Petroli yashuka, dizeli yaongezeka kiduchu baada ya kushuka miezi mitatu mfululizo
- Yaongezeka kwa Sh10 baada ya kushuka kwa stani wa Sh56 miezi mitatu iliyopita.
- Petroli yashuka kwa Sh34
Arusha. Kwa watumiaji wa vyombo vya moto vinavyotumia mafuta ya dizeli huenda wakauanza mwezi Agosti kwa maumivu baada ya bei ya mafuta ya dizeli kuongezeka kwa Sh10 kwa lita.
Maumivu haya yanakuja baada ya ahueni ya miezi mitatu kuanzia mwezi Mei mwaka huu ambapo bei ya nishati hiyo imekuwa ikishuka mfululizo kwa wastani wa Sh 56.3
Taarifa iliyotolewa na Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji Tanzania (Ewura) leo Agosti 6, 2025 inabainisha kuwa bei ya rejareja ya dizeli iliyoingizwa kupitia bandari ya Dar es Salaam imepaa kwa Sh10.
Kwa kiwango hicho, watumiaji wa mafuta kupitia bandari ya Dar es Salaam watanunua lita moja ya dizeli kwa Sh2,777, kupitia bandari ya Tanga Sh2,839 na kupitia bandari ya Mtwara Sh 2,870.
Kwa mujibu wa Ewura bei ya dizeli imepaa kwa mwezi Agosti kutokana na kuongezeka kwa gharama za mafuta yaliyosafishwa (FOB) katika soko la Uarabuni.
“Katika bei kikomo kwa Agosti 2025, bei za mafuta katika soko la dunia zimepungua kwa asilimia 2.3 kwa mafuta ya petroli, zimeongezeka kwa asilimia 5.5 kwa mafuta ya dizeli na asilimia 3.7 kwa mafuta ya taa” imesema taarifa ya Ewura.
AIdha, Ewura imefafanuakuwa gharama za kuagiza mafuta (premiums) katika Bandari ya Dar es salaam zimepungua kwa wastani wa asilimia 12.43 kwa mafuta ya petroli, asilimia 3.11 kwa mafuta ya dizeli na kuongezeka kwa asilimia 13.08 kwa mafuta ya taa katika Bandari ya Tanga hakuna mabadiliko.
Ahueni kwa watumiaji wa petroli
Wakati bei ya mafuta ya dizeli ikiongezeka kwa Sh10, bei ya petroli imeendelea kushuka kwa miezi minne mfululizo tangu Mei, 2025.
Bei ya bidhaa hiyo inayopitia bandari ya Dar es Salaam kwa mwezi Agosti imefikia Sh2,843 kwa lita, kupitia bandari ya Tanga Sh 2,904, na bandari ya Mtwara Sh 2,935.
Mwezi Mei bei ya Petroli ilishuka kwa Sh90 kutoka Sh3,037 iliyotumika mwezi Aprili, 2025 hadi Sh2947, bei hiyo ilishuka tena kwa Sh 62 mwezi Juni ambapo iliuzwa Sh2,885 kisha ilishuka tena Sh 8 mwezi Julai ambapo iliuzwa Sh2,877.
Pamoja na kushuka kwa bei hiyo nchini bado wakazi wa Kyerwa (Ruberwa) ndiyo wanaonunua mafuta hayo kwa bei ya juu zaidi ya Sh3,115 kulinganisha na wakazi wa maeneo mengine ikiwemo Dar es Salaam.
Latest



