Sababu, bei ya dizeli ikishuka, petroli ikiongezeka kiduchu Februari

February 4, 2026 11:40 am · Fatuma Hussein
Share
Tweet
Copy Link
  • Bei kuagiza mafuta ya petroli kupitia Bandari ya Dar es Salaam imeongezeka kwa asilimia 1.88.

Dar es Salaam. Mwezi Februari umeanza kwa ahueni na maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto mara baada ya bei ya dizeli kushuka huku petroli ikipaa ikichangiwa na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa mafuta.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Februari 4, 2026 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imepaa kwa Sh10 na  dizeli imeshuka kwa Sh25.

Kwa kiwango hicho, bei ya lita moja ya petroli inayotumika kwa mwezi Februari ni Sh2,788 ikiongezeka kutoka Sh2,778 iliyotumia Januari na dizeli inauzwa kwa Sh2,701 kulinganisha na Sh2,726 iliyokuwa ikitumika katika mwezi uliopita.

Kwa mujibu wa Ewura, bei ya dizeli imepungua kwa mwezi Februari kutokana na kupungua kwa gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la Uarabuni.

“Katika bei kikomo kwa Februari 2026, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 6.41 kwa mafuta ya petroli, asilimia 0.50 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 1.70 kwa mafuta ya taa.” imesema taarifa ya Ewura.

Aidha, Ewura imefafanua kuwa gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es salaam zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 1.88 kwa mafuta ya petroli, asilimia 1.65 kwa mafuta ya taa na kupungua kwa wastani wa asilimia 5.10 kwa mafuta ya dizeli.

Katika bandari ya Tanga zimepungua kwa asilimia 1.62 kwa petroli na dizeli na katika bandari ya Mtwara zimepungua kwa asilimia 9.24 kwa mafuta ya petroli na hakuna mabadiliko kwenye mafuta ya dizeli.

Kwa upande wa mafuta yanayoingia kwa bandari ya Tanga Petroli inauzwa kwa 2,849, dizeli Sh2,762 na mafuta Sh2,807.

Kyerwa maumivu zaidi

Pamoja na ahueni, wilaya ya Kyerwa mkoani Kagera ndiyo inayonunua mafuta hayo kwa bei ya juu zaidi mwezi Februari kulinganisha mikoa mingine nchini ambapo lita moja ya Petroli inauzwa kwa Sh3,061 kutoka Sh3,050 iliyorekodiwa mwezi Januari huku dizeli ikiuzwa kwa Sh2,974 kutoka Sh2,998.

Bei hiyo inayotumika ni wastani wa Sh273 zaidi ya bei inayotumiwa na wakazi wa jiji la Dar es Salaam.

Wakati wakazi wa wilaya hiyo mkoani Kagera wakiugulia maumivu ya kununua mafuta hayo kwa bei ya juu, Ewura inabainisha kuwa mkoa wa Dar es Salaam ndiyo unaonunua mafuta hayo kwa bei ndogo zaidi kulinganisha mikoa mingine. 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Follow Us on TikTok

Subscribe to Our YouTube Channel

Subscribe

Loading videos...

Loading videos...

Loading videos...

Enable Notifications OK No thanks