47.1 kutoka asilimia 48.2 mwaka uliopita ishara kwamba benki zimekuwa zikitumia gharama ndogo kuzalisha mapato zaidi.
Kwa wachambuzi wa uchumi, kupunguza ATM ni sehemu ya mkakati mpana wa kuboresha ufanisi wa biashara za benki.
Badala ya kutumia mamilioni ya shilingi kuendesha ATM moja, benki zinaweza kutumia mtandao wa mawakala ambao unawafikia wateja wengi zaidi kwa gharama ndogo.
Tanzania inaingia kwenye uchumi wa kidigitali
Kupungua kwa ATM pia kunaakisi mabadiliko ya tabia za Watanzania ambapo kwa miaka 10 iliyopita ATM na matawi ya benki zilikuwa kama njia kuu ya kufanya miamala.
Lakini leo hali imebadilika ambapo Watanzania wengi wamekuwa wakitumia njia za kidigitali kama vile programu tumizi za mitandao ya simu na mabenki kufanya miamala.
Malipo ya bili kama vile maji na umeme, ada za shule, manunuzi madukani, huduma za Serikali, tiketi za usafiri, malipo ya biashara na hata kutuma fedha vinafanyika kupitia simu za mkononi au programu za benki.

BoT inaeleza kuwa huduma za benki sasa zinatolewa kupitia mchanganyiko wa matawi, mawakala na majukwaa ya kidigitali, hatua ambayo imeongeza ujumuishi wa kifedha na kuwafikia wananchi ambao zamani walikuwa hawafikiwi kirahisi na huduma za benki.
Kwa maneno mengine, benki haziondoi huduma bali zinabadilisha mahali na namna huduma zinavyopatikana jambo linalochochea ukuaji wa uchumi hususan katika wakati huu ambao Tanzania inalenga kufikia uchumi wa Dola za Marekani trilioni moja unaoendeshwa na teknolojia ikifikapo 2050.
ATM zinaondoka, huduma zinawafuata wananchi
Faida kubwa ya mfumo wa mawakala ni kwamba hauhitaji mteja kwenda benki. Badala yake, benki ndiyo inamfuata mteja.
Frida John, mkazi wa kijiji cha Mloganzila, anasema kwa sasa hana haja ya kutumia zaidi ya Sh3,000 kufuata mahali ATM ilipo na badala yake anaweza kutoa pesa kwa wakala bila kuingia gharama alizokuwa anaingia awali.
Kwa Frida, kuongezeka kwa mawakala wa benki karibu na makazi yake si tu kumemwondolea gharama za usafiri, bali pia kumemwokoa muda na kurahisisha upatikanaji wa huduma za kifedha kila anapozihitaji.
“Zamani ilikuwa mpaka nipande bodaboda niende wilayani, lakini saizi sina haja tena maana nikienda kibandani natoa, naweka, nalipa ada, sina shida,” Frida ameiambia Nukta Habari
Lakini bado ATM hazitapotea
Licha ya kupungua kwake, uchambuzi wa Nukta Habari umebaini kuwa bado ATM zina nafasi muhimu katika mfumo wa fedha.
Wateja wanaohitaji kutoa fedha nyingi kwa wakati mmoja, kutumia kadi za kimataifa au kufanya baadhi ya huduma maalumu bado wataendelea kuzitegemea.
Kwa mantiki hiyo, ATM zinaweza kuendelea kuwepo katika maeneo yenye matumizi makubwa kama vile vituo vya biashara, viwanja vya ndege, masoko makubwa na maeneo ya mijini, huku sehemu kubwa ya huduma za kila siku zikihamia kwa mawakala na majukwaa ya kidigitali.
Maana yake kwa Mtanzania wa kawaida
Kwa Mtanzania wa kawaida, kupungua kwa ATM hakumaanishi huduma za benki zimepungua, kinyume chake, kunamaanisha huduma zimehamia mahali alipo mteja.
Mtu anayehitaji kutoa au kuweka fedha leo ana nafasi kubwa zaidi ya kupata wakala karibu na nyumbani, sokoni au kwenye duka la jirani kuliko kutafuta ATM.
Na kadri uchumi wa kidigitali unavyoendelea kukua, simu za mkononi, mawakala wa benki na huduma za kidigitali zinaonekana kuwa nguzo mpya za sekta ya fedha nchini.
Kwa hiyo, kinachoonekana kama kupungua kwa ATM si dalili ya kudhoofika kwa sekta ya benki, bali ni ishara kwamba benki za Tanzania zinabadilisha modeli ya biashara kutoka kwenye uwekezaji mkubwa wa miundombinu kuelekea huduma zinazogharimu kidogo, zinapatikana karibu zaidi na wananchi na zinazokwenda sambamba na kasi ya uchumi wa kidigitali.