Maumivu bei ya petroli, dizeli ikipanda Tanzania
- Bei ya bidhaa hiyo imeongezeka kwa mafuta yote yanayoingia kupitia bandari zote za Dar es salaam, Tanga na Mtwara.
- Ewura yasema mabadiliko ya bei katika soko la dunia, kupanda kwa gharama za usafirishaji kumechangia bei za mafuta kupaa.
Dar es Salaam. Huenda wamiliki wa vyombo vya moto wakatoboa zaidi mifuko yao baada ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura) kutangaza ongezeko la bei za mafuta kwa mwezi Machi 2026.
Taarifa iliyotolewa na Ewura leo Machi 4, 2026 inaeleza kuwa bei ya bidhaa hiyo imeongezeka kwa mafuta yote yanayoingia kupitia bandari zote za Dar es salaam, Tanga na Mtwara.
Bei ya rejareja ya petroli jijini Dar es Salaam imeongezeka kwa Sh76 hadi kufikia Sh2,864 kwa lita kutoka Sh2,788 iliyorekodiwa Februari mwaka huu.
Mafuta ya dizeli imeongezeka kwa Sh157 na itauzwa kwa Sh2,858 kwa lita kutoka Sh2,701 iliyotumika mwezi Februari huku mafuta ya taa yakiuzwa kwa Sh2,932 kutoka Sh2,746 ya mwezi uliopita.
Ongezeko la bei limeshuhudiwa kwa mafuta yanayopitia katika Bandari ya Tanga ambapo petroli imepanda hadi ShSh2,925 kutoka Sh2,849 ya mwezi Februari.
Dizeli itauzwa kwa Sh2,919 kwa lita baada ya kuongezeka kwa Sh157 kutoka Sh2,762 huku mafuta ya taa yakipanda kutoka Sh2,807 hadi Sh2,993 kwa lita.
Hali kama hiyo imeshuhudiwa pia katika Bandari ya Mtwara. Bei ya petroli imepanda na kufukia Sh2,956 kutoka Sh2,881 kwa lita huku dizeli ikiuzwa Sh2,951 kutoka Sh2,794.
Mafuta ya taa yanayopitia katika bandari hiyo, sasa yanauzwa kwa Sh3,025 baada ya kuongezeka kwa Sh187 kutoka Sh2,838.
Bei hizo mpya zimeanza kutumika leo Machi 3 katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.
Ewura yaeleza sababu kupanda bei ya mafuta
Ewura imeeleza kuwa mabadiliko hayo yamechangiwa na mwenendo wa bei za mafuta katika soko la dunia. Machi 2026 bei zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa petroli, dizeli (asilimia 9.8) na asilimia 7.4 kwa mafuta ya taa.
“Kwa bei za mwezi Machi 2026, wastani wa gharama za kubadilisha fedha za kigeni (Applicable Exchange Rate) umeongezeka kwa asilimia 8.54,” imeeleza taarifa hiyo.
Pia gharama za uagizaji wa mafuta zimechangia bei kupanda. Ewura imesema katika Bandari ya Dar es Salaam gharama zimeongezeka kwa wastani wa asilimia 0.07 kwa petroli na asilimia 10.76 kwa dizeli, huku gharama za mafuta ya taa zikipungua kwa asilimia 5.41.
“Katika bandari ya Tanga hakuna mabadiliko,” imefafanua taarifa ya Ewura.
Vita Mashariki ya Kati yatajwa
Tangazo la kupanda kwa bei ya mafuta kutoka Ewura linakuja ikiwa ni siku moja tu tangu Rais Samia Suluhu Hassan kutoa tahadhari juu ya kupanda kwa bei ya nishati hiyo kufuatia vita vinavyoendelea Mashariki ya Kati.
Rais Samia aliyekuwa akizungumza Machi 3, 2026 wakati wa hafla ya uwekaji jiwe la msingi la ujenzi wa matanki 15 ya kuhifadhia mafuta katika Bandari ya Dar es Salaam alisema kuwa misukosuko inayoendelea imeanza kuathiri bei za mafuta na huenda ikaendelea kusababisha ongezeko zaidi siku zijazo.
“Kama tunavyoona misukosuko iliyotokea wiki iliyopita na tunayoendelea nayo, tayari imeshapandisha bei ya mafuta kwa asilimia 13 mpaka jana sasa hatujui leo na siku zinazokwenda,” alitahadharisha Rais Samia.
Hata hivyo, Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo aliiambia Nukta Habari kuwa ongezeko la bei ya mafuta katika soko la kimataifa linalotokana na vita kati ya Iran, Israel na Marekani haliwezi kuiathiri Tanzania mara moja, isipokuwa kama vita hivyo vitadumu kwa muda mrefu.
“Tanzania tunanunua mafuta ya kututosha kwa kipindi cha miezi mitatu, hivyo ongezeko la bei katika soko la kimataifa haliwezi kutuathiri mara tu baada ya bei kupanda kwenye soko la kimataifa,” amesema Prof Kinyondo.
Prof Kinyondo amefafanua kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunaweza kusababisha mfumuko wa bei ya bidhaa zingine kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji unaoendeshwa na nishati hiyo.
Ewura imewataka wauzaji wa mafuta kuzingatia bei kikomo zilizotangazwa na kutoa stakabadhi za mauzo kupitia mashine za kielektroniki za kutoa risiti kwenye pampu za mafuta, ikitoa tahadhari kuwa hatua za kisheria zitachukuliwa dhidi ya watakaokiuka maelekezo hayo.
Latest