Matapeli wanavyopora mamilioni ya Watanzania mtandaoni – 2
- Leo katika sehemu hii ya pili tunaendelea kubainisha akaunti na mbinu zinazotumika kutapeli watu wanaotaka kununua bidhaa mtandaoni.
Dar es Salaam, Arusha, Mwanza. Katika uchunguzi wetu tulibaini pia uwepo wa akaunti nyingine ya Instagram yenye namba ya utambulisho (Instagram User ID) 479135418 inayotapeli watu na kubadili majina kila baada ya muda mfupi huku wakati mwingine akitumia majina yanayofanana na wafanyabiashara halali kuhadaa wateja.
Kuna wakati akaunti hiyo inatumia jina la home essential store linalofanana kidogo na lile mfanyabiashara halali ajulikanaye Instagram kama home_essentialstz na kufanya uwepo wa akaunti mbili zinazofanana kidogo.
Ili kubaini ukweli, tulinunua bidhaa kutoka kwenye akaunti zote mbili kwa nyakati tofauti ndani ya wiki moja. Mmoja ya waandishi wetu akiwa Dar es Salaam Novemba 13, 2025 aliagiza mashine ya kunyonyoa manyoya ya kuku kwa Sh45,000 kupitia akaunti yenye jina la home essential store. Aliambiwa na mhusika alipie fedha kupitia namba ya simu +255 765 553 847 iliyokuwa na jina la Aisha Omari Yahaya.

Baadhi ya wafanyabishara halali wakilalamikia wimbi la matapeli wanaoiga majina ya akaunti zao kutapeli Watanzania.
Wafunga ‘comments’
Kama ilivyokuwa kwa Neema, baada ya kupokea fedha tu mtu huyo alikata mawasiliano na mwandishi wetu kwa simu, WhatsApp na kwenye akaunti ya Instagram.
Tofauti na taratibu za biashara mtandaoni zinazohamasisha mrejesho wa wateja kupitia maoni, akaunti hiyo imefunga ‘comments’ (sehemu ya kutuma maoni) ili wateja au wafuasi wake wasiandike chochote.
Mwandishi wetu alinunua pia mzigo kwenye akaunti nyingine yenye jina la home_essentialstz ambayo ilileta mzigo mpaka aneo husika na kutoa risiti na kuthibitisha kuwa hiyo ndiyo akaunti halali.
Akaunti feki yenye jina la home essential store tuliyokuwa tukiichunguza awali ilitutapeli na baada ya wiki mbili ilibadili jina na kuwa “HOME_KITCHEN_DAR”.

Kufunga ‘comment’ ni miongoni mwa mbinu maarufu inayotumiwa na matapeli ili kukwepa kufikiwa na waliowatapeli.
Akaunti hiyo inayotapeli watu ilijiunga Instagram mwaka 2013 na mhusika amebadili jina la akaunti yake mara 19. Uchunguzi zaidi umekuwa akibadilisha jina kwa wastani kila baada ya muda fulani akitunga jina jipya au kurejerea yale ya zamani aliyowahi kutumia ili kuwachanganya zaidi wateja aliowatapeli.
Mpaka makala hii inaenda hewani alikuwa akitumia jina la home_store_stores ingawa aliwahi kutumia jina, home essential store, home storetz, na HOME_KITCHEN_DAR.
Ili kuwaaminisha watu katika baadhi ya machapisho anaweka vyombo na sura za watu ambao hawahusiani kabisa na biashara yake.
Kwa kutumia zana ya kidigitali ya Google ya kutafuta na kudhibitisha picha (Google Reserve Image Search), tulitafuta watu hao kwa kutumia picha walizoweka katika kurasa zao za mitandao ya kijamii na tukabaini kuwa ni za watu wengine. Pia baadhi ya picha siyo halisi zimetengenezwa na akili bandia.

Baada ya kufanya utapeli baadhi ya wafanyabishara hufuta taarifa zote katika akaunti zao au huzuia watu wengine wasione maudhui ili kuzuia aliowatapeli wasimfikie. Huu ni ukurasa wa Jumba la Pochi ambao kwa sasa hauna maudhui yeyote au yameuziwa kuonekana.
Hujibadili kama kinyonga
Sambamba na kubadili majina, wafanyabiashara hao hufuta machapisho yao katika mitandao ya kijamii, hubadili namba za simu baada ya kutapeli watu wengi huku zile za awali zikifungwa kupokea simu za kawaida. Mawasiliano ya mitandao kama Whatsapp nayo huyazuia kupokea simu na meseji.
Mfano, akaunti ya Instagram inayojulikana kama Jumba la Pochi aliyetutapeli pochi yenye thamani ya Sh60,000 kwa sasa amefuta taarifa zake zote kwenye akaunti hiyo na amewazuia wote aliowatapeli wasimfikie ili kufuta ushahidi.
“Hakuna utapeli kipenzi ni kijana amechelewa,” alieleza mfanyabiashara wa Jumba la Pochi kupitia ujumbe wa WhatsApp wakati akimjibu mwandishi wetu aliyekuwa akifuatilia bidhaa alizonunua kupitia mtandao wa Whatsapp baada ya kuchelewa kufikishiwa bidhaa aliyoagiza.
Tofauti na wengi, akaunti ya Jumba la Pochi haijabadili jina tangu ilipojiunga mwaka 2021. Namba ya simu aliyoiweka haipatikani na ukimpigia kupitia WhatsApp hapokei simu zaidi ya kukueleza utume meseji. Hadi Desemba 31, 2025 hakuna mzigo uliokuwa umetumwa na hakukuwa mawasiliano yeyote juu ya hatma ya fedha iliyochukuliwa.
Kama ilivyo kwa akaunti nyingine, katika uchunguzi wetu pia tulibaini akaunti yenye jina la freedelivery89 ya Tiktok yenye wafuasi zaidi ya 40,000 inayouza samani mbalimbali huku ikitapeli watu.
Ili kubaini ukweli, tulinunua bidhaa kutoka kwenye akaunti hii. Mmoja ya waandishi wetu akiwa Dar es Salaam Novemba 15, 2025 aliagiza stendi ya viatu (shoe rack) ambayo gharama yake ilikuwa ni Sh60,000 kulingana na muuzaji ilitakiwa kulipwa nusu ya gharama ya bidhaa ambayo ilikuwa ni Sh30,000 na baada ya siku mbili aliahidiwa bidhaa ingemfikia.
Kupitia akaunti hii ya freedelivery89 mwandishi wetu aliambiwa na mhusika alipie fedha kupitia namba ya simu +255 763 373 793 iliyokuwa na jina la Gerald Wilfred Luyagaza.
Ili aweze kuaminika, alieleza kuwa anapatikana Chanika Mwisho Mtaa wa CTC jijini Dar es Salaam kwa jina la Gerald Furniture kitu ambacho si kweli.
Baada ya kuona mzigo haufiki, mwandishi wetu aliamua kufunga safari hadi Chanika kumsaka mfanya biashara huyo bila mafanikio.

‘Maduka hewa’
Kwa kuwa baadhi ya wanunuzi wanapenda kununua bidhaa kwa wafanyabishara wenye anuani na maduka mitaani, matapeli hao pia wanaweka anuani bandia za “maduka yao” mtandaoni ili kuaminika zaidi lakini uchunguzi wetu umebaini kuwa biashara hizo hazipo katika mitaa wanayoeleza.
Kati ya biashara tano tulizotembelea Arusha, Mwanza na Dar es Salaam, nne hazipo katika maeneo halisi wanayodai biashara hizo zipo na hata watu wa karibu wala majirani wa maeneo husika hawazifahamu.
Hata tulipouliza majirani, viongozi wa Serikali za mitaa na wakazi wa mitaa hiyo wakiwemo bodaboda nao hawazifahamu au hawajawahi kuzisikia.
Miongoni mwa biashara hizo zisizoonekana jijini Dar es Salaam ni free delivery89 aliyesema yupo Chanika CTC, (Jumba la Pochi – Kariakoo), (Home Store store – (Goba Center), na Filber Store aliyedai anapatikana Kurasini.
“Katika eneo langu hakuna mtaa unaotambulika rasmi kwa jina la Chanika CTC. Tumekuwa tukipokea taarifa za utapeli ukiwemo unaotumia jina langu mwenyewe kama mtendaji jambo linalonipa changamoto kubwa mimi binafsi,” anaeleza Mtendaji wa Mtaa wa Chanika, Neida Kiduko.
Nukta Habari ilizunguka mitaa yote ya Chanika iliyopo kata ya Zingiziwa jijini Dar es Salaam kutafuta ofisi ya mfanyabiashara anayejulikana kama freederively89 bila mafanikio.
Pia Afisa Mtendaji wa Kata ya Zingiziwa, Abubakari Mahamudu Mussa, aemthibithibitisha kuwa hakuna eneo wala mtaa wa Chanika CTC hata anuani za makazi haioneshi uwepo wa eneo hilo.
Kwa upande wa Home Store Store waliodai wanapatikana Goba Center, Halmashauri ya Ubungo jijini Dar es Salaam, watu wote tuliowahoji wakiwemo madereva wa bodaboda wanasema hawalifahamu duka hilo wala hawajawahi kuliona.
“Tumefanya kazi hapa kwa muda mrefu, lakini hatujawahi kuona wala kusikia duka linaloitwa Home Store Store wala Home Kitchen store likifanya kazi hapa Goba Center,” anasema Seph Kibwana, dereva bodaboda wa Goba.

