Mwaka mpya waanza na maumivu bei ya petroli ikipaa kwa Sh29
- Uchambuzi wa Nukta Habari wabaini kupanda na kushuka kwa bei ya mafuta mwanzo wa mwaka.
Dar es Salaam. Mwaka mpya 2026 umeanza na maumivu kwa watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania baada ya bei ya petroli kupaa huku dizeli ikishuka kiduchu.
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Januari 7, 2025 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imepaa kwa Sh29.
Kwa kiwango hicho, watumiaji wa mafuta kupitia bandari ya Dar es Salaam watanunua lita moja ya petroli kwa Sh2,778, kupitia bandari ya Tanga Sh2,839 na kupitia bandari ya Mtwara Sh2,870.
Kwa upande wa bei ya dizeli imeshuka kwa Sh53 mwezi Januari 2026, ukilinganisha na bei iliyorekodiwa Desemba 3, 2025 ya Sh2,779.
Kwa mujibu wa Ewura bei ya dizeli imepungua kwa mwezi Januari kutokana na kupungua kwa gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la Uarabuni.
“Katika bei kikomo kwa Januari 2026, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 4.26 kwa mafuta ya petroli, kwa asilimia 12.83 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 10.44 kwa mafuta ya taa” imesema taarifa ya Ewura.
Aidha, Ewura imefafanua kuwa gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 1.1 kwa mafuta ya petroli, asilimia 4.0 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa.
Bei ya mafuta yapanda na kushuka mwanzo wa mwaka
Uchambuzi uliofanywa na Nukta Habari umebaini kuwa bei ya mafuta nchini Tanzania imekuwa ikishuka kwa viwango tofauti katika kila mwanzo wa mwaka ndani ya miaka miwili iliyopita ikitoa ahueni kwa watumiaji.
Mathalani Januari mwaka 2025 bei ya dizeli ilishuka kwa Sh135 kutoka Sh2,779 iliyokuwa ikitumika Desemba 2024 hadi Sh2,644 katika mwanzo huo wa mwaka.
Kadhalika bei ya petroli Januari 2025 ilishuka kwa Sh103 kutoka bei ya Sh2,898 iliyokuwa ikuitumika kununua kila lita moja ya petroli hadi Sh2,793.
Hali hiyo ilijitokeza tena mwanzoni mwa mwaka 2024 ambapo petroli ilishuka kwa Sh189 na petroli kwa Sh299 huku mwaka 2023 bei ikipungua Sh187 kwa petroli na Sh284 kwa kila lita ya dizeli.
Latest