Bei ya petrol, dizeli yapaa miezi minne mfululizo

April 2, 2025 10:51 am · Lucy Samson
Share
Tweet
Copy Link
  • Petroli inauzwa kwa Sh3,037, dizeli kwa Sh2,936.
  • Yapaa mara nne mfululizo.

Arusha. Ni maumivu juu ya maumivu kwa wamiliki wa vyombo vya moto nchini baada ya bei ya mafuta ya petroli na dizeli kwa mwezi Aprili kupaa ikiwa ni mara ya nne mfululizo tangu mwaka 2025 uanze.

Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Aprili 2, 2025 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya petroli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imepaa kwa Sh41 huku dizeli ikipanda kwa Sh51.

Kuongezeka kwa bei hiyo kutawafanya watumiaji wa mafuta kupitia bandari ya Dar es Salaam kununua lita moja ya petroli kwa Sh3,037, dizeli kwa Sh2,936 na mafuta ya taa Sh3,053.

Tangu kuanza kwa mwaka 2025 watumiaji wa mafuta ya petroli na dizeli wamekuwa wakitoboa mifuko yao ili kununua nishati hiyo ambayo imekuwa ikipanda kwa miezi miezi minne mfululizo.

Mwezi Machi watumiaji hao walinunua petroli kwa Sh2,996 na dizeli kwa Sh2,885 iliyoongezeka kwa wastani wa Sh176 na Sh182 mtawalia kutoka kiwango kilichorekodiwa Februari.

Kwa upande wa mwezi Februari petroli ilinunuliwa kwa Sh 2,820 huku dizeli ilinunuliwa kwa Sh 2,703 iliyoongezeka kutoka bei ya Sh2,793 kwa petroli na Sh2,644 kwa dizeli.

Kwa mujibu wa taarifa za Ewura za Januari hadi Machi kupaa kwa bei hiyo kulichangiwa na kuongezeka kwa bei za mafuta katika soko la dunia na kuongezeka kwa gharama za uagizaji wa nishati hiyo.

Hata hivyo, kwa Mwezi April Ewura imesema bei ya mafuta katika soko la dunia na gharama za uagizaji zimepungua ukilinganisha na ilivyokuwa katika miezi iliyopita.

“Bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 6.92 ya kwa mafuta ya petroli, asilimia 6.57 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 7.82 kwa mafuta ya taa mtawalia…

…Kwa mwezi Aprili 2025, gharama za uagizaji mafuta (premiums) zimepungua kwa wastani wa asilimia 6.08 kwa mafuta ya petroli, asilimia 7.09 kwa mafuta dizeli na imeongezeka kwa asilimia 1.11,” imesema taarifa ya Ewura.

Kwa upande wa mafuta yanayoingia kwa bandari ya Tanga Petroli inauzwa kwa 3,083, dizeli Sh2,982 na mafuta ya taa Sh3,099 huku mkoani Mtwara wakinunua petroli kwa Sh3,109 na dizeli kwa Sh3,008

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *

Enable Notifications OK No thanks