Watahiniwa milioni 1.2 darasa la saba 2024 kikaangoni kesho

September 10, 2024 3:56 pm · Esau Ng'umbi
Share
Tweet
Copy Link
  • Kufanya mitihani yao kwa siku mbili Septemba 11-12, 2024.
  • Watahiniwa waonywa kujiepusha na udanganyifu.

Dar es Salaam. Watahiniwa milioni 1.2 wa Tanzania Bara wanatarajia kuanza mtihani wa kumaliza elimu ya msingi waliyoianza miaka saba iliyopita huku wakionywa kuepuka udanganyifu. 

Baraza la Mitihani Tanzania (Necta) limesema mitihani ya kuhitimu elimu ya msingi (Primary School Leaving Examination PSLE) itafanyika kwa siku mbili kati ya Septemba 11 na 12, 2024.

Katibu Mtendaji wa Necta Dk Said Ally Mohamed amesema kati ya watahiniwa hao, 666,604 sawa na asilimia 54 ya waliosajiliwa ni wasichana.

“Watahiniwa 1,158,862 sawa na asilimia 94 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiswahili na watahiniwa 71,918 watafanya mtihani kwa lugha ya Kiingereza ambayo wamekuwa wakiitumia katika kujifunzia,” amesema Dk Mohamed katika mkutano na wanahabari leo Septemba 12, 2023. 

Dk Mohamed amesema kuwa watahiniwa wenye mahitaji maalum waliosajiliwa kufanya mtihani huo ni 4,583, ambapo kati yao 98 ni wasioona, 1,402 wenye uoni hafifu, 1,167 wenye uziwi, 486 ni wenye ulemavu wa akili na 1,530 ni wenye ulemavu wa viungo.

Watahiniwa hao watafanya mtihani huo katika masomo sita ambayo ni Kiswahili, Kiingereza, Sayansi na Teknolojia (Science and Technology), Hisabati (Mathematics), Maarifa ya Jamii na Stadi za Kazi (Social Studies and Vocational Skills) pamoja na Uraia na Maadili (Civics).

Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ni muhimu kwa wanafunzi kwa kuwa hupima maarifa na umahiri wa wanafunzi kwa yale waliyosoma katika ngazi hiyo. Pia ni daraja muhimu la kujiunga na elimu ya sekondari.

Weledi uzingatiwe

Aidha, Necta imewataka wasimamizi wa mtihani huo kuhakikisha wanatimiza majukumu yao kwa kuzingatia umakini, weledi na miongozo iliyowekwa ili kila mtahiniwa kupata matokeo anayostahili.

“Wasimamizi wahakikishe watahiniwa wote wanafanya mtihani katika muda uliopangwa, na katika hali ya utulivu. Aidha, wahakikishe watahiniwa wenye mahitaji maalum wanafanya mitihani yao ipasavyo ili wapate haki yao ya msingi, haki hizo ni pamoja na kuwapa mitihani ya nukta nundu kwa watahiniwa wasioona na maandishi yaliyokuzwa kwa watahiniwa wenye uoni hafifu,” amesisitiza Dk Mohamed.

Aidha, Necta imewataka wasimamizi kuwaongezea muda wa dakika 20 kwa kila saa kwa somo la Hisabati na dakika 10 kwa kila saa kwa masomo mengine kwa watahiniwa wenye mahitaji maalum.

Hata hivyo, jamii imetakiwa kutoa ushirikiano wa kutosha kwa kuheshimu na kuhakikisha utulivu katika maeneo yote ambayo mitihani itafanyika huku wanafunzi wakitakiwa kuepuka vitendo vya udanganyifu kwa kuwa vinaweza kusababisha wao kufutiwa matokeo yao yote.

Mwaka 2023 watahiniwa 31 wa shule ya msingi walifutiwa matokeo yao huku shule mbili zikifungiwa kuwa vituo vya mitihani kutokana na kubainika kufanya vitendo vya udanganyifu.

Adhabu hiyo ni kwa mujibu wa Kifungu 30(2)b cha Kanuni za Mitihani za mwaka 2016 kikisomwa pamoja na kifungu cha 5(2)(i) na (j) cha sheria za Necta sura ya 107.

Hata hivyo, idadi ya waliofutiwa matokeo mwaka 2023, ilipungua kutoka ile ya Mwaka 2022, ambapo Necta ilifuta matokeo ya watahiniwa 2,194 waliobainika kufanya vitendo vya udanganyifu.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks