YouTube waja na programu mpya kwa watengeneza maudhui

Joshua Stephen 0851Hrs   Septemba 25, 2023 Teknolojia
  • Ni YouTube Create.
  • Imeboreshwa zaidi kulinganisha na programu nyingine.
  • Inatarajiwa kuchochea ushindani na kuongeza ubunifu.

Dar es Salaam. Huenda hii ikawa habari njema kwa baadhi ya watengeneza maudhui duniani, baada ya mtandao wa kupakia maudhui wa YouTube kutangaza ujio wa programu tumishi kwa ajili ya kazi hiyo

Kikawaida wazalishaji wa maudhui hutumia programu mbalimbali kama InShot, CapCut, au TikTok kutengeneza maudhui na kisha kuyapakia katika mitandao ya kijamii ikiwemo YouTube ambao ndio mtandao maarufu zaidi.

Programu hiyo waliyoipa jina la YouTube Create inatarajiwa kuleta ushindani na kuchochea ubunifu kutokana na kufanyiwa maboresho zaidi kulinganisha na programu zilizopo.

Soma zaidi : Maboresho mapya ya WhatsApp Business kurahisisha biashara za mtandaoni

Septemba 21, 2023  Youtube kupitia tovuti yao pamoja na chaneli yao ya YouTube walitoa taarifa rasmi ya ujio wa programu hiyo na kubainisha kuwa itarahisisha utengenezaji wa maudhui ambapo mhusika ataweza kuichapisha moja kwa moja kwenye jukwaa hilo baada ya kukamilika.

“Tunajua mchakato wa kutengeneza video unaweza kuwa mgumu na mara nyingi humzuia mtayarishaji kupakia video yake ya kwanza Youtube, Ili kuratibu mchakato huu na kuruhusu mtu yeyote kuunda na kushiriki video moja kwa moja kwenye YouTube,” inasomeka sehemu ya taarifa hiyo.

Ni bure

Kwa sasa programu hiyo inapatikana katika soko la programu tumishi au ‘Playstore’ katika toleo la beta la Android toleo la 8.0 na kuendelea.

Aidha tofauti na programu nyingine ambazo ni lazima ulipie ili upate baadhi ya huduma, programu hiyo ni bure, na imeundwa ili kufanya utayarishasji wa video fupi au ndefu kuwa rahisi.

Soma zaidi : Rais Samia apangua vigogo TTCL, Tanesco, vilio vya umeme vikiendelea Tanzania

Ubora wa sauti 

Kama umerekodi video kwenye mazingira ya kelele au haisikiki vizuri, kwa kutumia programu hii ntumiaji ataweza kuboresha sauti na kuisafisha kwa kubofya ‘audio clean up’.

 Miungurumo ya mashine na uvumi wa upepo utakoma mara moja na sauti yako itasikika vizuri.

Tofauti na programu nyingine kama CapCut, watumiaji wanaweza kuongeza au kurekebisha sauti kwa kujirekodi na kuingiza sauti hizo bila kutumia data kutoka ndani ya programu jambo linapunguza muda na gharama kwenye ubunifu.

Itachechemua uzalishaji maudhui 

Wabunifu wanaweza kuongeza ladha na kuwezesha maudhui yao kufikia watazamaji wengi, kwa kuwa YouTube Create inamuwezesha mbunifu kuongezea video juu video nyingine yaani ‘picture in picture’. 

Video hizi zinaweza kutumika kutambulisha video zilizotangulia pamoja na kuongeza ubunifu katika uwasilishaji wa maudhui yako. 

Maudhui yako yanaweza kufikia watu wa jamii mbalimbali kwa kuongezea maelezo ya maandishi ‘subtitles’ au ‘caption’. 

Mtumiaji anauwezo wa kupakia faili la masimulizi ya lugha moja na kuchagua lugha nyingine unayotaka ionekane kwa maandishi.  

Soma zaidi : Tanzania yasaka Sh8 trilioni kukamilisha mradi SGR

Tovuti ya Zubtitle inasema kuwa ‘caption’ huongeza utazamaji wa video kwa asilimia 80 na watazamaji wanaweza kufuata kile kinachosemwa. Lakini pia husaidia kuongeza usikivu wa watazamaji na kuwafanya watazamaji waweze kutazama video hadi mwisho. 

Ashery Wilbard mtengeneza maudhui ameiambia Nukta Habari kuwa bado hajasikia lolote kuhusu YouTube Create, ingawa yeye hutumia zaidi programu ya CapCut kuhariri video kwa kuwa ni rahisi na anaweza kujazia sauti juu (voice over) yake. 

Hadi kufikia Agosti 2022, InShot kampuni ya uhariri picha na video imeendelea kuboresha programu hiyo kwa kuweka kipengele cha  ‘Green Screen effect' ambacho kinamuwezesha mtumiaji kutumia video nyingine kama ‘background’. 

Pia InShot waliongeza kipengele cha ‘Stabilize’ iliyosaidia kupunguza mwendo wa matukio na punguza kiasi cha kutikisika na kutia ukungu kwenye video.

Je ujio YouTube Create inaweza kufua dafu mbele ya programu maarufu za kuhariri video kama Inshot na CapCut? Unaweza kutoa maoni yako kupitia newsroom@nukta.com na 0677 088 088

Related Post