Bei ya petroli,dizeli yapaa Serikali ikiweka ruzuku ya Sh259
- Bei ya rejareja ya petroli kwa mwezi huu itakuwa Sh4,115 kwa lita dizeli itauzwa kwa Sh4,248 kwa lita.
Dar es Salaam. Watumiaji wa vyombo vya moto nchini Tanzania wameendelea kushuhudia ongezeko la bei ya mafuta ya petroli na dizeli licha ya Serikali kutoa ruzuku ya Sh259 kwa kila lita ili kupunguza maumivu zaidi kwa watumiaji wa dizeli.
Ongezeko hilo liloanza kushuhudia mwanzoni mwa Machi, 2026 limewafanya watumiaji wa nishati hiyo kutoboa mifuko yao karibu mara mbili au zaidi ya ilivyokuwa mwanzoni mwa Januari, Februari na miaka ya nyuma.
Taarifa ya Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (Ewura) iliyotolewa usiku wa kuamkia Aprili 6, 2026 inabainisha bei ya rejareja ya petroli kwa mwezi huu itakuwa Sh4,115 na dizeli Sh4,248 kwa lita.
Bei hizo zinazotumika jijini Dar es Salaam zimeongezeka kwa wastani wa Sh295 kwa petroli huku dizeli ikiongezeka kwa Sh442 kulinganisha na bei ya Sh3,820 na Sh3,806 mtawalia iliyotumika mwezi uliopita.
Kwa ongezeko hilo jipya, Sh10,000 kwa sasa itanunua lita 2.43 za mafuta ya petroli ikilinganishwa na lita 3.49 zilizopatikana Machi 4, 2026, wakati lita moja ya petroli ilikuwa Sh2,864.
Kwa lugha rahisi unaweza kusema kupanda huko kwa mafuta kumepunguza karibu lita 1.06 ya petroli kutoka kiwango kilichokuwa kikipatikana mwezi uliopita.
Ahueni kiduchu watumiaji wa dizeli
Huenda bei ya dizeli ingeongezeka zaidi kama Serikali isingeweka ruzuku ya Sh259 ambayo imekuwa likipigiwa chapuo na wadau mbalimbali nchini.
Ruzuku hiyo imekuwa ikitekelezwa mara kwa mara pale bei ya nishati hiyo hupaa ili kutoa ahueni kwa watumiaji, mathalan mwaka 2022 Serikali iliweka ruzuku ya Sh100 bilioni baada ya kupaa .
Bei elekezi ilitoka kutoka Sh2,969 hadi Sh2,886 kwa petroli na dizeli kutoka Sh3,125 hadi Sh3,083.
Maumivu ya bei mpya ya mafuta kwa mwezi Mei yatawagusa hadi wanaotumia usafiri wa umma ikiwemo daladala, pamoja na wananchi wa kawaida wanaotegemea bidhaa na huduma zinazotumia nishati hiyo katika usafirishaji.
Profesa wa Uchumi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Abel Kinyondo aliiambia Nukta Habari hivi karibuni kuwa kupanda kwa bei ya mafuta kunaweza kusababisha mfumuko wa bei ya bidhaa zingine kutokana na kupanda kwa gharama za uzalishaji na usafirishaji unaoendeshwa na nishati hiyo.
Kwa mujibu wa Ewura kupanda kwa gharama hizo kumetokana na vita inayoendelea katika eneo la Mashariki ya Kati, iliyoanza Februari 28, 2026, ikihusisha nchi za Marekani, Israeli na Irani.
Vita hiyo imeharibu miundombinu ya uzalishaji na usafishaji wa mafuta, na kupunguza upatikanaji wa bidhaa hiyo duniani, hivyo kusababisha bei kupanda kulikochangiwa zaidi na kufungwa kwa Mlango Bahari wa Hormuz unaopitisha karibu asilimia 20 ya mafuta duniani.
Pamoja na hayo, Kupungua kwa mzunguko wa meli na msongamano uliotokana na kufungwa kwa njia hiyo kumesababisha ucheleweshaji wa mizigo na kuongeza zaidi bei ya mafuta katika soko la dunia.
“Bei za mafuta yaliyosafishwa katika soko la Kiarabu ziliongezeka kwa asilimia 71, 117 na 122 mwezi Aprili 2026 kutoka wastani wa dola za Marekani 71.76 kwa pipa, dola 85.99 kwa pipa na dola 85.34 kwa pipa mwezi Februari 2026 kwa petroli, dizeli na mafuta ya taa, mtawalia…
…Mwezi Mei 2026, gharama hizo kwa bidhaa za mafuta zilizopokelewa kupitia Bandari ya Dar es Salaam ziliongezeka kwa wastani wa asilimia 6.2 kwa petroli, asilimia 5.4 kwa dizeli, na asilimia 7.2 kwa mafuta ya taa.” imesema taarifa ya EWURA.
Serikali kupitia EWURA imesema inaendelea kuchukua hatua mbalimbali kuhakikisha mafuta yanapatikana nchini wakati wote pamoja na kudhibiti athari za kiuchumi na kijamii zinazoweza kujitokeza kutokana na kupanda kwa bei hizo.
Latest