Picha ya Satilaiti ikionyesha eneo la Goba Centre jijini Dar es Salaam. Sehemu kubwa ya watu wanaoishi au kufanya biashara eneo hilo waliohojiwa na Nukta Habari wakiwemo bodaboda hawafahamu uwepo wa duka la Home Store_Stores. Picha|Google/Airbus.
Ni maumivu kila kona
Sehemu kubwa ya waliotapeliwa walipoteza fedha zao walizozitolea jasho huku wengine biashara zao zikiyumba kabisa.
Emmy Zuberi (30), mkazi wa jijini Arusha ameiambia Nukta Habari kuwa alitapeliwa Sh4 milioni kwa nyakati tofauti na wafanyabishara tofauti ndani ya kipindi cha mwaka mmoja, suala lilofilisi biashara yake na kumuacha katika maumivu makali.
“Nilikuwa nimeshajenga uaminifu kwa wateja, biashara ilikuwa inakua vizuri. Lakini baada ya tukio hilo, watu wameanza kuniona kwa wasiwasi, idadi ya wateja imepungua hata mtu akiniagiza basi tu anafanya kwa heshima ila anakuwa na hofu,” anaeleza Emmy anayeuza bidhaa mchanganyiko zikiwemo nguo na viatu.
Ukiachana na kupoteza mali, baadhi ya wanaotapeliwa huathirika kisaikolojia kiasi cha kuathiri shughuli zao nyingine za kiuchumi na kijamii.
Neema Edward, mwanafunzi wa chuo aliyetapeliwa na filber_store anasema, utapeli huo ulimfanya akashindwa kuzingatia masomo hususani wakati wa mitihani yake ya mwisho ya kumaliza shahada ya kwanza (UE).
“Ukitapeliwa lazima uchanganyikiwe maana bila msaada wa wazazi nyumbani kukulipia madeni ya wateja unaenda kufungwa maana mteja haelewi kwamba umetapeliwa yeye anachoelewa wewe ndio umemtapeli,” ameongeza Neema.
Inaendelea kesho.
Imeandikwa na Fatuma Hussein, Esau Ng’umbi (Dar es Salaam), Lucy Samson (Arusha) na Mariam John (Mwanza). Usanifu: Daudi Mbapani
1 thought on “Matapeli wanavyopora mamilioni ya Watanzania mtandaoni – 2”
Leave a Reply
Latest
Huyo anaetumia no. Yenye jina Aisha Omar Yahaya alishawahi kunitapeli mwezi januari 2025,muda huo nilikuwa form 5 Azania SS na nilikuwa nimesave pesa kiasi Cha 250000
Ili ninunue simu,niliona tangazo lake Instagram anauza simu,matokeo yake nikishawishika na kutumia hela lakini mpaka leo alikata mawasiliano na sikufanikiwa kumpata niliporudi hii kitu ili niaffect kwenye kwa mda mrefu nilikosa motisha ya kusoma na nkianguka kimasomo mpaka ,lakini kwa sasa pia nipo kwenye Sakata jingine la jamaa Moja anaitwa Dani yeye ana ofisi yake ipo riverside dar es salaam no. Yake ni 0760096776
Jina la ofisi ni wakaka simu tz,ipo njia ya kwenda mchichani huyu jamaa nimenunua simu kwake mwezi wa Saba 2025 baada ya kujikusanya Tena,simu aina ya iphone x kwa bei 250000 matokeo yake alinipa simu mbovu mara mbili na baada ya hapo m nilirudisha zote huo huo mwezi wa Saba nilikuwa narudi bweni shule sio mda mrefu akahidi kuwa atakamilisha hivi karibuni kabla sijaend shule lakini tang kipindi hicho nimekuwa nikipewa ahadi njoo kesho au wiki ijayo au baada ya wiki mbili,mara ananiblock , nasikitika kusema nmetoroka shule mara nyingi kwenda riverside ofisini ila bila mafanikio yoyote,alinipa visimu viwili vidogo 2 kwa sababu nilimwambia Sina chombo Cha mawasiliano,hapa huyu jamaa amekuwa akitumia advantage ya Mimi kuwa boarding school,Kama kunitapeli ili aweze kula hela yangu Bure,nimepambana sana lakini bado huyu jamaa amekamia kweli kunitapeli sa hvi nlitoka shule mwezi wa 12 2025 na yeye alivoona hvo alikimbia mji na kupotelea mkoania ofisini akiacha m2 mwingine anasubiria nirudi shule na yeye ndo arudi mjini afanye biashara zake mi ale hela yangu kiukweli hili jambo mi limeniuma Kama la mwanzoni Sina amani na nguvu hata ya kusoma hii ni aina nyingine naomba hili jamani lifanyiwe kazi haya mambo yanaathiri jamii hasa si wanafunzi na mwisho tunaumia,Francis Form 6 Azania ss